Lakini wakubwa hili la watu kufanya biashara tofauti kabisa na taaluma zao mnalionaje? Kuna Profesa wa Botany namfahamu anamiliki club ya pombe na bendi ya mziki wa kizaire. Profesa mwingine wa uhandisi anaendesha genge la kiti moto, ugali na bia! Yuko profesa wa surgery nilikuwa napishana naye kila siku jioni amebeba makombo ya ugali na wali na maganda ya viazi kwenye pick up yake, alikuwa anapita kuyakusanya kwenye majiko ya vyuo Muhimbili, IFM, CBE na DarTech na kwenye mabanda ya chipsi, kwa ajili ya kupeleka nyumbani kwake kulishia nguruwe. Mwingine alikuwa katibu mkuu wa chama kikongwe kwa miaka kumi, sasa analima viazi kijijini kwao kwa jembe la mkono, lilelile alilokuwa anaimba kwenye sera za chama chake kuwa halina tija, na kuwa chama hicho kingewakomboa wakulima waondokane nalo! Yuko mama mmoja alikuwa mkuu wa wilaya na baadae RDD (siku hizi inaitwa RAS), aliwahi kunitia msukosuko nilipokuwa mwalimu kwenye wilaya yake kwa kosa la kumwadhibu mwanae aliyekuwa anavuta bangi, sasa hivi yuko Visiga ana kiunga cha mihogo na anafuga bata kwa kuwalisha ukoko wa wali anaobakisha, na yule mwanae mvuta bangi bado yupo na ni mtu mzima lakini anamwibia mama yake kila siku! Biashara anayofanya huyo ex-DC: kusuka mikeka na nyungo na kuzipanga barabarani kusubiria wateja!
Na leo tumeambiwa RPC analima mananasi na kufuga nguruwe! Halafu akistaafu atakuwa anaendesha hoteli yake na wenzie (sijui atakuwa mkurugenzi au nani!), lakini nawaza hiyo hoteli yake itakavyoweza kutofautiana na Police Mess!
Mshangao wangu: Kwa nini hawa watu wasifanye biashara katika mambo ambayo wana uzoefu nayo, uwezo zaidi, na credibility? Wenzetu wa nchi zilizoendelea wakistaafu madaraka kama hayo wanatumia uzoefu wao katika ngazi za ushauri, na wanalipwa vizuri sana. Mfano ukitembelea ofisi za Security consultants utakuta ni mashushushu na maaskari wastaafu, na wakikufanyia consultancy ni uhakika! Watu wenye uzoefu wa utawala, uongozi, biashara, kilimo, elimu, sheria, usalama n.k. wanaanzisha firms za consultancy ambazo uzoefu wao pekee kabla hata ya elimu ya darasani ni credibility tosha ya kuwauzia ushauri watu wanaouhitaji, na wanakula kiulaini bila kugombana na watu kwenye hizi biashara ndogondogo! Na hata kama ni biashara kubwa, kama si fani yako itakushinda tu, labda ukodishe kwa mjasiriamali uwe unachukua tu mafao mtayokubaliana.
Nashangaa hivi, kwa nini watu wakubwa tu wenye uzoefu wa mambo yao makubwa mazuri, wanarudi kuzunguka palepale kwenye biashara za genge, viazi, kitimoto, kulima nanasi, kuuza juisi na barafu nk, kwa nini? Kwa nini wanarudi kwenye hatua ambazo kimsingi walipaswa wawe wameshazivuka? Nini kinawarudisha huko?