Upinzani wa kweli utapatikana tu pale wapinzani wote watakapojitambua kwamba ni wapinzani! Kuanzisha vyama lukuki wala hakutaisaidia nchi hii. Vitaanzishwa vingi lakini mwisho wa siku waanzishaji wanaishia kuwa wachumia tumbo, kila mtu na chake. NRA, UMD, NLD, UPDP, TADEA, Demokrasia Makini, FORD, CHAUSTA, TPP, nk vipo wapi?
Kama kweli wapinzani wote wana dhamira moja kwa nini wasijipange wakaungana na kuwa kitu kimoja.
CHADEMA walijifanya vipofu eti peke yao ndio wapinzani, wakiamini ya kwamba wao tu ndio wanaweza kuleta upinzani wa kweli na kutwaa dola; wakawaona wapinzani wenzao si kitu. Wakajimilikisha upinzani.
Leo naona wanazinduka na kuona kwamba wanawahitaji wenzao. Huo pia ni unafiki au kukosa maono. Kwa hiyo hawakufikiri mwanzo kwamba wanawataka wenzao au wanawaghilibu tu?
Ghiliba, ubinafsi, uzandiki, utumiwaji na uroho unavimaliza vyama vya upinzani nchini.
Utungaji wa Katiba mpya ni fursa mujarabu ya kuupatia upinzani nguvu lakini naona kama wanataka kuimwaga hii fursa.
Wakati tunadai katiba miaka ile ya 1990 (wengi wa UKAWA hakuwepo labda Mbatia wakati huo akiwa kijana mdogo na Mabere Marando) tukiongozwa na akina Mabere, Mapalala, Kasanga Tumbo nk hatukuwa tunadai serikali tatu sisi wengine tulikuwa tukidai vyama vingi, Tume Huru ya Uchaguzi, Haki za Binadamu kuidhinishwa kinagaubaga kwenye Katiba na kuhimizwa kutunzwa kwa mujibu wa Katiba pamoja na Rais wa Jamhuri kupunguziwa Madaraka lukuki aliyonayo kwa sasa. Mtikila yeye pamoja na hayo alikuwa akiidai Tanganyika na wala si serikali tatu; bali kila nchi iwe kivyake.
Leo tunakuja kuibua suala la Serikali tatu na linakuwa ndilo suala kuu, tumesahau masuala hayo muhimu. Kwa kulazimisha serikali tatu, tunataka kukosa fursa hizi nyingine ambazo ni muhimu kufika tunakokutaka.
Tupate Tume huru, twende kwenye uchaguzi, wapinzani kama wana nguvu ya kushinda kwenye uchaguzi huru na wa haki washinde. Baada ya hapo wakiwa madarakani basi waangalie muundo wa serikali wanaoutaka, si basi.
Kama CCM wanakwamisha serikali tatu, tupate Tume Huru, uchaguzi uwe huru, wapinzani washinde CCM wawe pembeni, turudi kwenye muundo wa serikali, hapo sasa tutaamua kama ni moja, mbili ama tatu! Kwisha. Lakini hili la kukimbia kwa sababu ya suala la muundo wa serikali na kuachana na fursa muhimu ambazo tumekuwa tukizipigania miaka nenda rudi, naona ni usaliti vilevile.
Tupate Katiba itakayoruhusu vyama kuungana na kuingia kwenye uchaguzi kama wenzetu Wakenya wanavyofanya. Tupate Katiba ambayo ukianzisha chama hata baada ya wiki moja uruhusiwe kwenda kwenye uchaguzi, tupate Katiba inayoruhusu mgombea binafsi ili kuepukana na udikteta wa vyama. Hawataki!!! Wanataka serikali tatu, kama hazipo tukose fursa hizo nyingine ambazo ni muhimu!!!