Kazi ya udereva aliomba kwa unyenyekevu, mathalani walikuwapo wengi, ila kwa hila na fitina wengine walitemwa na kupewa yeye hilo lori , kwa spana na bisibisi akaingia na wengine wakimshangilia kwamba yeye ni simba wa nyika na kwamba amefuzu Rally. Abiria tunatia huruma sana, nyuso zimekosa upako na mashavu yametudorora kama utumbo wa mbuzi. Baadhi ya ndugu zake wa ukoo mmoja na makenika wake aliopanda nao kituoni pale wameanza kuhofia pia iwapo hata rejeta kama ina maji. Baadhi ya mafundi alioingia nao hawaeleweki nyuso zao na wapo abiria wanaolalamika kwamba wengine sio mafundi kweli, wamefoji ustadi, lakini nani anajali ?
Matairi yameota matege, taa zimekwaa makengeza na nafsi zimevimba kwa mdondo wa mawazo tuliyo nayo. Matapishi yamelifanya gari lizidi kunuka kwa ndani lakini kila kelele tunayopaza ni ama dereva au makenika wake wengine alioingia nao watakukamata na kukupiga ngoto.
Ramani yetu haikuonyesha njia hii, kadi ya gari ilionyesha namna ya uendeshaji na masharti ya kuzingatia, lakini wanatung'ong'a. Midomo imebabuka na visogo vimetoka nywele kwa upepo. Tunapokwenda siko lakini mingurumo ya simba na harufu ya tairi vinanipa wasiwasi itakuwaje kama tutaishiwa mafuta katikati ya nyika?
MUNGU BARIKI SAFARI YETU LABDA IPO SIKU DEREVA WETU ATASIKIA KILIO CHETU