Abdul Nondo: TAMISEMI haipaswi kusimamia uchaguzi, haitotenda haki

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Fuatilia yanayojiri kwenye Siku ya pili ya Mkutano Maalumu wa vyama vya Siasa, leo Septemba 12, 2023.


Mpaka leo msimamo wa Serikali ni kana kwamba uchaguzi wa Serikali za miktaa unakwenda kusimamiwa na TAMISEMI. TAMISEMI ambayo waziri wake anatoka chama cha mapinduzi na anatoka Serikalini. Nakwenda kusimamia uchaguzi ambao sisi tunataka uchaguzi huo uwe wa haki na uchaguzi wa amani lakini Waziri kutoka TAMISEMI ndio anakwenda kusimamia huo uchaguzi. Yatafanyika yaliyofanyika mwaka 2019.

Pendekezo na ushauri wetu ni kwamba hili tuliangalie, kama kweli tunataka tudumishe amani, kama kweli tunataka tuwe na amani yetu, tuhakikishe tunakuwa na mifumo imara ya kitaasisi.

Uchaguzi wa Serikali za mitaa usisimamiwe na TAMISEMI. Uchaguzi wa Serikali za mitaa uwepo katika sheria ya uchaguzi. Wamesema kuna muswada wa sheria ya uchaguzi ambao unapaswa kupelekwa oktoba na novemba, tunataka katika sheria hiyo uchaguzi wa Serikali za Mitaa uwepo kwenye hiyo sheria ya uchaguzi na sio sheria ya Serikali za mitaa.

Tukifanya hivyo tutakuwa na uchaguzi unaopaswa kusimamiwa na tume ya uchaguzi na sio TAMISEMI.

Ni muhimu tuwe na ratiba ya utekelezaji, mfano Zanzibar katika Maridhiano yaliyokuwa yanafanyika Zanzibar kulikuwa na ratiba ya utekelezaji. Tunapokutana hapa tunajadili bila Serikali kutuambia ratiba ya utekelezaji ni ipi tutakuwa hatufanyi jambo lolote la msingi.

Demokrasia ndio inaleta amani, nchi zenye demokrasia hawapigani, demokrasia inakuja kwa misingi imara ya kitaasisi, tunataka misingi imara ya kitaasisi ili tufanye uchaguzi huru na wa haki.

TAMISEMI haipaswi kusimamia uchaguzi, haitotenda haki, kutakuwa na post election violence, tutapigana hapa kwa makosa ambayo tunashindwa kuyasahihisha sasa hivi.

IVAN MAGANZA, MWENYEKITI WA VIJANA, TLP TAIFA
Demokrasia ndani ya vyama vya siasa haipo, vijana na wanawake wanakatishwa tamaa ndani ya vyama vyao. Ndani ya vyama ya siasa kuna unyanyasaji mkubwa sana kwa makundi ya vijana na wanawake.

Mfano hai ni chama changu TLP, nafanya kazi za chama tangu Mrema aondoke. Nimekuwa napigwa vita hadi watu wananipigia simu, mwenyekiti mbona unapitia misukusuko hivi? Kweli siasa ndo ya kuingilia kwa vijana?

Ofisi ya msajili umulike hivi vyama kwa wanawake na vijana. Demokrasia iimarishwe ndani ya vyama ili wananchi wanapoona waone haja ya kushiriki uchaguzi.

JOSEPH SELASINI, MWENYEKITI WA CHAMA CHA NCCR MAGEUZI
Namshukuru Rais kuunda Kikosi Kazi. Kikosi Kazi hiki kilikuwa kinalalamikiwa sana; nashukuru Mungu sikuingia kwenye huo mtego.

Utamaduni wa Watanzania kukaa pamoja katika jambo ambalo ni zito ili tulijadili pamoja, ni jambo zuri sana.

Ni ngumu sana kwa mtu mwenye uchumi mdogo kushinda Uchaguzi Tanzania. Wanaoshinda asilimia kubwa ni Watu wenye uwezo mkubwa kifedha. Tunaomba tuanze kufanya chaguzi za gharama ndogo ili kuwasaidia wenye uwezo mdogo kifedha kupata nafasi

Watu wa makundi maalum wataingiaje kwenye uchaguzi wakiwa hawana uwezo?

Wakati tukiangalia namna ya kuyasaidia haya makundi maalum, tuangalie namna ambayo tutafanya uchaguzi huu usiwe uchaguzi wa gharama kubwa, ili tuwawezeshe wale wenye uwezo wa kuiongoza waingie kwenye uchaguzi na wapate hiyo nafasi

DOMINATA RWECHUNGURA, MAKAMU MWENYEKITI -TLP
Ili amani iwepo, ni lazima iendane na haki. Haki, Uwazi, Uwajibikaji – vyote vinatengeneza amani.

Ili tuendelee kuwa na amani, tutafiti masuala ya pesa kwenye uchaguzi. Kwenye chaguzi tunaingia watu wenye uwezo tofauti. Hiyo ni sawa na uwanjani wengine wataingia na viatu, wengine pekupeku.

NDONGE SAID NDONGE, MWENYEKITI WA CHAMA CHA AAFP WALEMAVU
CCM waache kufanya Demokrasia ya Ubaguzi ya kukaa na Vyama walivyovikosea peke yake badala yake wakae na Watu wa Vyama vyote vya Siasa kutafuta muafaka na maridhiano

Tangu Uhuru nyie tu hamchoki kuongoza CCM? Achieni wengine pia Madaraka. Watu hawajitokezi kupiga kura kwa sababu wanajua tukienda kupiga kura CCM itashinda na tusipoenda kupiga kura bado CCM itashinda

Niwaambie CCM kuwa hata kuongozwa ni uzalendo; uzalendo gani wewe kuongoza kila siku tu? Mnahitaji kujitathmini.

YASSIN MOHAMED – M/KITI NGOME YA WAZEE – ACT
Kwenye makabrasha tunaona Demokrasia na Amani, lakini haya yote hayawezi kufanyika ikiwa hakuna Haki. Haki ndiyo inayoanza. Vurugu unazozisikia huko nje ni kwa sababu ya kukosekana kwa haki. Haijalishi tuna sharia gani au katiba gani, ikiwa haki hakuna, vyote havipo!

Ili Rais apate nishani ya kuaminika, lazima ahakikishe uchaguzi unakuwa wa haki. Walioshinda watangazwe. Walioshindwa wasitangazwe [kama washindi].

Mchakato [wa uchaguzi] huu unaingiliwa mpaka na polisi ili kuhakikisha CCM inashinda. Kwa macho yangu nimeshuhudia vyombo vya usalama vikiingilia mchakato na watu wengi wamepata matatizo makubwa walipotoa kauli zao.

ESTHER SEMANYA, KAIMU M/KITI WA WANAWAKE TAIFA - NCCR-MAGEUZI
Nilishuhudia uchaguzi mmoja Kinondoni mwaka 2015 mgombea mmoja ambaye hakushinda alitangazwa kuwa mshindi kisha baada ya hapo akapandishwa kwenye gari la polisi na mabomu yamachozi yakapigwa. Polisi hawawezi kufanya uchafuzi wa namna hiyo bila kupata maelekezo ya kiongozi fulani kutoka TAMISEMI. Ombi langu ni tuwe na siasa zenye tija.

KEVIN NYAMORI – M/KITI WA DIASPORA CLUB
Wapiga kura hawapati nafasi ya kuwajua vizuri wagombea kwani muda unaotolewa na Tume ya Uchaguzi ni usiozidi miezi miwili. Kuna wachache wataweza kufanya hizosiasa na kujitangaza kwa wapiga kura.

Mtu akitangaza leo kuwa ana nia ya kugombea urais mwaka 2025 itamuathiri vipi rais aliye madarakani? Kukiwa na uwezo wa kufanya hivi itasaidia vyombo vya usalama na vyombo vya habari kumchunguza huyu mtu na kuwanika. Kama atakuwa ana mabaya, basi itakuwa ni sifa kwake. Kama atakuwa ana mabaya, basi atajitathmini sababu ya muda mrefu ambao watu wamemfuatilia na kumwelewa vizuri.

Tume ya Uchaguzi itoe muda kuwa mtu wakati wowote aoneshe nia kuwa yeye anataka kugombea nafasi fulani. Hii itasaidia wananchi kumjua mgombea vizuri – mazuri na mabaya yake.

SALAMA JUMA, M/KITI WANAWAKE WA CCK
Mimi nitaongelea Rushwa. Mimi imeshawahi kugombea; unakwenda mahali unaitisha mkutano, watu wanakuja vizuri unaongea nao, unahutubia unanadi sera vizuri, wanafurahi. Ukishashuka jukwaani, wanakufuata wanakuuliza, “sasa unatuachaje?”

Sasa ukiwauliza nawaachaje vipi, wanasema wenzio wanatuachia sukari, wengine wanatuachia chumvi sijui na vitu gani. Kwakweli hili ni tatizo mpaka vijijini, si tu mjini. Ni tatizo la Watanzania wote! Hakuna cha asiyejua kusoma wala anayejua kusoma, mjinga wala mjanja – wote wanadai Rushwa.

Wapiga kura waelimishwe waache kudai rushwa.

SHEIKH JALALA, JUMUIYA YA WASHIA TANZANIA
Tunahitaji demokrasia ambayo haitaharibu mila zetu, desturi zetu, tamaduni zetu za Kitanzania ambazo nitamaduni nzuri.

Leo tuna tatizo kubwa la kimaadili. Tuna changamoto kubwa ya ushoga. Tuna changamoto kubwa ya hili balaa zito na tatizo adhiim. Kwakweli linahitajia demokrasia yetu ya Kitanzania. Je, inaliruhusu jambo kama hili? Je, inalikubali jambo kama hili katika jamii yetu?

Pia tuliangalie jambo la dini. Tumekuwa ni raia wema. Tumekuwa ni watu tunaoelewana. Amani yetu inapigiwa mfano kila mahala, kwanini? Kwa sababu Watanzania Serikali yao haina dini ila Watanzania ni wana dini. Watanzania ni Wakristo, Watanzania ni Waislamu. Dini hii ndiyo sababu imetufikisha kupigiwa mfano. Kwahiyo tunapokwenda, demokrasia yetu iheshimu misingi hii ambayo imeifanya Tanzania ni kisiwa cha amani hadi leo.

NEEMA LUGANGIRA, MBUNGE WA VITI MAALUM (CCM)
Wenyekiti wa vijiji 11,669, wanawake ni asilimia 2.1 peke yake. Wenyeviti wa Vitongoji wanawake ni aslimia 6.7 tu. Kwa maana kwamba kati ya wenyeviti wa vitongoji 58,411, wanawake ni takribani 4,171. Tukija kwenye wenyeviti wa Serikali za mitaa, hivi sasa wanawake ni asilimia 12.6 tu. Kwa maana kwamba, kati ya wenyeviti wa serikali za mitaa 3,643, wanawake ni kama 528 tu.

Hiyo inaonesha katika ngazi ya serikali za mitaa namna ambavyo uwakilishi wa wanawake katika uongozi upo chini sana. Na tukirejea sensa hivi karibuni inaonesha kwamba wanawake ni zaidi ya takribani asilimia 51.

Tunapiomarisha demokrasia ni lazima tutambue uwakilishi wa wanawake ulivyo chini, na tuone namna gani ya kuboresha ushiriki huo.

Ndani ya Bunge, asilimia ya wanawake ambao ni wanawake wa majimbo ni asilimia 9.1 tu. Hii inaonesha ya kwamba tungekuwa ahatuna viti maalum leo, ina maana uwakilishi ndani ya bunge na sauti ya wanawake ingekuwa pia ipo chini.

Kwa muktadha huu wa hali ya kidemokrasia, mimi naomba sana tutambue kwamba hatuwezi kuwa na demokrasia sawia kama hatuzingatii suala la usawa wa kijinsia katika demokrasia.

ASKOFU BAGONZA
Jambo la kwanza, sisi ni wadau wa demokrasia. Tumekuja kutathmini utekelezaji wa Kikosi Kazi.

Kwangu mimi, kazi ya Kikosi Kasi ilikuwa ni kama mwendelezo wa kazi ya Tume ya Warioba. Tunavyokwenda mbele nahisi kama kuna mgongano baridi kati ya Kikosi Kazi na Kazi iliyofanywa na Tume ya Mzee Warioba. Ningeshauri zitafutwe njia za hekima kuondoa huo mgongano baridi. Maonin ya wananchi yalishakusanywa nchi nzima; Kikosi Kazi kilikusanya, Mzee Warioba alikusanya, tunahitaji kuunganisha kazi hii iwe moja na taifa liweze kusonga mbele kutoka kwenye huu mkwano.

Nihimize maboresho ya sheria yanayoenda kufanywa mwezi Oktoba yafanyike kwa uwazi ili tuondokane na legitimacy – yaani aliyeshinda anashangaa, aliyeshindwa anashangaa na waliosimamia wanashangaa.

CAMILLIUS KASALA, MKURUGENZI WA HUMAN DIGNITY - BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI
Kwanini tunapokuwa kwenye chaguzi zetu amani ya Tanzania inatikiswa?

Kwasababu tangu mfumo wa vyama vini ulipoanzishwa, ulianzishwa kwa kusitasita. Wengi walikuwa hawataki vyama vingi viwepo. Ni kama bado tunaendelea na mfumo wa demokrasia kwa shingo upande. Na ukifanya vitu kwa shingo upande hufanyi kwa moyo. Na sishangai mapendekezo ya tumen a vikosi kazi ya huko nyuma hayatekelezwi.

Pia, soma: Rais Samia: Hatukutoa fursa ya Mikutano ya hadhara watu wakavunje sheria, wasimame kutukana, kukashifu na kuchambua dini za wengine
 
Back
Top Bottom