Spika kitanzini
na Charles Mullinda
Tanzania Daima
NGUVU za Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa zinaelekea kuporomoka baada ya kambi yake kuu kuanza kumgeuka.
Sitta, ambaye mara kadhaa tangu aliposhika wadhifa wa Uspika amekuwa akijikuta katika migongano ya hapa na pale na wabunge na wananchi, amekuwa akiitegemea zaidi kambi ya wabunge vijana kumkingia kifua, wakiwemo wale wa kambi ya upinzani.
Kambi hiyo ya wabunge vijana, sasa imemgeuka Spika baada ya matukio ya hivi karibuni kuhusu uamuazi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kukata rufaa akilitaka Bunge lipitie upya adhabu ya kusimamishwa aliyopewa mwezi Agosti.
Baada ya kupokea barua ya mbunge huyo kuhusu suala hilo, Spika alikaririwa akimbeza Zitto na kusema kuwa anamuonea huruma kutokana na kuonyesha kwake (Zitto) kutokomaa kisiasa.
Zitto ni mmoja wa wabunge mahiri katika kambi ya wabunge vijana, ambao mara kadhaa wamelitikisa Bunge kutokana na hoja zao na pia, ingawa ni mbunge wa upinzani, amekuwa moja ya nguzo muhimu za Spika hasa kwa mahasimu wake wa kisiasa wa ndani ya chama chake.
Habari zilizolifikia Tanzania Daima Jumapili, zilieleza kuwa Zitto, amemuweka Spika Sitta katika wakati mgumu baada ya kuendelea na msimamo wake wa kutaka adhabu yake ipitiwe, licha ya kauli ya Sitta.
Ingawa jana katika mahojiano yake na gazeti hili alisema hataki kulumbana na Spika Sitta katika suala hilo kwa sababu anamuheshimu sana, Zitto aliendelea kusisitiza kwamba anachotaka ni haki itendeke kwa sababu anaamini adhabu iliyotolewa na Bunge dhidi yake haikuwa sahihi.
Ninamuheshimu sana Spika, sipendi kabisa kubishana naye, ninachokiomba ni haki itendeke kwa sababu ninaamini sikutendewa haki kwa kupewa adhabu ile, sijaridhika. Lakini kamati ikiketi na kupitia adhabu hiyo nitaridhika na maamuzi yake, alisema Zitto.
Aidha, akizungumzia madai kwamba alisambaza barua yake hiyo kwa vyombo vya habari na katika mtandao wa internet, jambo ambalo Spika amekaririwa akieleza kuwa ni kinyume cha taratibu za Bunge, Zitto alisema hilo si kweli kwa sababu alitoa nakala kwa kiongozi wa upinzani bungeni na kwa katibu wa Bunge tu.
Huku akiongea kwa kuchagua maneno, Zitto alisema kamwe hana nia ya kutumia nafasi hiyo kutafuta umaarufu. Sikutumia nafasi kujitafutia umaarufu kama inavyoelezwa, ningetaka hivyo ningezungumzia jukwaani, kwa sababu wakati naadhibiwa watu wengi walikuwa hawampendi Spika, hapo ndipo ningemchafua.
Ninasema kweli, ningetaka umaarufu ningekwenda mahakamani, nina orodha ndefu ya wanasheria wazuri wanaotaka suala hili nilipeleke mahakamani na wao watalisimamia ili haki ipatikane, lakini mimi nasema hapana, na tangu nilipoadhibiwa nilikuwa kimya, nimetumikia kifungo kimya, hiyo yote ni kwa sababu ya kumuheshimu tu Spika, ni unyenyekevu wa hali juu, alisema Zitto.
Inadaiwa kuwa msimamo huu wa Zitto na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Spika dhidi ya barua iliyoandikiwa na mbunge huyo, unaashiria kuwa Spika ana wasiwasi kuwa iwapo Kamati ya Kanuni za Bunge itaipitia upya adhabu hiyo, Bunge linaweza kujikuta matatani kwa kukiuka kanuni au desturi zake.
Wataalamu wa wafuatiliaji wa masuala ya Bunge waliozungumza na gazeti hili walieleza kuwa, Bunge linaendeshwa kwa kanuni na desturi ambazo huliongoza kufikia maamuzi yake, lakini katika kesi ya Zitto, vyote hivyo havikufuatwa.
Ukweli huu unathibitishwa na adhabu kadhaa zilizokwishatolewa na Bunge kwa wabunge ikiwemo aliyopewa aliyewahi kuwa Mbunge wa Temeke, Augustino Mrema baada ya kutamka bungeni kuwa serikali imepanga kumuua yeye (Mrema) na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharrif Hamad.
Mrema aliliambia Bunge kuwa habari hizo alipewa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa Imran Kombe. Bunge lilimpa Mrema siku tano za kuthibitisha maelezo yake, lakini alishindwa kufanya hivyo na kujikuta akiadhibiwa kusimama kufanya shughuli za Bunge kwa muda wa siku 40.
Baadhi ya wabunge walioadhibiwa kwa utaratibu wa kupewa siku za kuthibitisha kauli zao ni pamoja na Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa aliyetiwa hatiani kwa kuchezea taarifa za Bunge kuhusu sakata la fedha za matibabu zilizotumiwa na Hassy Kitine.
Mwingine ni Philemon Ndesamburo ambaye aliadhibiwa na Bunge baada ya kushindwa kuthibitisha kauli yake kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, aliwaambia wafanyabiashara wakitaka mambo yao yawanyookee, wajiunge na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa kuzingatia mlolongo huu wa matukio ya adhabu zilizokwishawahi kutolewa bungeni, kambi ya wabunge vijana imepanga kumshinikiza Spika kuiamuru Kamati ya Kanuni za Bunge kuipitia upya adhabu hiyo na kwamba matokeo yake yatachambuliwa ili kuona kama kamati hiyo inafanya kazi kwa kufuata haki.
Mmoja wa wabunge vijana kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Halima Mdee, alilieleza gazeti hili kuwa kambi ya wabunge vijana haikubaliani na msimamo wa Spika na inataka adhabu ya Zitto ipitiwe mpya kwa sababu hata Rais Jakaya Kikwete ameonyesha kwa vitendo kutokubaliana na adhabu hiyo.
Adhabu aliyopewa Zitto ilitokana na hoja yake ya kutaka mkataba wa Buzwagi uchunguzwe, wabunge wa CCM waliungana kumpinga kwa sababu wanazozijua na ambazo sasa Watanzania wengi wanazijua, wakamsimamisha.
Lakini ninaamini walimsimamisha kwa sababu za kiitikadi, ingawa mimi sikuwepo, hawa wamemsimamisha, rais kaunda kamati ya kupitia upya mikataba ya migodi ya madini ukiwemo huo wa Buzwagi, haijalishi hata kama kaunda kisiasa au kwa dhamira ya dhati, kinachoonekana hapo ni kwamba rais amekubaliana na hoja ya Zitto.
Na kama rais amekubaliana na hoja ya Zitto, maana yake ni kwamba adhabu aliyopewa na Bunge haikuwa sahihi, sasa Bunge linapaswa lijitizame upya, vinginevyo kulishitaki ni sawa tu.
Kwa Spika, kumuita mbunge mtoto ni jambo la ajabu sana kwa mtu tunayemuheshimu kama yeye, utoto wa mtu haupimwi kwa umri bali hoja zake, wanaomsikiliza Zitto akitoa hoja wanajua kama ni mtoto au la
katika hili atauona utoto wetu, alisema Halima kwa kujiamini.
Pamoja na hayo yoye, kivuli cha Rais Kikwete nacho, ambacho kimekuwa kikiyaandama maamuzi ya Spika, kinaonyesha kumuweka katika hali ngumu zaidi kwa vile kimekuwa kikipingana naye kila mara.
Kwa uchache, Rais Kikwete alionekana kutofautiana na Spika pamoja na wabunge mapema mwaka jana, pale walipokosoa madai yao ya nyongeza ya mishahara na marupurupu wakati taifa likiwa katika hali ngumu ya chakula na ukosefu wa umeme.
Kikwete pia ameonekana kutofautiana na Spika na wabunge wa CCM baada ya kuunda kamati ya kupitia upya mikataba ya madini, jambo ambalo lilikuwa likidaiwa na Zitto kabla ya kusimamishwa na wabunge wa CCM.
Wafuatiliaji wa masuala ya Bunge wanaeleza kuwa iwapo Spika Sitta hatatumia busara zaidi katika kutatua mgogoro huu na kambi ya wabunge vijana, na hivyo kusababisha kufarakana nao, atakuwa amebakia peke yake jambo ambalo ni hatari zaidi kwa siasa za hapa nyumbani.
Wengi wamemtaka akumbuke kazi kubwa iliyofanywa na wabunge hao, wakati wa sakata lake na Mbunge Malima, ambapo baadhi ya vigogo ndani ya chama chake waliamua kumshughulikia huku wakiwa na dhamira ya dhati ya kumuengua katika Uspika.
Sitta aliokolewa na kambi ya wabunge vijana, baada ya Mdee kuwasilisha hoja bungeni, akilitaka Bunge kumuadhibu Malima kwa kumdhalilisha mbunge na kiti cha Uspika, hoja ambayo iliua nguvu za wapinzani wa Spika na kumpa mwanya wa kukwepa mashambulizi yaliyokuwa yakielekezwa kwake.