Zitto Kabwe: Buriani Mzee James Mapalala, Wajibu umeutimiza

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,879
Buriani Mzee James Mapalala, Wajibu umeutimiza

Zitto Kabwe

James Kabalo Mapalala ametangulia mbele ya haki. Mwenyezi Mungu ndiye anajua amali zake duniani na yeye ndiye atampima kwa matendo yake. Lakini Mzee huyu alitimiza wajibu wake kwa sisi wanadamu tunaoishi Tanzania.

Mimi sikuwa karibu na Mzee Mapalala. Sikuwahi kufanya naye kazi isipokuwa kipindi kifupi cha mwaka 2014 katika Bunge Maalumu la Katiba. Hata huko Mimi sikupata nafasi ya kumjua kwa karibu kwani muda mwingi wa Bunge lile nilikuwa namwuguza Mama yangu Marehemu Hajjat Shida Salum. Sikupata bahati ya kumfahamu vema Mzee James Mapalala. Hata hivyo nikiwa mwanafunzi wa historia ya nchi yangu ambaye niliingia na kuendeleza vuguvugu la kudai na kujenga demokrasia ya vyama vingi nikiwa kijana mdogo wa miaka 17 nilimsoma Mzee James Mapalala.

Historia ya harakati za demokrasia nchini haiwezi kuandikwa bila ya kutajwa kwa James Mapalala. Alikuwa miongoni mwa Watanzania wa mwanzo kabisa kudai mfumo wa vyama vingi nchini. Aliandika barua kwa Mwalimu Nyerere ambayo ilimpelekea kufungwa kwenye vituo vya polisi mbalimbali bila ya kufikishwa mahakamani na hatimaye kuwekwa kizuizini. Katika umri wake wa miaka 83 aliyoishi duniani, miaka 6 aliipoteza akiwa kizuizini Mikoa ya Kusini mwa Tanzania na kisiwani Mafia. Mapalala ni moja ya Watanzania kadhaa walioteswa na sheria kandamizi zilizokuwepo Wakati wa Utawala wa Awamu ya kwanza na ya pili chini ya Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Ali Hassan Mwinyi. Sheria ya kuweka watu kizuizini ( detention ) ni moja ya Sheria ambazo Tume ya Jaji Nyalali kuhusu Mfumo wa Vyama vingi ilitamka kuwa ni Sheria mbaya. James Kobelo Mapalala alilipia miaka 6 ya uhai wake ili Watanzania wawe na Uhuru wa kisiasa. Gharama kubwa sana ambayo ni wachache walikuwa tayari kuilipa kwa faida ya Nchi yetu.

Mfumo wa vyama vingi ulipoanza Mzee Mapalala alishirikiana na wenzake kutoka Zanzibar kuanzisha chama cha CUF. Baadaye akaanzisha chama cha CHAUSTA. Chama cha CHAUSTA sasa kimefutwa katika daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa na Mzee amefariki tukiwa hatujui kama aliwahi kujiunga na chama kingine au aliamua kuishi na kutazama matunda ya Mfumo wa vyama vingi alioanzisha yakiwa yamezungukwa na miba kwa ajili ya kuumaliza.

Leo wakati tunashuhudia juhudi za kurejesha Nchi katika Mfumo wa chama kimoja ni muhimu sana kuwakumbuka kina Mzee Mapalala ambao walipoteza Uhuru wao ili tuwe na Uhuru wa kufanya Siasa. Wakati vyama vinahangaika Leo kuhusu haki ya kukusanyika, kina Mzee Mapalala na wenzake walilipia damu kupata haki hiyo. Kwa hakika sisi tuliohai na tuliobeba wajibu wa kina Mapalala tuna Deni kubwa kwao kwani walichokipigania tunaruhusu kiondoke bila hata kupambana. Utawala wa sasa umeturudisha miaka 30 nyuma katika madai ya haki za msingi.

Mapalala anafariki akiwa hatujampa stahiki zake kama Mwasisi wa mageuzi ya kisiasa nchini. Si yeye tu, tumesahau wengi sana. Kina Mashaka Nindi Chimoto, kina Shaaban Mloo, kina Soud Yusuf Mgeni na wengine wengi ambao wametangulia mbele ya haki. Kuna makosa kadhaa Wazee wetu hawa waliyafanya ikiwemo kuruhusu demokrasia ya kupewa na CCM badala ya demokrasia ya kuchukua. Hata baada ya vyama kuanzishwa bado CCM na dola ilihakikisha inapenyeza propaganda ambazo zilileta mgawanyiko miongoni mwao kama waasisi bila wao kung’amua kuwa wanagawanywa ili CCM ibakie madarakani. Makosa haya bado yanaendelea kufanywa na sisi kizazi kipya cha wanasiasa wa mageuzi.

Nakumbuka mwezi Februari mwaka 2018 nilipokwenda kumwona ndugu Lissu hospitali Ubelgiji, aliniambia maneno muhimu sana na kila wakati nayakumbuka . Aliniambia “ ndugu yangu, tumekulana damu zetu wenyewe kwa wenyewe kwa faida ya watesi wetu. Tusiruhusu hili tena kutokea “. Haya ni maneno ambayo yanapaswa kukaririwa na kila mwana mageuzi wa sasa ili kurekebisha makosa ya kina Mzee Mapalala. Tusiruhusu kamwe propaganda za CCM kutugawa kama zilivyowagawa wao. Nakumbuka mmoja wa wenzake na Mapalala aliandika katika kitabu chake kuwa Mzee James Mapalala aliaminishwa mambo ambayo hayakuwepo na licha ya juhudi za kumfafanulia bado haikuwezekana tena kuwa pamoja na wenzake. Mzee Mapalala mwenyewe katika mahojiano yake na moja ya magazeti hapa nchini anasema kuwa ni kweli waligombanishwa na Dola na alichelewa kung’amua hilo.

Kwenye Nchi zenye ustaarabu James Mapalala angekuwa na nishani maalumu ya utumishi kwa Nchi kwa harakati zake. Lakini kwa kuwa harakati zake zilikuwa za wapinzani watawala wenye mamlaka ya kutoa nishani hawakuona haja kufanya hivyo. Nishani za miaka 50 ya Uhuru hazikupaswa kuisha bila kuwapa watu aina ya James Mapalala, Mabere Marando, Seif Shariff Hamad, Edwin Mtei, Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu, Prince Mahinja Bagenda, Mashaka Nindi Chimoto, Dkt. Ringo Tenga na Vijana wao wa wakati huo James Mbatia, Freeman Mbowe, Ismail Jussa Ladhu, Msafiri Mtemelwa na Antony Kalist Komu na wengine kadhaa ambao sijaweza kuwataja hapa.

Tangulia Mzee James Mapalala, mwasisi wa mageuzi ya kisiasa nchini kwetu. Umetimiza wajibu wako duniani. Hatuna tunachokudai ila wewe unatudai sisi uliotuacha.

Zitto Kabwe
Kiongozi wa ACT Wazalendo
Kibingo, Mamlaka ya Mji Mdogo Mwandiga - Kigoma
24/10/2019
 
Mbia wako hapo ACT ndio alimpora chama mpinzani wa kweli mzee Mapalala!

NHC wamuenzi mteja wao kwa kuiita Mapalala morocco Square!
 
What an epitath!!! ingekuwa bora zaidi kama ungeelezea udhalimu wa Seif dhidi ya Mzee Mapalala ambapo walimpoka CUF na ungeukemea na kuwakemea madhalimu wote bila kujali upo nao au la.
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom