Chadema kimemkaribisha mbunge huyo kujiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa NCCR-Mageuzi. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook alisema: Kafulila akumbuke kwamba hakufukuzwa Chadema ila alijiondoa mwenyewe.
"Milango yetu ipo wazi kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na taratibu za chama chetu,"alisema Zitto. Hata hivyo, Zitto ameeleza kuwa anaamini NCCR Mageuzi watamaliza matatizo yao kwa mujibu wa katiba ya chama chao na Kafulila atazikabili changamoto hizo kama kiongozi kijana wa kisiasa badala ya kukata tamaa.
"Ifahamike wazi kabisa kwamba David ni mtu huru mwenye mawazo yake na maamuzi yake. Kwamba sisi ni marafiki wa karibu na kwamba tunatoka mkoa mmoja,"alisema na kukanusha taarifa zinazomuhusisha yeye na Kafulila kuhusu mgogoro ndani ya NCCR Mageuzi.
"Napenda kuweka wazi kwamba sihusiki kwa namna yeyote ile na migogoro ya chama kile. Ninaomba nisihusishwe na mambo yasiyonihusu. Ni dhahiri kwamba kuvuliwa uanachama kwa David ni jaribio kubwa kwa mfumo wetu wa demokrasia kama ilivyokuwa huko nyuma wakati kina Erasto Tumbo walipovuliwa uanachama wa chama chao cha UDP."
Zitto alisema haina maana kwamba lolote afanyalo ama Kafulila amemtuma yeye au anahusika na kuongeza kwamba, anaheshimu msimamo wake siku zote na huwa yupo upande wa anayeonewa, kudhulumiwa na mnyonge. "Msimamo huu wa msingi usiwape watu nafasi ya kunihusisha na mambo ya chama dhaifu kisicho na dira kama NCCR-Mageuzi,"alisema.
SOURCE: MWANANCHI YA 20-12-2011