UPDATES:
12:30pm
Idadi kubwa ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Polisi wameonekana wakiranda maeneo mengi ya Jiji la Zanzibar tangu alfajiri, ikiwa ni siku ya kupiga kura.
Wakiwa ndani ya magari na wengine kutembea barabarani kwa makundi, wameonekana wamebeba silaha huku wengine wakifunika nyuso zao kwa soksi-uso nyeusi.
Pamoja na kuwepo kwa hali ya utulivu, lakini hali hiyo inaelezwa kuogofya baadhi ya wapigakura, hasa katika majimbo yenye idadi kubwa ya wanachama na mashabiki wa vyama vya upinzani, hasa ACT-Wazalendo.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina amesema kwamba kuwepo askari wa usalama siku ya kupiga kura siyo kosa kwani "wanalinda haki na kuhakikisha kila mtu anakuwa huru kuchagua kiongozi anayemtaka bila kushurutishwa."
Mwandishi wetu ametembea baadhi ya majimbo na kuona wanajeshi na askari wengine wakiwa wamebeba silaha ndani ya maeneo ya kupigia kura. Hatua hii inakatazwa na sheria kwani huenda ikaogofya wapigakura.
Katika Jimbo la Pangawe, Shehia ya Kijitoupele na kituo cha Shule ya Kijitoupele, wanajeshi sita wakiwa na silaha walionekana wakiwa ndani ya eneo la kituo cha kupigia kura. Jimbo hilo lina idadi kubwa ya mashabiki wa chama kikuu cha upinzani, AT-Wazalendo.
Aidha, imeshuhudiwa idadi kubwa ya askari katika Jimbo la Welezo, wakiranda kutoka kituo kimoja cha kupigia kura hadi kingine wakiwa na magari ya deraya, magari yenye maji ya kuwasha na magari mengine.
Katika majimbo ya Raha Leo, Mwanakwerekwe, Bububu na Chambani, hali ilikuwa tofauti, idadi ndogo ya askari walishuhudiwa wakizunguka vituo vya kupigia kura, wakiwa na virungu na wengi wa askari hao wakiwa wanawake.
Hadi mchana wa leo, hali ya usalama imekuwa shwari na hakuna taarifa za vurugu wala rabsha katika maeneo ya vituo vya kupigia kura au barabarani katika maeneo mengi ya Unguja.
UPDATE 2: