Je, jamii ambayo inajikuta inatengwa, inanyanyaswa na kuonewa na jamii kubwa je inayo haki ya kutafuta ulinzi wake yenyewe na uhai wake? Je ina haki ya kutafuta mahali ambapo inaweza kuwa salama kwani ni mahali pake? Kwa mfano Albania na Macedonia, au tuangalie suala la Kosovo. Tena mfano mzuri ni Kosovo je wananchi wa Kosovo walikuwa na haki ya kutafuta mahali pao na kujitambua kama ni kwao na hata kujitangazia uhuru kwa sababu Serbia ilikuwa inawanyanyasa?
Biafra ilikuwa inahusiano gani na sehemu nyingine za Nigeria na ni kitu gani kilisababisha kina Ojukwu kutaka kujitenga na Nigeria?
Ukiondoa Tanzania nchi nyingine zilizoitambua Biafra ni pamoja na Gabon, Ivory Coast, Haiti, na Zambia. Je hizi nchi ziliitambua Biafra kwa sababu gani?
Tunaambiwa na historia kuwa mwaka 1966 Septemba WaIgbo 30,000 waliuawa huko Kaskazini mwa Nigeria na kusababisha mauaji ya malipizi vile vile sehemu nyingine za Nigeria. Matukio hayo yakaanza kusababisha wananchi wenye asili ya Biafra kuanza kurudi kwa wingi kwenye eneo lao la asili.
Hadi hivi tunavyozungumza bado ipo movement ya wananchi wa Biafra kuwa na nchi yao na kama Sudan Kusini watajitenga na Sudan kama inavyotarajiwa itawapa moyo wananchi wa Biafra kujitenga hata kwa kupiga kura ya maoni. Litakapoundwaa taifa la Biafra siku moja ndipo kwa mara nyingine tutaona kuwa Nyerere alikuwa mbele sana ya historia. Kila watu wana haki ya kuwa mahali pao ambapo watakuwa salama. Hii ni haki ya Wapalestina kama ilivyo kwa Waisraeli. Hata katika Tanzania yetu hii kama kuna kundi au kabila moja litaonekana kuonewa, kunyanyaswa na kutengwa na serikali kabila hilo litakuwa na haki ya kuishi kutaka kuwa salama katika eneo lao.
Na wakati mwingine nina hofu naweza kuhisi ni kabila gani linaonekana kuonewa na kuanza kutengwa na kulaumiwa kwa kila baya.