Mchango Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) 18 April 2012 (Hii ilichangia Rais kuwawajibisha mawaziri)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, lakini vilevile niwasihi Wabunge wenzangu tusilalamike, jukumu letu sisi ni kuisimamia Serikali. Pale ambapo tunaona Serikali haitekelezi kile ambacho tunaagiza, tuna jukumu la kutoa azimio na kufanya chochote ambacho tunataka kufanya kama Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wetu wa kulalamika, utaratibu wetu wa kunung'unika ndiyo unawajaza viburi Mawaziri waliokuwepo hapo mbele. Ndiyo maana Tanzania yetu imefika sasa kwamba mtu akiwa Mbunge, akichaguliwa kuwa Waziri anachowaza yeye ni kwenda kupiga deal. Baadhi ya Mawaziri wako hivyo, tumeona, tumemsikiliza Mheshimiwa Kangi Lugola, nimemsikiliza kwa makini nilikuwa ofisini, anazungumza kwa namna gani Mawaziri badala ya kwenda kutekeleza wajibu ambao Rais amewaamini, kumsaidia kuongoza hii nchi wanafanya mambo ndivyo sivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Wabunge wanalalamika, mimi hiki ni kipindi cha pili, Mheshimiwa Kafulila kasema kweli ukisoma Hansard mambo ambayo yanalalamikiwa leo ndiyo mambo ambayo tuliyajadili Bunge lililopita, Mawaziri wamejisahau.
Kuna baadhi wanafanya kazi, lakini kuna wengi wanadhani kwa kupewa Wizara, kupewa shangingi, kwa kupewa nafasi ya kusaini mikataba ni sehemu ya kupata pesa na majuzi nilisikitishwa sana kwa kuona kwa kiasi gani Mawaziri wetu hawako serious. Lilipoulizwa swali kuhusiana na mashamba kule Kapunga Mbarali, aliuliza Mbunge hapa kwamba jamani maeneo ya wananchi yamemwagiwa sumu
na mwekezaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri wa Kilimo
anasimama hapo anatoa majibu kama vile hilo suala lilikuwa halijawahi kumfikia, kama vile hilo suala lilikuwa halijawahi kujadiliwa kwenye Vikao vya Bunge, kama hivyo hilo suala halijawahi kutolewa maazimio kufuatia taarifa ya Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma mwaka 2009 kuhusiana na suala la Kapunga.
Maeneo ya wananchi, eneo la wanakijiji linalokaribia hekta 1800 limechukuliwa na mwekezaji kwa kushirikiana na watu wa Serikali ambao siyo waaminifu kinyume na utaratibu. Kamati yetu ikasema kupitia Mwenyekiti wetu, alikuwa Zitto, Serikali ikaji-commit lakini utashangaa miaka miwili na nusu au mitatu baadaye Waziri amesahau, hajui kinachoendelea, anatoa
ahadi mpya, ndiyo Mawaziri wetu, nchi itakwenda?
Haiwezi kwenda! Kwa hiyo, mimi nawaomba Wabunge wenzangu ifike kipindi hawa watu kwa sababu wanalipwa, mara Waziri akienda Jimboni kuna mambomambo huko, wanalipwa ili wafaye kazi za wananchi. Kama hawafanyi kazi za wananchi, tuna uwezo wa kuwazuia katika mazingira mbalimbali, mamlaka hayo tunayo. Tuache
kulalamika, tukilalamika, wananchi waliotuchagua watatushangaa! Watashangaa kwamba Wabunge tumewapeleka wakaisimamie Serikali lakini wao wanageuka walalamikaji, wananchi wafanye nini? Tutekeleze wajibu! Naomba katika hili masuala ya itikadi tuweke pembeni, tunapojadili masuala ya msingi tuache kuangalia u-CCM, u- CUF, u-CHADEMA na u-TLP. Tukiamua kumwadhibu Waziri, tunamwadhibu kwani ni jukumu letu kufanya hivyo. Kwa hiyo, mimi naomba tuache kulalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, Kamati ya Mashirika ya Umma imezungumzia masuala ya viwanda nadhani pia kwa sababu ya muda hawakuweza kupata nafasi ya kuzungumzia kwa kina taarifa ya ufuatiliaji wa mashamba na viwanda hasahasa mashamba kwa sababu viwanda wamei- capture vizuri sana shughuli ambayo imefanywa na CHC. Tumekuwa tukizungumza kwamba watu wezi, mafisadi na kadhalika lakini kuna taarifa huku zinatisha. Zinatisha kwa nini?
Kuna huyu mtu anaitwa Chavda sijui amekufa au yuko hai? Watu wa aina ya akina Chavda kama kweli wapo hai wanatakiwa wakamatwe kama wezi wengine.
Wakamatwe na wanyongwe, kwa nini tunasema hivi? Taarifa hapa inamwonyesha Bwana Chavda katika mashamba makubwa matatu tofauti yenye ukubwa wa kati ya hekta 5000-6000, mashamba matatu tofauti kwa ajili ya dili zilezile ambazo Mawaziri tuliowapa ridhaa kipindi kile wakamuuzia eneo hilo kwa bei chee! Alichokifanya Bwana Chavda, akaenda kuchukua mkopo kwa mashamba yote matatu, baada ya kuchukua mkopo kwa dhamana ya shamba, mali ya Watanzania ambao wengi hawana ardhi akachikichia, shamba akalitelekeza, eti Serikali inasema inaangalia itamlipaje fidia mtu mwingine aliyeuziwa na Benki ya CRDB ambapo waliuza shamba lile kwa sababu lilitumika kama security ili eti atafutwe mwekezaji mwingine, lugha nyepesi kwa masuala mazito!
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoka Arumeru, ardhi Tanzania itatumwagisha damu baadaye, kila unapokwenda ni mgogoro wa ardhi. Akija mgeni, Waswahili tuna msemo usemao 'mgeni njoo mwenyeji apone'. Tanzania akija mgeni kwenye suala la ardhi, msemo unakuwa 'mgeni njoo mwenyeji asulubike'. Leo Mtanzania wa kawaida ni vigumu kupata hekari moja ya ardhi, wanaishia kuwa wavamizi, lakini kuna wajanja wachache, wenye fedha, wanaojua kula na viongozi Serikalini, wanapewa maeneo chee, hawayaendelezi na Serikali ina-incur gharama mara mbili, hatuoni haya?
Waheshimiwa Wabunge, mimi naomba, hawa watu sisi ni vijana, watoto na wajukuu zetu sisi tutawaachia nini? Hawa watu wazima wanatuangusha, inawezekana wanaona future yao miaka 10 mbele wameshakatika, sisi tuna miaka 30 au 40 mbele mnataka mtuachie nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa dhati, Bunge tuna meno, haiwezekani mashamba 14 makubwa yenye ukubwa kati ya hekta 4000-5000 watu wamechukua, wameyatelekeza halafu Serikali haichukui hatua, inabembelezana nao, kama ninyi siyo wadau, kwa nini hamchui hatua? Kwa hiyo, naomba sheria ichukue mkondo wake, tunavyohukumu mafisadi wengine na hawa ni mafisadi vilevile kama wanashindwa
kusimamia mali za Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la TBS, ninasikitika majibu ya Mawaziri na ni kwa mtindo huohuo wa masuala ya ardhi. Hapa kuna report ya CAG, anasema makampuni yamepewa kinyume na utaratibu, makampuni hayana vifaa, makampuni hayalipi tozo kwa TBS lakini bado wanarudiwa kupewa mikataba, eti Waziri anasimama hapa anatoa majibu mepesi, Waziri anasimama hapa anaongea lugha nyepesi, wataalamu wanashauri hii kampuni haifai kupewa kazi hii kwani haina uwezo, lakini wanalindwa. Kwa hiyo, mimi naomba Wabunge tusimame, tumechoka kulalama, msilalame kwani wananchi watawarushia mawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.