Tarehe 8 February 2011 Mh. Mdee aliuliza swali Namba 8 kikao cha 2
Jimbo la Kawe ni miongoni mwa Majimbo yanayokabiliwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa maji:-
(a) Je, Serikali ina mipango gani ya muda mrefu na ya muda mfupi na wa kati ya kutatua tatizo hilo sugu?
(b) Kama mipango husika ipo, utekelezaji wake utaanza na kukamilika lini?
Mh. Eng. Gerson Hosea Malangalila Lwenge, Naibu Waziri wa Maji alijibu:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kumaliza tatizo la ukosefu wa maji katika Jimbo la Kawe, Serikali imeandaa mipango ya muda mfupi, wakati na muda mrefu. Mpango wa muda mfupi unahusu kuimarisha mfumo wa usambazaji, kupunguza uvujaji wa maji pamoja na kufunga dira kwa wateja wote wanaopata maji ili maji yanayozalishwa yawafikie watu wengi zaidi.
Kazi hii inaendelea, lengo ni kupunguza kiwango cha maji yanayopotea kutoka asilimia 50 ya sasa hadi asilimia 35. Pia Serikali kupitia DAWASA imepanga kutekeleza mradi huu kujenga mtandao wa majisafi wenye urefu wa kilomita 300 na kuunganisha wateja katika maeneo ya Tegeta, Ununio, Mbweni, Bahari Beach, Mivumoni, Boko, Bunju na Mpiji. Kazi hii itatekelezwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP).
Kazi ya usanifu na kuandaa vitabu vya zabuni imekamilika. Ujenzi wa mradi utaanza Julai, 2011 na kukamilika Julai, 2012. Serikali inatekeleza upanuzi wa mitambo ya Ruvu Chini kwa lengo la kuongeza uzalishaji maji kutoka lita milioni 180 hadi lita milioni 270 kwa siku. Kazi hii inagharimiwa na Shirika la Millennium Challenge Corporation ya Marekani kwa kiasi cha shilingi bilioni 31.5. Kazi inaanza mwezi Februari, 2011 na itakamilika mwezi Machi, 2013.
Mheshimiwa Spika, mpango wa muda wa kati unahusisha pia ujenzi wa bwawa la Kidunda ili kuongeza uhakika na uendelevu wa upatikanaji maji katika vituo vya Ruvu Chini na Ruvu Juu. Kazi ya usanifu inandelea na itakamilika mwezi Juni, 2011. Mpango huo pia unahusisha upanuzi wa kituo cha Ruvu Juu. Ujenzi utaanza baada ya kukamalika kazi ya usanifu wa miradi yote miwili.
Serikali kupitia DAWASA inatekeleza mradi wa maji ya visima katika eneo la Kimbiji na Mpera, katika Wilaya ya Temeke. Uchimbaji wa visima unatarajiwa kuanza mwezi Agosti, 2011. Utakapokamilika mradi huu utaongeza upatikanaji wa maji Jijini Dar es Salaam kwa lita milioni 260 kwa siku. Kwa kuwa maeneo ya kusini mwa Dar es Salaam yatapata maji kutoka Mpera na Kimbiji, hali hiyo itaboresha upatikanaji wa maji Kaskazini mwa Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na Jimbo la Kawe maeneo ambayo yatahudumiwa na mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu.
Tarehe 20 July 2011 Mh. Mdee aliuliza swali Wizara ya Tamisemi
(a) Je, Serikali hutenga wastani wa shilingi ngapi kwa ajili ya ukarabati ndani ya Manispaa ya Kinondoni, na ni utaratibu gani unatumika kufuatilia toka kwa Wahandisi wa Manispaa kuhakikisha kwamba barabara zote za Manispaa zinapatikana nyaraka zote?
(b) Je, kuna utaratibu gani wowote wa kuthaminisha gharama zilizotumika na uhalisi wa kila kilichotengewa?
NAIBU WAZIRI Mh. Aggrey Mwanri, alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee Mbunge wa Kawe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni hupata fedha kwa ajili ya miradi ya barabara, Madaraja na Makalvati kutoka katika Mfuko wa Barabara, ruzuku za fedha za maendeleo ya Serikali za mitaa na vyanzo vya mapato ndani ya Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2009/2010 Manispaa kupitia vyanzo hivyo ilipata jumla ya shilingi bilioni 4.3. Fedha hizi zilitumika kufanya matengenezo ya barabara za lami kilomita 1.65, kufanya matengenezo ya changarawe kilomita 48, kuziba viraka katika barabara za udongo kilomita 23.5 matengenezo ya madaraja ya madaraja 11, kujenga kalvati 1 na ununuzi wa Motor Grader 1.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mfuko wa Barabara (Road Fund) hutuma utaratiu wa kutumia Wahandisi na Wataalam wengine kutoka ofisi zao kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji au kuhakiki kazi hizo (Physical and Financial Audit).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imepanga kutumia shilingi bilioni 3.2 kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Manispaa shilingi milioni 350 kama Ruzuku ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa (LGCDG) kwa ajili ya kujenga daraja la Makongo maeneo ya Goba na shilingi bilioni 5.6 kutoka vyanzo vya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya kujenga barabara kiwango cha lami, changarawe na madaraja.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Makaguzi wa ndani, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kamati ya Kudumu ya Bunge Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na kitengo cha ufuatiliaji na tathimini (M&E) katika Halmashauri, Mkoa na OWM-TAMISEMI hufanya ukaguzi wa Miradi inayotekelezwa ili kuona kama fedha hizo zimetumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kupata thamani ya fedha katika miradi hiyo (Value for Money).
Tarehe 6 April 2011 Mh. Mdee aliuliza swali la nyongeza namba 22 kikao cha 3Mheshimiwa Spika, kwa kuwa matatizo ya karagwe yanafanana kwa kiasi kikubwa sana na matatizo ya Jimbo la Kawe hasa katika Vijiji vya Mabopambe, Mbopo na baadhi ya maeneo ya Kata ya Bunju ambayo yako katika Jimbo la Kawe, katika Jiji la Dar es Salaam lakini hayana umeme.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akaliambia Bunge hili Tukufu kwamba kuna mikakati yoyote ya kutatua matatizo ya umeme katika maeneo hayo kwenye Jimbo la Kawe?
Waziri wa Nishati na Madini Mh. William Ngeleja alijibu:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Serikali ina mikakati ya kupanua huduma mbalimbali na hasa usafirishaji na usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Kwa Dar es Salaam tuna mradi maalum ambao tunafadhaliwa na wafadhili mbalimbali ambao pamoja na kupanua miundombinu ya kusafirisha lakini pia tunaongeza usambazaji kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuzidi kuwasiliana kwa sababu pia amekuwa akifuatilia ofisini kwetu kujua majaliwa ya wananchi wa maeneo mengine ambayo ameyaombea.
Tarehe 20 July 2011 Mh. Mdee aliuliza swali la nyongezaMheshimiwa Spika, nashukuru, nina swali moja tu la nyongeza. Kufuatia mvua kubwa sana zilizonyesha Mkoa wa Dar es Salaam, karibu asilimia 80 za Barabara za Manispaa ya Kinondoni ni mbovu sana; na kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam na husasan Manispaa ya Kinondoni ndiyo inatoa mchango mkubwa sana katika Road Toll, karibia asilimia 80.
Je, Serikali haioni sasa Dar es Salaam inatakiwa iangaliwe kwa jicho la pekee linapokuja suala la mgao wa fedha za barabara?
Mh. Aggrey Mwanri NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA LA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu
Mheshimiwa Spika, kitu ambacho Mheshimiwa Halima Mdee anakisema hapa ni valued. Politics na economics za nchi hii zinakuwa determined na Dar es Salaam kwa sababu ya mambo ambayo yanafanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Tukisema tunakuja hapa kuzungumza habari za barabara kutengeneza Mji wa Dar es Salaam kupitia Bajeti tunayozungumza hapa tunaota ndoto na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja hapa akasema tutahitaji kuwa na utaratibu maalum. Kwa hiyo halima anachosema pale wala siwezi kumpinga. Ukichukua Bajeti yetu na mapato yanayotoka Dar es Salaam, bandari, viwanda vikubwa viko Dar es Salaam kwa hiyo mapato yanayotoka pale ni makubwa.
Lakini nchi yetu kwa sababu inajali watu inatenga hela kufuatana na mahitaji katika nchi nzima bila kujali fedha imetoka, Kilimanjaro wanazalisha kahawa, Mtwara wanazalisha, Mwanza wanazalisha, ukisema unaangalia pale itakuwa ni matatizo. Lakini nikiri mbele yako kwamba iko haja kuliangalia suala hili na tulishasema kwamba kuna haja ya kuliangalia jambo hilo kwa sura hiyo anayozungumza pale.
Tarehe 26 July 2011 Mheshimiwa Mdee aliuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Sheria na katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru. Kwa kuwa tatizo la Mchinga linafanana kabisa na tatizo la Jimbo la Kawe na katika Bunge lililopita aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria aliahidi kuifanyia ukarabati Mahakama ya Kawe suala ambalo halijafanyika kabisa.
Je, Mheshimiwa Waziri anaahidi kama alivyosema hapa kwenye Bajeti yake kwamba moja kati ya Mahakama ambazo zitapewa kipaumbele ni Mahakama ya Kawe?
Mh. Selina Kombani Waziri wa Sheria na katiba alimjibu:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika Bajeti ya mwaka 2010/2011 Mahakama ya Kawe ilikuwa ni mojawapo ambayo ilikuwa kwenye orodha ya Mahakama zitakazokarabatiwa. Tayari mchakato umefanyika na fedha zipo Mahakama hiyo itajengwa katika mwaka huu kwa sababu fedha zimepatikana mwishoni mwa mwaka.
Tarehe 15 November 2011 Mh. Mdee aliuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Nchi OMR/ Mazingira
Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa mazingira katika Jimbo la Kawe na hususan maeneo ya Kawe Beach ambapo pamoja na mambo mengine, wenye fedha wanajenga baharini kinyume na sheria lakini vilevile wanajenga kuzuwia kingo za mto.
Taarifa ambayo Wizara yako inayo na Mheshimiwa Waziri wa Mazingira alitembelea pale na maagizo yameshatolewa kutoka kwenye Wizara tatu, Wizara yako, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ardhi kwamba, watu waliojenga pale wanatakiwa wavunjiwe. Lakini utekelezaji umekuwa duni na kuna tuhuma kwamba, Halmshauri ya Manispaa ya Kinondoni imehongwa na vilevile Jeshi la Polisi limehongwa kwa sababu, hawataki kutoa ushirikiano kwa NEMC.
Mh. Dr. Terezia Huvisa, Waziri wa Nchi OMR/ Mazingira alijibu:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema mwenyewe kwamba, Wizara yangu iliwajibika kikamilifu baada ya kipindi cha Bajeti na tulishirikiana na yeye katika kutembelea eneo hilo na yote aliyoyasema tuliyaona kwa pamoja. Kama alivyosema kwamba, majukumu haya yako katika Wizara tatu. Wizara yangu kama kiungo, itaitisha mkutano tena na Wizara zote tatu na tuweze ku-review hatua zilizofikiwa.
Mheshimiwa Spika, lakini jingine kubwa ni kwamba, Mheshimiwa Halima kama Mbunge wa eneo, tunategemea kupata taarifa nyingi kutoka kwake na ushirikiano mkubwa kutoka kwake. Suala la kuhongwa au kutokuhongwa kwa Halmashauri, sio rahisi Wizara kulijua hilo lakini tutamtegemea yeye kutupa taarifa ili tuweze kuzifanyia kazi Wizara zote tatu.
Tarehe 29 June 2011 Mheshimiwa aliuliza Swali na. 143 SESSION # 4Mapema mwaka juzi Serikali ilizikamata fedha za wananchi zilizotokana na mchezo wa upatu maarufu kama DECI, lakini ukimya mkubwa umekuwepo baada ya fedha husika kuchukuliwa na Serikali:-
Je, ni nini hatima ya fedha hizo za wananchi?
Naibu Waziri wa Fedha Mh. Teu, Gregory George alijibu:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali haijachukua fedha za DECI bali fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 14.81 zimezuiliwa katika akaunti zinazomilikiwa na Wakurugenzi wa DECI katika Mabenki mbalimbali nchini. Fedha hizo ni asilimia 37.77 ya fedha ambazo zinazodaiwa na wanachama wa DECI ambazo ni takriban shilingi bilioni 39.27.
Mheshimiwa Spika, uamuzi wa kuzizuia fedha hizo uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni hatua mojawapo ya uchunguzi dhidi ya DECI ambayo ilikuwa inaendesha mchezo wa upatu (Pyramid Scheme).
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu na kulikumbusha Bunge lako Tukufu kuwa, kesi ya DECI Nambari 109/2009 iliyofunguliwa tarehe 12 Juni, 2009 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado inaendelea kusikilizwa. Hivyo basi, hatima ya fedha hizo za wananchi itategemea hatma ya kesi hiyo kwani DECI ilikuwa na matawi 40 katika mikoa 18 ya Tanzania Bara. Usikilizwaji wa mashahidi wa Dar es Salaam umekwishakamilika na hatua za kuwapata mashahidi kutoka mikoa mingine zimekwishaanza. DECI ilikuwa na jumla ya wanachama wapatao 649,859 na sehemu ya wanachama hawa watahitajika kuja kutoa ushahidi Mahakamani.
Tarehe 29 June 2012 Mheshimiwa Mdee aliuliza swali namba 107 kikao cha 8Mheshimiwa Spika, Serikali iliifungia Kampuni ya DECI ikiwa ni pamoja na kukamata mali, fedha na kuwafungulia mashataka Wakurugenzi Wakuu waKampuni hiyo:-
(a) Je, Serikali ilifanikiwa kuokoa kiasi gani cha fedha na fedha hizo ziko wapi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani na fedha hizo?
(c) Je, nini mustakabali wa fedha zilizowekezwa na Watanzania waliopanda mbegu zao wakitarajia kupata zaidi?
NAIBU WAZIRI wa Fedha Mh. Janet Zebedayo Mbene, alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha naomba nijibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali iliweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 14.81 kati ya shilingi bilioni 39.27 zilizokuwa zinadaiwa na washiriki wa DECI. Fedha hizi zimezuiliwa katika akaunti zinazomilikiwa na Wakurugenzi wa DECI katika mabenki mbalimbali hapa nchi.
Mheshimiwa Spika, hatma ya fedha hizi itategemea hukumu ya kesi 109/2009 iliyofunguliwa tarehe 12 Juni 2009 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Aidha, mnamo Julai 17 mwaka 2012 Mahakama itatoa uamuzi kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.
Tarehe 9 November 2011 Mheshimiwa Mdee aliuliza swali Namba 22 kikao cha 5
Ingawa wananchi wamekuwa wakijigharamia wenyewe kuvuta umeme majumbani mwao, lakini kupata umeme huo imekuwa ni kero na ghiliba kubwa:- Je, ni nini hasa kikwazo cha kupatiwa huduma hii ya msingi?:-
Mheshimiwa Adam Malima Naibu Waziri wa Nishati na Madini alijibu
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida, wateja waliopo umbali usiozidi mita 30 kutoka kwenye nguzo hupatiwa umeme ndani ya siku 30 kuanzia siku wanapolipia huduma hiyo. Wakati mwingine muda huu huzidi kutokana na ucheleweshaji katika kupatikana kwa vifaa vya huduma ya umeme kwa mteja kwa kuwa vifaa vingi huagizwa nje ya nchi na kutokana na taratibu ndefu za manunuzi na za kutoa mizigo bandarini, mara nyingi vifaa hivi huchelewa kufika na hivyo kusababisha baadhi ya wateja ambao wamelipia na kukamilisha taratibu zote kuchelewa kupata umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa wateja waliopo umbali unaozidi mita 30 nguzo hutakiwa kusimikwa na gharama za nguzo ni za mteja.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kama tulivyoeleza hapa Bungeni wakati wa kujibu swali la Mheshimiwa James Daudi Lembeli, Mbunge wa Kahama tarehe 9 Agosti, 2011, tangu wakati huo hadi sasa kuna hali ya kuridhisha ya upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya kuwaunganishia wateja umeme kwa muombaji wa umeme aliyelipia hupata huduma hiyo ndani ya muda unaostahili.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kawe ambao wamekwishaomba na kulipia kuunganishiwa huduma ya umeme, wawasiliane na Ofisi za TANESCO Mikocheni kwa ajili ya taratibu za kupata huduma hiyo na kama matatizo haya yakiendelea nipatiwe taarifa kupitia kwa Mheshimiwa Mbunge kwa hatua zaidi.
Mheshimiwa Spika, TANESCO hivi sasa imeweka utaratibu wa kuweka matangazo na kuwasiliana na wateja moja kwa moja, pale inapotokea kuwepo ucheleweshwaji wa kuwasili kwa vifaa vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi, kwa wateja ambao walishalipia huduma ya kuwekewa umeme na kwa wale ambao hawajalipia huombwa wasilipie hadi pale ambapo pana uhakika wa kupatikana vifaa hivyo.
Swali la nyongeza kwa swali lake la msingi
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2011 wakati Rais alipotembelea Wizara ya Nishati na Madini kwa malengo ya kuzungumza na wafanyakazi pamoja na mambo mengine alielekeza Wizara kuhakikisha kwamba gharama za kuunganishwa kwa umeme zinapungua. Sasa nilitaka Mheshimiwa Naibu Waziri anieleze ni kwa kiasi gani ahadi hii ya Rais imetekelezwa ama imeanza kutekelezwa au ilikuwa ni yale matamko ya kisiasa ambayo hayana utekelezaji?
Swali langu la pili, kwa kuwa TANESCO imeonyesha kuzidiwa na nguvu katika kutoa huduma hii nyeti na kwa kuwa malengo ya Serikali ni kwamba itakapofika mwaka 2015 kuwe na nyongeza ya asilimia 30 ya Watanzania ambao wanapata huduma hii. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuruhusu makampuni binafsi kuweza kuwekeza katika umeme kufanya shughuli ya kusambaza umeme ili kuleta ushindani lakini vilevile kupunguza gharama kwa Watanzania?
Jibu la swali la nyongeza:
Mheshimiwa Spika, inawezekana Mheshimiwa Halima Mdee hakuelewa yale maagizo ya Rais. Maagizo ya Rais yalikuwa kuielekeza TANESCO itafute mbinu na ifanye tathmini ya namna ya kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa mteja. Sisi Wizara ni wasimamizi wa zoezi lile. Sio kama sisi Wizara yenyewe ndio tutapunguza gharama ile na haikuwa matamko ya kisiasa.
Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kwamba kwa hivi sasa gharama ya kuunganisha umeme inakwenda kwenye shilingi 480,000/= ukiweka na VAT. Kwa maana ukiondoa ile asilimia 20 inakuwa kama shilingi 400,000/= kwa maana ya gharama zenyewe halisia. Lakini kwa miaka hii miwili, mitatu ambayo gharama imebaki hivyo, gharama zile za vifaa vyenyewe zimefika hadi shilingi 600,000/=. Kwa hiyo, hadi hapo tunapokwenda kwenye shilingi 480,000/= bado pana gharama ambayo imeongezeka ambayo bado inafidiwa na Serikali yenyewe ili wananchi waweze kuunganisha umeme kwa bei hiyo ambayo tunaunganisha sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kusema kweli ni kwamba gharama hizo kwa sasa hivi bado TANESCO wenyewe wanalalamika kwamba hazi-reflect cost ile au gharama halisi ya wao kununua vifaa. Kwa hiyo, hili ni jambo kusema kweli ambalo lazima tulifanyie kazi na katika moja ya maeneo ambayo tumesema tuyafanyie kazi ni kwa mfano pale ambapo nguzo zinazotoka hapa hapa Tanzania ambazo gharama yake kwa mfano labda ni shilingi 300,000/= kwa wastani, ziangalie namna ya kupunguza bei, lakini pia kuongeza ubora ili vilingane na nguzo ambazo zinazotoka Afrika ya Kusini ambazo kwa sasa ni bei nafuu zaidi. Kusema kweli ni kwamba zoezi hilo linaendelea na halikuwa ni zoezi linalotokana na matamishi ya kisiasa, lakini lililenga kupunguza gharama, kwenye nguzo lakini pia kwenye mambo mengine.
Mheshimiwa Spika, suala la pili, labda niseme kwamba sheria tayari inaruhusu makampuni binafsi kuingia kwenye zoezi hili, tatizo linakujaje, kwamba makampuni binafsi yakiingia yatataka kufanya kazi hii kwa biashara. Ikiwa ni kampuni labda kama ya Mzee Cheyo au ya Bwana Malima atataka gharama hizo ziwe kwa shilingi 600,000/= ile aliyogharamia. Kwa hiyo, labda tuingie kwenye makubaliano ya kumpa ruzuku ili aweze kufikisha gharama hiyo kwa shilingi 400,000/=.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo labda niseme tu hapa sasa hivi pia tuna changamoto hii ya kwamba mazingira ambayo yapo ya kufikisha gharama ile kwa wananchi wanayakwaza makampuni binafsi kuingia kwa sababu itabidi watoe huduma hiyo kwa gharama kidogo ya juu ambayo wananchi watashindwa kuifikia.