Katika moja ya familia za ukoo wetu alitokea kaka mmoja mpambanaji sana. Hakuwa amesoma, ila alipambana anavyojua yeye katika kazi, biashara nk na muda si mrefu mafanikio yakaanza kuonekana. Pale kijijini akawa yeye ni kati ya watu wenye uwezo, nyumba nzuri, magari, biashara nk.
Baada ya yule kaka kuanza kuwa tajiri, yakaanza maneno hasa baada ya mtoto wake wa kwanza wa kiume kufariki kwa ajali. Watu wakaanza kusema huyu kaka ndio kamtoa mwanae kafara ili awe tajiri. Muda si mrefu ikawa sasa kila mtu anaepata tatizo katika ukoo iwe ni kufilisika, kuugua, kufukuzwa kazi nk shutuma zikawa ni kwa yule jamaa kwamba yeye ndio ameshika nyota za wanafamilia wote na ndio anasababisha wasiendelee..!
Miaka kadhaa mbele, yule kaka tajiri akauawa na watu wasiojulikana. Watu waliomuua hawakuwahi kupatikana, wala hakukua na kesi. Akaacha familia ya mke na watoto wadogo wengine wakiwa shule na wengine hawajaanza shule bado.
Leo hii tunapoongea ni zaidi ya miaka 10 imepita tangu yule kaka auawe. Wale ndugu waliokua na shida, bado wana shida tena sasa zimezidi maana angalau yule jamaa alikua anawasaidia saidia. Waliokua wamefukuzwa kazi, sasa ndio wanakunywa mataputapu kule kijijini, hali zao ni mbayaa na wengine tumeshawazika. Katika kundi la watu masikini pale kijijini, hakuna mwenye ahueni mpaka sasa, na mbaya zaidi familia ya yule kaka nayo imeingia kwenye kundi la masikini wa pale kijijini baada ya mali kumalizika.
Ninachotaka kusema ni hiki: Unaweza kuua watu wote unaodhani kwamba ndio chanzo cha matatizo yako, na baada ya hapo ukajikuta kwamba hali yako inakua ngumu maradufu ya ilivyokua hapo kabla!
Ushauri wangu: Acha kutafuta mchawi wa maisha yako, mara kuna watu wanataka kukuua, mara sijui kuna laana za mababu, hivyo ni visingizio tu ambavyo havina msingi. Pengine mchawi ni wewe mwenyewe na familia yako!!! Mafanikio hua yana misingi ya kuzingatia, na kama hamuizingatii mtalaumu kila mtu. Je, mnazingatia masomo? Je, mnazingatia biashara? Je, mnaendekeza Ulevi? Anasa? Ushirikina? Udini? Ugomvi? Jichunguze mkuu, then chukua hatua stahiki acha mawazo ya kuua watu bila sababu za msingi.