Tangu chaguzi za marudio kata 29 mwaka jana, mwezi Oktoba, CCM wamekuwa wakishangaza jambo moja muhimu sana katika mahesabu ya kiuchaguzi! Wamekuwa sawa na bwana mkubwa mjinga nitakayemwelezea hapa chini;
Hivi bwana mkubwa mwenye watumwa 40 mfano anakwenda vitani na mtu mmoja anayedhaniwa kuwa dhaifu, asiye na kitu ambaye anajitutumua na anafanikiwa kupambana na jeshi la bwana mkubwa na kuteka watumwa wanne kati ya wals 40, vita hiyo fupi inakwisha, bwana mkubwa anaanza kujisifu kwa kushinda vita na kubakia na watumwa 32, hakumbuki kuwa mtu yule ambaye hakuwa na chochote ameweza kupambana na 'kumshinda' kwa kuweza kuwachukua na kuwaweka huru waliokuwa watumwa wake.
Maeneo hayo ambayo wameweza kupata viongozi na wajumbe wa CHADEMA, kuanzia juzi ni maeneo huru, yamekombolewa kutoka utumwani mwa mikono ya serikali dhalimu ya CCM inayohangaika kujiokoa katika anguko kubwa. Wamekuwa watu huru. Wamepata utumishi. Watatumikiwa hawatatawaliwa.
Wananchi hao ni sawa na mkulima aliyeamua kufuga paka wachache tu kuwaweka ndani ya ghala kubwa la chakula lililokuwa limejaa mapanya wengi. Ulaji (kuminya haki za wananchi, kuwadhulumu, kuwanyanyasa n.k) katika maeneo hayo sasa, hautakuwa kama ilivyokuwa.
Kama CCM imefikishwa mahali ambapo inaweza kujivunia kushinda vijiji na vitingoji, maana yake ni kwamba kuna mshindani huko na mshindani huyo ukimshinda inabidi utambe mji mzima. Haikuwahi kutokea katika historia ya upinzani nchini. Dalili za CCM kufa, wanazionesha kwa maneno na vitendo vyao wenyewe.
Wameshakabwa hadi kwenye vitongoji. CHADEMA sasa imefika na imesimikwa kila mahali nchi nzima. Hili ndilo lilikuwa la muhimu na hatua kubwa sana katika safari hii iliyoanza miaka mingi iliyopita.