Waziri wa Uchukuzi, Prof. Mbarawa azindua Bodi Mpya ya Wakurugenzi TRC

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
large-1694501703-Uzinduzi wa Bodi 1_050046~3.jpg

Shirika la Reli Tanzania - TRC imefanya hafla fupi ya uzinduzi wa Bodi mpya ya wakurugenzi iliyoongozwa na mgeni rasmi Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa iliyofanyika katika jengo la stesheni ya SGR lililopo jijini Dar es Salam Septemba 11, 2023.

Bodi mpya iliyozinduliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi Bw. Ally Karavina akiwa na wajumbe wa Bodi ambao ni Dtk. Shaaban Ramadhani Mwijaka, Bw. Narcis Aloyce Lumumba, Bw. Masanja Kungu Kadogosa, Bw. Shaaban Ahmed Kabunga, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa na Bw. Redemtus Peter Bugomola.

Prof. Mbarawa ameipongeza Bodi mpya ya wakurugenzi ya TRC kwa kuaminiwa na Serikali na kuteuliwa kusimamia Shirika la Reli Tanzania ambalo linatoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya reli.

“Niipongeze pia Bodi iliyomaliza muda wake kwa kazi nzuri waliyoifanya ya usimamizi wa huduma za Shirika pamoja na miradi ya kimkakati ukiwemo wa SGR na mradi wa kukarabati reli ya kati kipande cha Dar es Salaam - Isaka” alisema Mhe. Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa alieleza kuwa Serikali inaendelea kuweka fedha katika mradi wa ujenzi wa SGR ambao unaendelea vyema katika vipande vitano vya awamu ya kwanza ambapo kipande cha kwanza Dar es Slaam - Morogoro kina urefu wa kilometa 300, kipande cha pili Morogoro - Makutupora chenye urefu wa kilometa 422, kipande cha tatu Makutupora - Tabora chenye urefu wa kilometa 368, kipande cha nne Tabora - Isaka chenye urefu wa kilometa 165 na kipande cha tano Isaka - Mwanza chenye urefu wa kilometa 341 na kipande cha sita Tabora - Kigoma chenye urefu wa kilometa 506.

Hata hivyo Prof. Mbarawa alisema kuwa TRC inaendelea na ukarabati wa reli ya kati kwa kipande cha Kaliua - Mpanda, ujenzi wa daraja kipande cha Kilosa - Gulwe pamoja na ukarabati wa maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Isaka kupitia mradi wa TIRP 2.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Amina Lumuli amefafanua kuwa bodi ya wakurugenzi ya TRC inaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 12, kifungu kidogo cha 1 (a) cha Sheria ya Shirika la Reli Na. 10 ya mwaka 2017 ambayo inakua na Mwenyekiti pamoja na wajumbe saba ambao wanatoka katika ofisi mbalimbali za Serikali.

“Kwa mujibu wa kifungu hicho wajumbe wa Bodi wanatakiwa kuwa na taaluma ya Uhandisi, Rasilimali Watu, Utawala na Biashara, Sheria, Uchumi, Fedha na Usafirishaji” alizungumza Bi. Amina.

Bi. Amina alieleza kuwa TRC ina jumla ya wafanyakazi 2974 kati yao 2688 ni wa ajira ya kudumu na 286 ni wa ajira ya mkataba.

TRC imekuwa na mchango mkubwa katika kutoa huduma za usafirishaji wa njia ya reli kwa jamii ambapo pasi na uendeshaji wa treni za abiria na mizigo kwa masafa marefu na treni za mijini pia TRC inaendelea na miradi ya ujenzi ukiwemo mradi mkubwa wa kimkakati wa SGR, mradi wa ukarabati wa reli ya kati kwa vipande mbalimbali pamoja na ukarabati wa vichwa vya treni na mabahewa.
 
Back
Top Bottom