BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,376
- 8,120
Wakati mikakati ya kuboresha huduma za afya ikiendelea kuwekwa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amebainisha dalili za kufa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutokana na kulemewa na madeni ya matibabu ya wanachama wake.
Akifungua mkutano wa siku tano wa kikanda wa kuwajengea uwezo kuhusu ugonjwa wa kipindupindu jijini hapa jana, Waziri Ummy alitaja magonjwa yasiyoambukiza ndiyo sababu kuu ya gharama kubwa.
“Kuongeza uelewa ni jambo la msingi, kwa mfano bima yetu ya afya (NHIF) inakaribia kufa kwa kuwa umeelemewa na ongezeko la madai yanayohusu NCD (magonjwa yasiyoambukiza),” alionya Ummy.
Magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha moyo, saratani, mfumo wa upumuaji na kisukari yanayochangia asilimia 71 ya vifo vinavyotokea duniani ambapo ni sawa na watu milioni 41 kila mwaka.
Akisisitiza kuhusu uelewa wa dalili za magonjwa na jinsi ya kujikinga nayo, Waziri Ummy alisema “fanyeni kuwa jukumu la msingi ili kuzuia kuenea kwa maambukizi, najua tutafanikiwa kupambana na kipindupindu katika nchi zetu.”
Kutokana na hali hiyo, waziri huyo ameiagiza NHIF kuachana na utaratibu iliouanzisha hivi karibuni wa kudhibiti idadi ya wagonjwa wanaohudhuria vituo vya afya.
Taarifa ya NHIF
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 11 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema wametumia Sh99.09 bilioni mwaka 2021/22 kulipia magonjwa yasiyoambukiza.
Alisema kiasi hicho ni sawa na asilimia 18 ya fedha zote zilizolipwa huku dawa za saratani na huduma ya kusafishwa figo (dialysis) zikitumia fedha nyingi zaidi. Alisema magonjwa yasiyoambukiza ni mzigo mkubwa kwa mfuko huo.
“Dawa za saratani zinaila zaidi NHIF. Haya ni magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha, kuna huduma ya kusafishwa damu kwa wagonjwa wa figo, tunatumia Sh35.4 bilioni kwa mwaka,” alisema.
Konga, alisema mpaka sasa mfuko huo una wanachama 4,831,233 sawa na asilimia nane ya Watanzania wote huku asilimia sita wakihudumiwa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) huduma nyingine za bima zikihudumia asilimia moja. Hata hivyo, alisema kuna udanganyifu mwingi unaofanywa na watoa huduma hali inayouumiza mfuko huo lakini wanapambana na hali hiyo.
“Udanganyifu upo na tumekuwa tukichukua hatua, tutasitisha mikataba itakayoonekana inahatarisha uendelevu wa mfuko. Tumekuwa tukichukua hatua ikiwamo kupiga faini, kuwaripoti wahusika katika mabaraza yao kuhakikisha tumelipia huduma halali kulingana na miongozo,” alisema Konga.
Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mashirika ya umma ya Machi 2022, inaonyesha NHIF ilipata hasara ya Sh109.71 bilioni.
Pia Soma: Waziri Ummy: Magonjwa yasiyo ambukiza yanauelemea mfuko wa bima ya afya
Chanzo: Mwananchi