Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi TASWA Media Day Bonanza 2024, Februari 10, 2024

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Majaliwa2.jpg

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa bonanza maalumu la waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini "TASWA Media Day Bonanza 2024" linalotarajia kufanyika Februari 10, 2024, Msasani Beach Club, Dar es Salaam, kuanzia Saa 3:00 asubuhi, ambapo pia kutafanyika uzinduzi wa Tuzo za Wanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2024 zinazotolewa na TASWA.

Kutokana na matukio hayo mawili, TASWA imemualika Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa na ameridhia kuwa mgeni rasmi kwenye shughuli yetu na atawasili eneo la tukio saa 8:00 mchana. Lengo la bonanza ni kuwakutanisha, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja, waandishi wote wa habari pamoja na wafanyakazi wa kada nyingine katika vyombo vya habari.

Kutakuwa na michezo ya riadha, ambayo itahusisha mbio za mita 100, mbio za kupokezana vijiti, kutembea haraka, kuruka chini, kukimbia na gunia, kukimbia na yai kwenye kijiko na kukimbia na glasi yenye maji.

Michezo mingine ni mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa pete yote ikichezwa ufukweni, kurusha tufe, kuvuta kamba, kuruka kamba, mchezo wa vishale, mpira wa meza, draft, pool table, bao, karata, rede, mdako, kupenya ndani ya pipa, kushindana kucheza muziki, kushindana kunywa soda, kushindana kufukuza kuku na kushindana kula ugali na kuku mzima wa kuchoma.

Kwa upande wa uzinduzi rasmi wa Tuzo za Wanamichezo Bora wa Tanzania kwa mwaka 2024, TASWA iliunda Kamati ya Tuzo chini ya Mwenyekiti, Jemedari Said, kamati hiyo tayari imeanza kazi na imefanya uteuzi wa Mchezaji Bora wa Januari, ambaye atatangazwa siku hiyo na kupatiwa zawadi yake.

Pia uongozi wa TASWA utatumia bonanza hilo kuzindua rasmi kamati zake ilizoteua kwa ajili ya kusaidia masuala mbalimbali ya kiutendaji, ambazo ni Kamati ya Mafunzo na Maadili chini ya Dk Egbert Mkoko, Kamati ya Fedha na Mipango inayoongozwa na CPA Shija Richard na Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu inayoongozwa na CPA Baraka Katemba.

Nyingine ni Kamati ya Katiba inayoongozwa na Boniface Wambura, Kamati ya Tuzo za Wanamichezo Bora iliyo chini ya Jemedari Said na Kamati ya Wanawake na Michezo inayoongozwa na Timzoo Kalugira.

TASWA inatarajia wageni zaidi ya 2,000 watashiriki bonanza na uzinduzi huo, wakiwemo viongozi kutoka vyama mbalimbali vya michezo, wanamichezo nguli wa zamani nchini na wadau wa masuala ya habari hapa nchini.
TASWA TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI_page-0001.jpg
 
Back
Top Bottom