Waziri azomewa na wasomi
2008-03-17 08:55:43
Na Juma Ng\'oko, PST, Mwanza
Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Lawrence Masha, ameonja joto ya jiwe baada ya kuzomewa na baadhi ya wahadhiri pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) cha jijini Mwanza.
Alizomewa baada ya kujikanganya kuitetea serikali kufuatia hoja iliyotolewa na mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Bw. Zitto Kabwe, iliyozungumzia usiri kwenye mikataba ya madini na namna ambavyo wananchi hawafahamu juu ya ukweli wa madini yao.
Mada iliyowasilishwa na Bw. Kabwe ilielezea mafanikio pamoja na matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta ya uchimbaji madini.
Bw. Kabwe tofauti na Waziri Masha, aliingia ukumbini saa 6:41 mchana na kushangiliwa, alisema pamoja na mapungufu mengine serikali haiko wazi katika kutoa taarifa zinazohusu pato wala mikataba ya madini.
Waziri Masha alizomewa hadharani kwenye mjadala aliposema serikali iko wazi katika kutangaza masuala mbalimbali yahusuyo madini.
Alisema Watanzania wasioelewa kuhusiana na mikataba hiyo ya madini ni wale wenye uelewa mdogo na ama hawasomi magazeti au hawasikilizi redio.
Alitoa maelezo kwenye kongamano ambalo alikuwa mgeni rasmi lililoandaliwa na SAUT ambapo pamoja na mambo mengine, alishiriki kwenye mdahalo kuhusu uimarishwaji sera ya madini, kilimo na uvuvi kuelekea katika uboreshaji wa mali asili nchini.
``Kama nilivyotangulia kusema, Mheshimiwa Kabwe ni rafiki yangu. Ila ninachotaka kusema ni kwamba siyo kweli kwamba watu hawasomi magazeti na hawasikilizi redio wakati serikali inapokuwa inatangaza masuala mbalimbali yanayohusu mikataba,`` alisema Bw. Masha na kuanza kuzomewa.
PST ilikuwepo na ilishuhudia Bw. Masha akizomewa mchana saa 7:52 wakati akijaribu kufafanua mada hiyo.
Mbunge huyo alisema kuwa karibu Watanzania wote wanaamini kwamba pato la taifa kutokana na sekta ya madini ni asilimia tatu kwa mwaka lakini bila kuwa na ufafanuzi wowote.
Bw.Kabwe ambaye pia alikuwa mgeni mwalikwa kwenye mdahalo huo alisema kuwa hali hiyo imesababisha wananchi washindwe kuamini kwamba taifa linafaidika na sekta ya madini, kwa vile mikataba na pato litokanalo na madini ni siri ya viongozi wa juu serikalini pamoja na wawekezaji wenyewe.
Alisema wananchi wanaoishi jirani na migodi hiyo hawafaidiki na madini hayo na kwamba wengi wao wanaishi chini ya pato la Sh. 1,000 kwa siku.
Alitoa mfano kwamba tafiti zinaonesha kwamba Wilaya ya Geita mkoani humu, ndiyo ilikuwa ya mwisho mwaka 2005 kwa umasikini wa kipato kitaifa.
`` Kwa mfano, takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 2005 Geita ndiyo ilikuwa wilaya ya mwisho kwa umasikini miongoni mwa wilaya zenye madini ambapo asilimia 62 ya wakazi wake waliishi chini ya Sh.1,000 kwa siku,`` alisema Bw. Kabwe.
SOURCE: Nipashe