mlaizer
JF-Expert Member
- Jan 31, 2011
- 233
- 41
UDAKTARI, Uanasheria na Uhandisi zimetajwa kuwa ni kada za utumishi zenye uzito mkubwa zinazostahili mshahara mkubwa kuliko nyingine. Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Ummashi, Hawa Ghasia alisema kada inayoongoza kwa uzito ni udaktari ikifuatiwa na Sheria na Uhandisi. "Tathmini ya kazi iliyofanyika serikalini mwaka 2000 inaonesha kuwa kada ya udaktari ilikuwa na uzito mkubwa ikilinganishwa na kada nyingine na ndiyo maana ikatengewa mshahara mkubwa ikilinganishwa na kada nyingine," alisema Ghasia. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) aliyetaka kufahamu vigezo ambavyo Serikali inatumia kutofautisha mishahara ya kada mbalimbali za watumishi wa umma kama vile walimu na madaktari. Machali alitoa mfano kwamba mwalimu mwenye Shahada analipwa Sh 400,000 lakini Daktari mwenye Shahada analipwa Sh 900,000 wanapoanza kazi. Alihoji kama hali hiyo siyo ubaguzi, inayowavunja moyo baadhi ya watumishi walio na viwango vya elimu sawa lakini wanalipwa kidogo. Waziri Ghasia alisema tofauti na viwango vya mishahara kati ya kada moja na nyingine inatokana na uzito wa majukumu uliofikiwa baada ya tathimini. Alisema uzito hupimwa kwa kuzingatia kiwango cha elimu na muda unaohitajika kupata elimu husika, uzoefu unaohitajika, usimamizi wa rasilimali mbalimbali, athari au umuhimu wa kazi, mazingira ya kazi na uhuru wa kufanya uamuzi wakati wa kutekeleza majukumu husika. Alisema utaratibu huo hutumika hata katika sekta binafsi na duniani kote na ndiyo unaotumika katika utumishi wa umma kupima tofauti ya majukumu miongoni mwa kada zilizopo katika utumishi wa umma. "Pamoja na kwamba viwango vya elimu miongoni mwa watumishi wa kada mbalimbali vinaweza kufanana, ni ukweli usiopingika kwamba uzito wa majukumu hauwezi ukalingana na kada nyingine," alisema. Akisisitiza kuwa hakuna ubaguzi katika kupanga mishahara ya watumishi, akisema; "kwa mfano, uzito wa kazi ya Daktari hauwezi kuwa sawa na uzito wa kazi ya Ofisa Utumishi pamoja na ukweli kwamba wote ni wahitimu wenye Shahada ya chuo kikuu." source:habarileo la 11/04/2012 NB:Kwa hoja hizi sekta zingine zitaendelea kudorora siku hadi siku,tofauti ya mshahara kwa zaidi ya mara mbili hauwezi kuhalalishwa kwa hoja hizi.Mwalimu ambaye ndiye anayewaandaa hao watumishi wengine wote ndiyo mshahara wake uwe wa mwisho? |