Licha ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, BoT, Profesa Benno Ndulu kutoa ufafanuzi juu ya madai ya kuajiriwa kwa watoto kadhaa wa vigogo wasio na sifa katika taasisi hiyo, bado bosi huyo ameendelea kubanwa.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa, wamesema kuwa baada ya kusambazwa zaidi kwa majina ya watu wanaodaiwa kuwa ni watoto wa vigogo waliojazana katika benki hiyo, sasa ni jukumu la Gavana Ndulu kutoa majibu yenye kufafanua juu ya ukweli wa kuajiriana `kishkaji` katika benki hiyo ama vinginevyo.
``Majina yanazidi kusambazwa. Ukifuatilia, kila kukicha unakutana na taarifa kwenye mtandao zinazoonyesha kuwa wakubwa wamewachomeka watoto wao pale na orodha ya baadhi ya watoto hao inafahamika.
Ni wakati muafaka sasa kwa Gavana kutoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na tuhuma hizo,`` akasema Bw. Abdallah Mashaka, aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Sinza Jijini.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kama Mama Alvin, mkazi wa Mbezi Tangi Bovu, ameiambia Alasiri kuwa mbali na Gavana kuuthibitishia umma kuwa watoto wa vigogo walio BOT wameajiriwa kutokana na sifa stahili, pia anapaswa kueleza bayana juu ya orodha hiyo inayosambazwa kwenye mtandao kama hao wanaotajwa humo ni waajiriwa wa taasisi yake ama la.
``Kama orodha tunayosambaziwa kwenye mitandao na pia kwenye simu zetu za mkononi ni ya kweli, basi kuna jambo... ni orodha ndefu sana.
Gavana anapaswa kutueleza ni kwa vipi wakawa wao tu, tena kwa idadi kubwa il-hali wapo pia vijana kibao waliomaliza hadi masters (shahada ya uzamili) na kutopata fursa hizo,`` akasema Mama Alvin.
Naye Mwenyekiti wa chama cha Wananchi, CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kwa hali ilivyo sasa katika taasisi nyingi za umma ikiwemo hiyo ya BoT, ni kwamba kuna ufisadi mkubwa wa ajira.
Amesema hata yeye ameiona orodha hiyo kwenye mtandao lakini akasema hana uhakika kama taarifa hizo ni za kweli au uzushi wa watu kupitia mtandao.
Ninachofahamu ni kuwa kuna uchunguzi uliwahi kufanyika BoT na watu kadhaa wakakamatwa wakidaiwa kughushi vyeti, ila hili la kwenye mtandao kwa kweli siwezi kulizungumzia kwa kuwa sina uhakika kama ni la kweli au la, akasema Prof. Lipumba.
Ametaka uchunguzi ufanyike haraka kuhusiana na ufisadi kwenye ajira kwa kuwa kumekuwepo na tabia ya kutoa ajira kutokana na kumjua mtu na si kwa kufuata vigezo vya taaluma ya mtu.
Hili suala la ufisadi naona linaingia hadi katika ajira, uchunguzi unatakiwa kufanywa katika nyanja hii ili kujua ukweli, akasema.
Aidha, katika `blog` kibao za mitandaoni, wasomaji wameendelea kulijadili suala hilo na kutuma maoni yao mbalimbali kuhusiana na kurundikwa kwa watoto wa vigogo BOT.
Mojawapo ya meseji tele za kwenye `blog`inasomeka hivi:
Kama kweli ni zoezi la kudumu hebu papaseni kwenye mabenki mengine na sekta za Serekali, mtazirai wenyewe.
Tanzania watu wanaishi kwa kuiba vyeti vya wengine. Hebu piteni piteni na mikoani, ndio kumejaa uozo kila mahali.
Watoto wa vigogo wamepachikwa kila mahali na ndio maana wasomi wengi hawana ajira. Kama unabisha, ingia Wizara za Elimu, Afya, Forodha na Uhamiaji, kweli kuna mambo.
Mwalimu anaulizwa swali na mwanafunzi anashidwa kujibu hadi akaulize wenzake, si makubwa hay?.
Najua itachukua muda kuwafichua lakini kama tuna nia ya kuijenga Tanzania basi wakati ni huu.Tufichue maovu yote ndani ya Serekali....