Nimemsikia Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji Mstaafu Warioba akidai kupitia ITV leo kuwa Mwalimu Nyerere hakuwa na mawazo mgando, na kwa maana yake, anataka kuhalalisha kuwa kama angekuwepo, Mwalimu angeunga mkono mawazo yao ya kuibuka na serikali tatu. Amedai kuwa endapo angekuwepo Mwalimu leo angekuwa amekasirika mno kutokana na Katiba iliyopo ilivyochezewa. Naweza kumuunga mkono kwa hilo lakini ni ukweli ulio wazi Mwalimu asingeunga mkono muungano wa serikali tatu kamwe! Ni udhalilishaji mkubwa wa mtazamo wa Mwalimu kudai kuwa Mwalimu angeunga mkono serikali tatu!! Sote tulikuwa hai wakati Mwalimu alipoingilia kati, tena kwa nguvu zake zote, na kuziua juhudi za kikundi cha 45 cha kuanzisha harakati za kuunda muungano wa serikali tatu, harakati zilizokuwa tayari zimeshaungwa mkono na Mzee Malecela akiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya utawala wa Mzee Mwinyi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba. Huu anaoutangaza hivi sasa Warioba ni udhalilishaji mkubwa wa mawazo na msimamo wa Mwalimu kuhusu muungano. Ukweli ni kwamba muungano chini ya serikali tatu sio muungano. Hauna mashiko na ni rahiusi mno kuuvunja akitokea kiongozi mkorofi kutoka upande wa Tanganyika au Zanzibar kuliko muungano katika mtindo uliopo sasa. Na Warioba pamoja na heshima zake, asiwadhalilishe wananchi wanaopinga mawazo ya kuwa na serikali tatu kwa kuwaita ni "wenye mawazo mgando"--kama anavyoupigia yeye debe muungano wa serikali tatu pia hao wana haki ya msingi na ya kikatiba kuupinga muungano wa serikali tatu. Akae akijua sio suala la gharama tu linalopigiwa kelele, ila ni suala la mashiko katika muungano wenyewe. Kwa mtazamo wangu anayeupigia upatu muungano wa serikali tatu, hautaki muungano! Ukweli ni kwamba pamoja na juhudi zote hizo za kuutetea muungano wa serikali tatu, lakini Warioba hayuko wazi kuhusu ni wananchi wangapi wanaoutaka muungano huo. In fact, katika wananchi wapatao laki 3 waliohojiwa na tume yake kutoka bara na Visiwani, ni watu wapatao 19,000 tu waliounga mkono muungano wa serikali tatu--hakuna uhalali wowote wa kimahesabu na kimantiki unaoweza kusema kwa kujiamini kuwa Watanzania sasa wanaulilia muungano wa serikali tatu. Kwa kuanzisha muungano wa serikali tatu, ni wazi kabisa tutadhoofisha mno uzalendo wa Utanzania, ambao miaka ya hivi karibuni umeanza kuimarika sana ndani na nje ya nchi. Hivi sasa bendera ya Tanzania inapepea katika madaladala, bodaboda, viwanjani na vitu vyenye alama ama bendera ya Tanzania vimeanza kutapakaa nje ya nchi!! Watanzania tuwe makini sana katika suala hilo--mvi sio hekima!!