Mtikila afanya kampeni za kumpinga Kikwete 2010
ADAIWA KUPITA MAKANISANI AKIMWAGA SUMU ASICHAGULIWE MWAKANI
Frederick Katulanda, Mwanza
JESHI la polisi nchini linamchunguza Mwenyekiti wa chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila kutokana na kufanya mikutano katika makanisa jijini Mwanza na kuwahimiza waumini kutoichagua CCM na Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jamal Rwambow, jeshi hilo linafanya uchunguzi kufuatia taarifa walizopokea kutoka kwa wasamaria wema kuwa mchungaji huyo yupo jijini Mwanza kwa muda wa majuma mawili sasa akiendesha mafunzo makanisani yanayodaiwa kuwa yanawahimiza waumini kutomchagua Kikwete pamoja na CCM katika uchaguzi ujao.
"Tumepokea taarifa toka kwa wasamaria wema, lakini bado tunazichunguza kujua ukweli wake; hivyo hatuna cha kueleza kwa sasa kwa vile bado tunafuatilia kwa kina ili kujua iwapo madai hayo yana ukweli," Kamanda Rwambow alisema jana wakati akizungumza na Mwananchi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Mchungaji Mtikila amekuwa akiendesha mikutano yake katika makanisa mbalimbali jijini Mwanza akifundisha mada mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi wa viongozi, ikiwa ni pamoja na kuwahimiza waumini kuikataa CCM kutokana na kushindwa kuuondoa ufisadi nchini.
"Moja kati ya mada ambazo amekuwa akitufundisha ni juu ya ufisadi na CCM, nchi kukosa maadili pamoja na suala la udini. Anaeleza kwa kina na anapambanua juu ya utawala wa awamu ya nne kushindwa kuongoza nchi kutokana na kuzidiwa nguvu na mafisadi," alieleza mmoja wa wachungaji wa Kanisa la Anglikana kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Mchungaji huyo alibainisha kuwa alihudhuria mafunzo ya mchungaji mwenzake Mtikila kanisani kwao hivi karibuni.
Alisema mpaka sasa Mtikila amekwishatoa mafunzo hayo kwa wachungaji na waumini wa makanisa mbalimbali ambayo yako chini ya Umoja wa Makanisa ya Kikristo nchini.
Akizungumza na gazeti hili Mchungaji Mtikila alikiri kuwa yupo mkoani Mwanza kwa lengo na madhumuni ya kufanya mikutano.
Alifahamisha kuwa amekuwa akitoa mada mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu ya uraia kwa waumini wa makanisa hayo ambayo alisema yamemwalika.
"Nipo hapa Mwanza kwa mwaliko wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo ambao waliniita kutoa elimu ya uraia. Hata hivyo nimeanzia Mwanza, lakini nitazunguka nchi nzima na katika mafundisho yangu nawaeleza waumini hawa wasiichague CCM na wala wasimchague Kikwete," alieleza.
Alisema katika elimu yake ya uraia amekuwa akifundisha mada moja kuu ya Wajibu wa Kanisa katika uongozi wa Nchi na Maadili ya Taifa na kwamba, amekuwa akieleza kwa kina na wazi kumomonyoka kwa maadili ya taifa na kukomaa kwa ufisadi nchini ambao umemshinda Rais Kikwete kuutokomeza; hivyo kuwahimiza wananchi kutomchagua yeye na chama chake.
'Umoja wa makanisa wananikusanyia waumini wao, mimi natoa mada, ninawaeleza wasiichague CCM na Kikwete na hili liko wazi. Nawaeleza sababu za kutomchagua kuwa ni ufisadi, kifo cha maadili na udini" alieleza Mchugaji Mtikila.
Hata hivyo, wakati Jeshi la Polisi likieleza kumchunguza Mtikila jana saa 4: 46 asubuhi mchungaji huyo akiwa na gari moja alionekana akiingia katika ofisi za Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza na kutoka saa 5: 30 baada ya kuzungumza naye.
Habari zaidi zimeeleza kuwa Mtikila alikwenda kuonana na kamanda wa polisi kutokana na kuambiwa kuwa jeshi hilo limeanza kufuatilia mafunzo yake katika makanisa anakopita.
Miongoni mwa makanisa ambayo wachungaji wake wameshiriki kwenye mafunzo hayo ni Anglikana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Soruce:Mwananchi
Habari hii niliiweka hapa jana jamaa anamwaga sumu