Wakuu wa mikoa watakiwa kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kabla ya Desemba 15

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,011
9,876
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka wakuu wa mikoa yote kuhakikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine ya elimu ambayo Serikali Kuu imeipatia fedha inakamilika kabla ya Desemba 15, mwaka huu.

Alitoa agizo hilo jana wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya alipofanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kayuki na Chuo cha Uwalimu cha Msasani.

Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao kila mmoja kusimamia miradi hiyo kwenye eneo lake la utawala ili wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari mwezi Januari wasikwame kwa sababu ya kutokamilika kwa vyumba vya madarasa.

Alisema serikali imeshatoa fedha nyingi za miradi hiyo zikiwamo za utekelezaji wa miradi ya Uviko-19 na kwamba lengo ni kuhakikisha matatizo ya sekta ya elimu yanapungua na wanafunzi wanasoma katika mazingira rafiki.

“Usipokamilisha miradi hiyo utakuwa umeshindwa kuleta matokeo chanya ambayo ndilo lengo la serikali, na usipoleta matokeo chanya tutakuwa wakali sana kwenye eneo hili, kwa hiyo nimeamua nitoe meseji kwenu leo,” alisema Majaliwa.

Hata hivyo amewataka viongozi hao kuhakikisha miradi hiyo inajengwa kwa viwango vinavyoendana na kiwango cha fedha zilizotolewa na kwamba ili kufikia lengo hilo ni lazima wahakikishe vifaa vinavyotumika ni bora.

Baada ya kutembelea vyumba vya madarasa katika Shule ya Wasichana ya Kayuki pamoja na Chuo cha Uwalimu cha Msasani, Majaliwa aliwapongeza wasimamizi wa miradi hiyo kwa madai kuwa waliisimamia vizuri na imejengwa kwa viwango.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, alisema walipokea zaidi ya Sh. bilioni 15.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa vyumba vya madarasa, miundombinu ya barabara pamoja na miundombinu ya afya.

Vilevile alisema hivi karibuni walipokea Sh. bilioni 1.7 ambazo zinatokana na tozo za simu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika halmashauri mbalimbali za mkoa huo.

“Maagizo yako Mheshimiwa Waziri Mkuu tumeyapokea na tutayatekeleza, lakini kwa zile fedha za tozo tumeshaanza kujenga vituo mbalimbali vya afya kikiwamo cha Kata ya Ndato,” alisema Homera.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, alisema serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu ya elimu ikiwamo vyuo vya ualimu, shule za msingi na sekondari.


NIPASHE
 
Back
Top Bottom