Wanafunzi 2, 000 warundikana kwenye vyumba 12 vya madarasa

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,379
8,123
1677860520440.png

Wanafunzi 2, 084 wa Shule ya Msingi ya Mvinza Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wanabanana katika vyumba 12 pekee vya madarsa vilivyopo shuleni hapo huku zaidi ya nusu yao wakikaa chini sakafuni kutokana na upungufu wa madawati.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mvinza, Zacharia Charles, mahitaji halisi ya vyumba vya madarasa kwa idadi ya wanafunzi waliopo ni vyumba 46; lakini vilivyopo ni vyumba 12 pekee, hivyo kufanya upungufu kuwa vyumba 31.

Kutokana na upungufu huo, Mwalimu Mkuu huyo anasema kati ya 80 hadi 150 wanalazimika kutumia chumba kimoja cha darasa kinyume cha Sera ya Elimu inayoelekeza chumba kimoja cha darasa kutumiwa na wanafunzi 45.

Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa madawati ambapo zaidi ya nusu ya wanafunzi wa shule hiyo huketi sakafuni kutokana na shule hiyo kuwa na madawati 184 pekee kati ya madawati 694 yanayohitajika.

Kwa hesabu za haraka ya dawati moja kukaliwa na wanafunzi watatu, shule ya msingi Mvinza inakabiliwa na upungufu wa madawati 510.

Matatizo yaliyopo shuleni hapo yaliibuliwa kupitia video iliyosambaa kupitia mitandao ya kijamii ikiwaonyesha wanafunzi wakiwa wanasoma nje huku wameketi chini ardhini ambako wamemwaga majivu kwa lengo la kutengeneza eneo (ubao) la kuandikia.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Isack Mwakisu, pamoja na sababu zingine, upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati katika shule ya msingi Mvinza unachangiwa na kuongezeka kwa idadi ya watu baada waliokuwa wanaishi ndani ya eneo la hifadhi kuhamishiwa Kijiji cha Mvinza.

Shule ya msingi Mvinza ilianzishwa mwaka 1975; mwaka mmoja pekee baada ya kuanzishwa kwa Kangu Kijiji cha Mvinza mwaka 1974.

Hatua za dharura na muda mrefu

Uongozi wa shule ya msingi Mvinza kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu umechukua hatua za muda mfupi na mrefu kutatua tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati shuleni hapo.

“Tumewagawa wanafunzi katika mikondo miwili; mkondo mmoja wa wanafunzi wa darasa la nne hadi la saba wanaingia shuleni asubuhi, huku wale wa darasa la kwanza na hadi la tatu wanaingia mchana. Hii ni hatua ya haraka kukabiliana na tatizo la mrundikano darasani,” amesema Mwalimu Mkuu.

Akizungumzia mipango ya muda mrefu, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Isack Mwakisu amesema Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu inatekeleza mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarsa ambapo tayari Sh100 milioni zimetolewa kujenga vyumba vinne vya madarasa shuleni hapo.

“Tayari ujenzi unaendelea. Pia Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa kushirikiana wadau wengine wa maendeleo wamepata madawati 200 kwa ajili ya Shule ya Msingi Mvinza,” amesema Mwakisu

Tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati pia linashuhudiwa katika shule zingine za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu yenye jumla ya shule 85 za msingi.

Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Msingi na Awali Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Elestina Chanafi, halmashauri hiyo ina upungufu wa vyumba zaidi ya 1, 000 vya madarasa kutokana na mahitaji halisi kwa ajili ya wanafunzi 90, 000 waliopo kuwa vyumba zaidi ya vyumba 2, 000 vya madarasa, wakati vilivyopo ni zaidi ya vyumba 700 pekee.

Kwa upande wa madawati, halmashauri hiyo inahitaji zaidi ya madawati 30, 000 lakini yaliyopo ni madawati 16, 000 pekee; hivyo kukabiliwa na upungufu wa madawati 14, 000.

MWANANCHI
 
Kwa hali hii walimu poleni, hapo ufundishe watoto wote waelewe!!!
Kwanini tunataka kuongeza Wizara? Kwanini tuna wabunge viti maalumu? Kwanini tunanunua magari ya gharama kwa watendaji wa Serikali? Kama hata madarasa tu tumeshindwa kujenga?
 
Back
Top Bottom