Wakulima walipwa bil. 68/- za korosho

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,011
9,879
Hayo yalibainishwa na Meneja wa MAMCU tawi la Masasi, Joseph Mmole, alipokuwa akizungumza na gazeti hili, kuhusu malipo ya zao la korosho kwa msimu wa 2019/2020.

Mmole alisema zaidi ya kilo milioni 47.3 za korosho za wakulima wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) katika Wilaya ya Masasi na Nanyumbu zimeuzwa kwenye jumla ya minada tisa.

Alisema katika minada hiyo tisa iliyofanyika kwa vipindi tofauti, wakulima hao wamelipwa zaidi ya Sh. bilioni 68.2 hadi sasa.
Mmole alisema malipo hayo kwa sehemu kubwa wamelipwa wakulima wa vyama vya msingi vilivyopo katika eneo la Halmashauri ya Mji Masasi pamoja na wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.

Alisema kwa mnada wa tisa na wa kumi, wakulima wameanza kulipwa fedha zao ambapo awali malipo hayo yalikuwa yamechelewa kidogo kwa sababu mbambali.

"Tunashukuru sana kwani katika misimu ya korosho ambayo tumefanya vizuri katika malipo ya korosho kwa wakulima ni wa 2019/ 2020 kwa sababu wakulima wengi wamelipwa fedha zao vizuri bila misuguano ya aina yeyote," alisema Mmole.

Alisema katika kuelekea kufunga msimu wa korosho 2019/2020, vyama 87 vya wilaya za Nanyumbu na Masasi vyama 41 kati ya hivyo vimeshafunga msimu kwa sababu kwenye maeneo yao korosho zimekwisha.

Mmole aliongeza kuwa ni vyama 46 pekee kati ya hivyo ndivyo hadi sasa vinaendelea kukusanya korosho za wakulima na kuzipeleka katika maghala makuu kwa ajili ya kusubiri minada kuziuza.

Alisema hadi sasa korosho za wakulima ambazo hazijaingizwa katika maghala makuu kutoka kwa wakulima ni kilo zaidi ya milioni 1.4, na kwamba muda wowote korosho hizo zitaingizwa katika maghala makuu kuuzwa.

Mmole alisema kwa msimu huu wa 2019/2020 hakukuwa na changamoto zozote kubwa ambazo zilijitokeza na hiyo ni kutokana na viongozi wengi wa AMCOS kuzoea mfumo wa sasa ukilinganisha na msimu uliopita wa 2018/2019.

Naye Bakari Said, mkulima kutoka Wilaya ya Nanyumbu, aliipongeza serikali kwa usimamizi mzuri wa zao la korosho, na kwamba wakulima wanaendelea kulipwa fedha zao bila vikwazo.

Chanzo: Nipashe
 
Back
Top Bottom