Wakili Kibatala, Shahidi walivyochuana taratibu za kumtambua mtuhumiwa

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
1687361512547.png

Dar es Salaam. Kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara na tajiri wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya imeendelea kuunguruma Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, huku wakili wa utetezi na shahidi wakikabana koo kuhusu gwaride la utambuzi.

Mchuano mkali wakati kesi hiyo ilipounguruma jana Jumanne Juni 21, 2023 ulikuwa ni kati ya wakili wa utetezi, Peter Kibatala na shahidi wa 12 wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi (Inspekta) Henry Kambalile katika kutafsiri na kuzingatia masharti ya Mwongozo wa Jeshi la Polisi (Polisi General Order – PGO).

Katika kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018, mjane huyo wa marehemu Bilionea Msuya, Miriam Mrita anatuhumiwa kumuua wifi yake, Aneth Msuya; yeye na mwenzake, mfanyabiashara Revocatus Muyella, maarufu kama Ray.

Aneth aliuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, miaka mitatu tangu kuuawa kwa kaka yake, Bilionea Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha Mashtaka, wakili wa Serikali, Generose Montano, Inspekta Kambalile kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Kinondoni, Oysterbay, alieleza kuwa ndiye aliyeandaa gwaride la utambuzi wa mshtakiwa wa pili, Muyella.

Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa katika gwaride la utambuzi, Muyella alitambuliwa na shahidi mtambuzi, Getruda Peniel Mfuru kuwa mhusika katika tukio la mauaji hayo.

Getruda alikuwa mfanyakazi wa ndani wa marehemu Aneth na shahidi muhimu anayetarajiwa kuitwa mahakamani kutoa ushahidi wake kwani anadaiwa kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa mauaji hayo.

Inspekta Kambalile alieleza kuwa wakati akiandaa gwaride hilo, Agosti 21, 2016, alikuwa akifanya kazi katika kituo cha Polisi Kilwa Road, akiwa na cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (ASP).

Alieleza kuwa siku hiyo asubuhi akiwa ofisini aliipokea maelekezo kutoka kwa mkuu wake, RCO Temeke, Mchomvu ya kuandaa gwaride la utambuzi.

"Alinitaka kuandaa na kusimamia gwaride la utambulisho, kuhusu kesi KGB/IR/2849/2016 kosa la mauaji. Mtuhumiwa alikuwa anaitwa Revocatus Everist. Alikuwa mahabusu katika kituo cha Polisi Kilwa Road," alidai Inspekta Kambalile.

Alidai kuwa baada ya kuona wajihi wa mtuhumiwa alitafuta washiriki wanne wenye uwiano sawa na mtuhumiwa kimaumbile na umri unaokaribiana ambao aliwapanga na mtuhumiwa akajitambulisha kwake na mtuhumiwa naye akajitambulisha kuwa anaitwa Revocatus Everist.

"Nilimuelezea haki zake za msingi kuhusiana na gwaride la utambulisho, kwanza kwamba ana haki ya kuchagua sehemu yoyote kati ya wale watu wanane, haki ya kubadilisha mavazi, kumuita ndugu, jamaa au wakili kuwepo wakati wa gwaride la utambulisho," alidai shahidi na kuongeza:

"Mtuhumiwa aliamua kubadilisha mavazi. Alibadilisha shati kutoka kwa wale washiriki waliokuwepo,”.

Kuhusu kumuita ndugu rafiki au wakili, Inspekta Kambalile alisema kuwa mtuhumiwa alimweleza kuwa hakuna shaka wanaweza kuendelea na zoezi na kwamba alichagua kusimama nafasi ya pili kutoka kulia.

Alidai kisha shahidi mtambuzi alipelekwa eneo la gwaride na WP Zakati, akajitambulisha kwake na shahidi akajitambulisha kuwa anaitwa Getruda Peniel Mfuru na kwamba kisha alimweleza kuwa jukumu lake ni kumtambua mtuhumiwa wa mauaji hayo.

"Nilimuelezea kuwa atapita mbele na nyuma endapo atamtambua mhusika anaweza kumgusa bega,"alidai shahidi huyo na kuongeza:

"Shahidi Getruda Mfuru alianza kupitia mbele na mstari wa nyuma baadaye akaenda kumgusa Revocatus Everist, akasema huyu ndio mhusika."

Inspekta Kambalile alidai kuwa wakati wa gwaride kulikuwa na Mwanga wa kutosha kwani lilifanyika asubuhi.
Alidai kuwa baada ya hapo alijaza fomu ya utambuzi namba PF186, majina ya washiriki wote wa gwaride, namba zao za simu na wakasaini.

Kisha Inspekta Kambalile alimtambua mshtakiwa mahakamani kwa kumgusa begani
“Ni huyu hapa mheshimiwa. Lakini pia naomba kwa ridhaa yako avue Baraka,”,

Mshtakiwa huyo alivua barakoa aliyokuwa ameivaa na shahidi akasema: “Ndiye mwenyewe mheshimiwa,”.

Kisha mshtakiwa huyo aliiomba Mahakama ikaipokea fomu ya utambuzi kuwa kielelezo cha nane cha upande wa mashtaka, kisha mshtakiwa akaisoma fomu hiyo maelezo yaliyomo.

Baada ya maelezo hayo ndipo ukafika wakati ule ambao mashahidi huwa hawatamani ufike, shahidi kuulizwa maswali ya dodoso kutoka upande kinzani. akaulizwa maswali ya dodoso na wakili Kibatala, yaliyojikita katika taratibu za uandaaji wa gwaride hilo na matumizi na uzingatiaji wa masharti ya PGO.

Sehemu ya mahojiano hayo baina ya wakili Kibatala na shahidi huyo, wakili Kibatala na mwendesha mashtaka na wakati mwingine Jaji anayesikiliza kesi hiyo Edwin Kakolaki akiingilia kati ama kwa kuwauliza maswali mawakili hao au kutoa mwongozo.

Wakili Kibatala: Kabla ya hili zoezi la kisheria (kuandaa gwaride la utambuzi) ulishawahi kushiriki zoezi lolote?
Shahidi: Hapana

Kibatala: Kwa hiyo hukuwa na uzoefu?
Shahidi: Sio suala la uzoefu bali la kisheria

Kibatala: Ni sahihi kuwa hili hatua zote zinetungiwa taratibu kwa mujibu wa PGO?
Shahidi: Ni kweli

Kibatala: Masharti yaliyowekwa kwenye PGO ni ya lazima au hiyari?
Shahidi: Ni ya lazima

Kibatala: Jukumu lako lilikuwa kusimamia parade (gwaride) kwa maoni yako au kwa mujibu wa PGO?
Shahidi: Kwa mujibu wa PGO

Kibatala: Nani alifanya hatua za awali kutafuta washiriki (wa gwaride)?
Shahidi: Ni mimi niliyefanya hatua hizo.

Kibatala: Wewe hukuwa officer Incharge of the case?
Shahidi: Ndio sikuwa Incharge.

Kibatala: PGO 232 inasema ‘officer Incharge’ ndio ataandaa na kuingiza taarifa zinazohusiana na gwaride, kuna changamoto kuelewa hayo masharti?
Shahidi: Hakuna.

Kibatala: Kwa ushahidi wako ni wewe uliyejaza hiyo fomu (fomu ya gwaride la utambuzi), siyo?
Shahidi: Ndio

Kibatala: Ulitii hayo masharti ya PGO?
Shahidi: Ndio kwani nilikuwa Assistant Insp.

Kibatala: PGO 232 (2) (a) Kuna maelezo ya Inspekta Msaidizi?
Shahidi: Leta nikusomee

Shahidi anasoma PGO 232 (2) (b)

Kibatala: Nimesema (a) huko (b) tutakwenda maana PGO yote iko hapa.
Shahidi: Anasoma (b) inasema gazetted officer na anayeendesha (gwaride) asiwe connected na kesi (asiwe anahusika)

Kibatala: Wewe ulikuwa connected na hiyo case?
Shahidi: Sikuwa connected

Kibatala: Ulimwambia Jaji kwamba wewe hukuwa connected?
Shahidi: Sikumwambia

Kibatala: Wewe ulikuwa gazetted officer (afisa wa polisi mwenye cheo cha kuanzia Mrakibu Msaidizi wa Polisi – ASP)?
Shahidi: Sikuwa gazetted

Kibatala: Ulimwambia Jaji kwamba kulikuwa na mazingira ya afisa asiye gazetted kufanya hilo zoezi (kuendesha gwaride la utambuzi)?
Shahidi: Sikumwambia sababu sheria iko wazi

Kibatala: Nakurudisha PGO 232 (a), kwa mujibu wa PE 8 (prosecution exhibit - kielelezo cha 8 Cha upande wa mashtaka, yaani fomu ya Polisi namba 186 ya taarifa za utambuzi wa mtuhumiwa) nani ulimtaja kama officer Incharge of the case (Kiongozi wa Upelelezi)?
Shahidi: Hakuna Incharge of the case.

Kibatala: Kwa mujibu wa PGO 232(c) jukumu la kumuarifu mtuhumiwa kufanyiwa utambuzi ni la nani?
Shahidi: Officer Incharge

Kibatala : Officer Incharge of the case ambaye tumekubaliana haikuwa wewe si ndiyo? Na kwa ushahidi wako hilo zoezi (kumtaarifu mtuhumiwa kufanyiwa gwaride la utambuzi ) ulilifanya wewe, sawa?
Shahidi: Ndio

Kibatala: Nikisema prejudice unaelewa?
Shahidi: Sielewi

Kibatala: Unafahamu ni madhara gani mtuhumiwa kufanyiwa zoezi hilo (kutaarifiwa) na asiye officer of the case?
Shahidi: Sielewi

Kibatala: Umesema mtuhumiwa alikwambia hakuwa na pingamizi (kufanyiwa gwaride la utambuzi) akija akikwambia wewe hakukukwambia kuwa ana pingamizi kwa sababu wewe hukuwa officer Incharge of the case maana anatakiwa kuambiwa na officer Incharge of the case utasemaje?
Shahidi: Sheria iko wazi kwamba kama ana objection (pingamizi) anamwambia Incharge ndo aniambie

Kibatala: Ndio maana nakuambia hakukwambia wewe kwa sababu huhusiki, utasemaje?
Shahidi: Sitasema kitu.

Kibatala: Unafahamu au hufahamu huyu uliyemgusa alikamatwa mkoani Arusha na hana ndugu Dar wala rafiki?
Shahidi: Mi Sifahamu.

Kibatala: Haukuwa na jukumu la kumweleza kuwa kama anataka amuite ndugu au jamaa, unafahamu ni jukumu la kwako?
Shahidi: Ndio

Kibatala: Wakati unatoa ushahidi wako ulimwambia Jaji kuwa ulimwambia mshtakiwa kuwa mna jukumu la kumweleza mtuhumiwa kuwa ana haki kuita ndugu kutoka Arusha?
Shahidi: Nilimwambia lakini sikumwambia kwa maneno yako hayo wewe.

Kibatala: PGO 232 (2) (f) unaelewa?
Shahidi: Nimekuelewa

Kibatala: Shahidi, hebu tukumbushe nani alikuwa ni msimamizi wa Getruda (kuhusiana na suala la gwaride la utambuzi kabla ya kupelekwa eneo la gwaride)?
Shahidi: WP (Polisi wa kike) Zakati.

Kibatala: Na tumekubaliana kuwa WP Zakati hakuwa connected katika hiyo case?
Shahidi: Ndio

Kibatala: Ulimwambia Jaji kuwa WP Zakati hakuwa anahusika katika hiyo kesi?
Shahidi: Nilieleza, hiyo ni IR ya Kigamboni na sisi Kilwa Road hatuhisiki (na kesi za kituo cha Kigamboni.

Kibatala: Kwa hiyo ufahamu wako IP (identification parade - gwaride la utambuzi) ilifanyika Kilwa Road kwa sababu ninyi ni neutral kwa sababu kesi iko Kigamboni?
Shahidi: Sio ufahamu wangu, ni kwa mujibu wa PGO.

Kibatala: Nani alimuita shahidi Getruda kutoka alikokuwa kuja kwenye paredi?
Shahidi: Afande Mchomvu (Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke, wakati huo?

Kibatala: PGO inasema wewe (Afisa msimamizi wa gwaride la utambuzi) ndio unapaswa kumuita, ulimuita wewe au alimuita afisa mwingine?
Shahidi: Mimi nilimuita.

Kibatala: PGO 232 (2) (l)ni masharti ya lazima ya PGO kwamba washiriki wa zoezi la utambuzi wanapaswa kuwa hawatambuani na anayfanyiwa utambuzi?
Shahidi: Nafahamu

Kibatala: Mwambie Jaji kama ulimweleza kuwa ulijiridhisha kuwa ( washiriki wa gwaride) hawahamiani na shahidi?
Shahidi: Nilimwambia kuwa nilichagua washiriki wanaokaribia kufanafana?

Kibatala: Swali langu umelielewa?
Shahidi: Ndio

Kibatala: Haya sasa mwambie Jaji wale uliowachagua (washiriki wa gwaride) ulimweleza Jaji kuwa ulijiridhisha kuwa hawafahamiani na Getrude (shahidi mtambuzi)?
Shahidi: Sikufafanua

Kibatala: Shahidi unajua kwa sheria yako OGO kwa nini hao watu hawatakwi kuwa wanafahamiana?
Shahidi: Nafahamu

Kibatala: Mwambie Jaji ni kwa nini?
Shahidi: For justice (kutenda haki)

Kibatala: Kwa mujibu wa PGO 232 (2)(s) inasema afisa anayeendesha gwaride ukimuuliza shahidi mtambuzi baada ya utambuzi kuwa ni kigezo gani umemtambua mtuhumiwa na yeye anayokujibu unapaswa kurekeodi kwenye hiyo fomu, hayo yapo?
Shahidi: Hayajarekodiwa

Kibatala:. PGO 232(2) (v), baada ya zoezi la utambuzi picha ya mnato inachukuliwa, ulitoa maelezo iwapi picha zilichukuliwa au hazikuchukukuwa nankamankukikuwa na mazingira ya kutokuchukua?
Shahidi: Sikumwambia kwa sababu siyo mandatory (siyo takwa la lazima)..

Kibatala: Kwa nini waandishi wa PGO walishauri kwamba baada ya paredi picha zipigwe?
Shahidi: Mimi sijui.

Kibatala: Ulitoa sababu yoyote kwa nini picha hazikuchukukuwa?
Shahidi: Sikutoa kwa siyo mandatory.

Kibatala: PGO 232(4), unaifahamu.kama ipo?
Shahidi: Nafahamu

Kibatala: Unafahamu masharti yake?
Shahidi: Sifahamu maana mimi sikuwa incharge.

Kibatala: Hapa mahakamani kuna mshtakiwa anaitwa Revocatus Everist Muyella, wewe uliyoelezwa na RCO kuwa Revocatus Everist ulimfafanulia Jaji kuwa huyo Revocatus Everist ndiye huyohuyo Revocatus Everist Muyella?
Shahidi: Sikuwambia

Kibatala: Umesema position ya mtuhumiwa (mahali aliposimama mtuhumiwa kwenye gwaride la utambuzi) alikuwa second (wa pili) kwa mujibu wa hiyo fomu umefafanua second from right au left (wa pili kutoka kulia au kushoto)?
Shahidi: From the right (kutoka kulia).

Kibatala: Kwenye hiyo fomu kuna maneno from the right?
Shahidi: Hapa haijaandikwa

Kibatala: Hiyo fomu Ina mhuri wa Kilwa Road?
Shahidi: Haina


Baada ya wakili Kibatala kumaliza kumhoji shahidi maswali ya dodoso, mweneldesha mashtaka, Wakili Montano alimuongoza tena shahidi kutoa ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa katika madodoso.Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Montano: Shahidi, uliulizwa kama fomu hiyo ina muhuri wa Kilwa Road ukssma hapana hebu ifafanulie Mahakama
Shahidi: Mheshimiwa Jaji chini ya PGO 232 suala la muhuri si takwa la lazima kwenye fomu ya utambuzi

Wakili: Shahidi pia uliulizwa kuwa kwenye hiyo fomu kuna jina la Revocayus Everist lakini kwenye rekodi za mahama ni Revocatus Everist Muyella hebu ieleze Mahakama.
Shahidi: Mheshimiwa jina nililopewa mimi ni Revocatus Everist.

Wakili: Pia uliulizwa kama Ulimwambia Jaji kwamba mlimwambia mtuhumiwa kuwa mna jukumu la kumtafutia ndugu au wakili ukajibi hukumwambia hebu ifafanulie mahakama.
Shahidi: Mheshimiwa kama.nilivyoeleza awali mtuhumiw nilimpa haki zake kwa hiyo ilikuwa ni hiyari yake kama akitaka awepo ndugu au jamaa lakini hakuhitaji.

Wakili:Shahidi pia uliulizwa kuhusu kwa nini hamkuchukua picha ya gwaride, hebu ifafanulie mahakama.
Shahidi: Mheshimiwa kama inavyojieleza PGO 232(2)b suala la kuchukua picha siyo mandatory hivyo hapakuwa na ulazima.wa kuchukua picha kwenye paredi.

Wakili: Pia Shahidi uliulizwa kuhusu PGO 232(2) (a) hebu ifafanulie kuhusiana na officer of the case na arrangements.
Shahidi: Mheshimiwa kama inavyojieleza preliminary arrangement (maandalizi ya awali ya gwaride la utambuzi) ni hatua za awali ambazo officer Incharge huwa anazifanya ikiwemo kuandaa eneo la paredi.
Pia ni kuhakikisha mtuhumwa na shahidi wanapatikan kwa ajili ya zoezi hilo la paredi ya utambulisho. Hizo ndizo officer Incharge anahusika.

Wakili: PGO232(2)(b) kuhusu officer Incharge of the case kuwepo kwenye paredi ifafanue
Shahidi: Mheshimiwa hii inasema officer Incharge of the case akiwepo ndo anaweza kuhusika lakini kama hayupo gazetted officer. Endapo gazetted hayupo office wa chini ya ASP asiye connected anaweza kuendesha hivyo nilikuwa nastahili kuendesha pared kwa PGO hii.

Kesi hiyo inaendelea tena leo Juni 21, 2023 kwa ushahidi wa shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka.

CREDIT: MWANANCHI
 
Kibatala hajawahi kushinda kesi yoyote.

Mbowe alikutwa na ugaidi mahakamani akiwa anatetewa na Kibatala.
 
Back
Top Bottom