Doctor Mama Amon
Platinum Member
- Mar 30, 2018
- 2,311
- 3,490
Na Waaandishi Wetu
BAADA ya kuanza kukua na kushika kasi kwa ajenda ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kutaka kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa 2025, wasomi, wanazuoni na wachambuzi wameibuka kuunga mkono.
Wengi wanaona umuhimu wa kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa ajenda ya Chadema kusitishwa kwa mchakato wa uchaguzi hadi kufanyika kwa marekebisho ili kuwepo uchaguzi huru na wenye haki sawa kwa kila chama, wagombea na hata wapiga kura.
Mchambuzi mahiri wa siasa, maendeleo, mwanadiplomasia Tanzania, Deus Kibamba ameshauri kwamba ni vyema bunge la mwisho kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu, lisivunjwe na badala yake liongezewe muda wa kutunga sheria ya mazungumzo ya taifa kuhusu uchaguzi.
Ameshauri muswada wa sheria kuhusu jambo hilo uitwe ‘The National Dialogue Act 2025.’ Lengo likiwa ni kutoa fursa kufanyika kwa mjadala wa kitaifa kuhusu marekebisho ya sheria za uchaguzi.
Kibamba anaseme katika mazingira yaliyopita na hata sasa, mchakato wa kufanyika uchaguzi na hata kutangazwa matokeo, kumepoteza maana, hivyo kunahitajika suluhisho la kudumu kupitia mjadala wa kitaifa utakaolindwa na sheria.
Akizungumza na Pambazuko mwishoni mwa wiki, Kibamba alisema hata ajenda inayopiganiwa Chadema, ya 'No reform - No election' imetokana na uchaguzi wa Tanzania kupoteza maana kwa kutokuheshimu uamuzi wa umma kupitia sanduku la kura.
Kibamba amesema kunahitajika watu wanaoitakia mema Tanzania wasaidie kufanya ushawishi ili jambo hilo lifanikiwe kuepuka umwagaji wa damu unaoweza kutokea endapo Chadema wataendelea na mikakati yao ya kuzuia uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Mchambuzi huyo ambaye pia ni mwalimu wa Chuo cha Diplomasia cha Dkt Ahmed Salim, anayefundisha masomo ya mazungumzona na maaridhiano, utatuzi wa migogoro na sheria za mikataba ya kimataifa, alisema uchaguzi Tanzania umepoteza maana kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo rushwa pamoja na uamuzi wa wananchi kupitia sanduku la kura kutoheshimiwa.
“Nitoe ushahidi; moja ni kwamba uchaguzi wenyewe unatakiwa uwe ni mchakato wa wananchi kuweka watu wachache washike mamlaka na pia uwezo wa kuwaondoa wanaposhindwa kutimiza wajibu wao, lakini hilo kwa sasa haliwezekani..."
“Agenda ya No reform - No election siyo ya mchezo, imewashika, hii ina madhara katika mfumo, nadhani umeona jinsi ambavyo watu wameanza kuropoka ovyo, wengine wanasema ‘watakinukisha’ hili likiachwa hadi Oktoba linaweza kusababisha mambo mabaya katika nchi yetu...”
“Ili tusifike huko kitu, pekee kinachoweza kunusuru hali hiyo ni meza ya mazungumzo itanuliwe, iwe ya kitaalamu na kisayansi na isiwe kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema pekee, bali makundi mengine..."
“Tumekwishajifunza kwani mazungumzo ya awali ya CCM na Chadema yalishindikana kwa sababu walikwenda kujifungia Ikulu peke yao, Chadema walighiribiwa nao wakaghiribika, hatutaki hayo yatokee tena," alisema mtalaam huyo wa diplomasia.
Akaongeza; "hayo yanayozungumzwa leo kuhusu umuhimu wa uchaguzi huru na haki yalianza mwaka 1991/1992 wakati Jaji Nyalali (Francis) alipewa kazi na Rais Ali Hassan Mwinyi (wakati huo), aliongoza tume iliyochunguza mfumo wa vyama vingi akabaini sheria 40 zilitakiwa kufutwa au kufanyiwa maekebisho kabla hatujaingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa..."
“Kwamba je, nini kinatakiwa kifanyike ili huo mfumo ufanye kazi vizuri, sasa bado tunajiuliza hilo hilo hadi leo, ili mfumo wa vyama vingi ufanye kazi vizuri.”
Aidha, Kibamba alisema No reform - No election ina mnyororo mrefu kuanzia kwa Tume ya Jaji Nyalalaji, uchaguzi mbalimbali uliowahi kufanyika ukiwemo ule kati ya mgombea wa CCM, Azim Premji na Walid Kabour wa Chadema mwaka 1994 Jimbo la Kigoma mjini.
Hayo yanayozungumzwa ilikuwa ni mwaka 1991/1992 Jaji Nyalali (Francis) alipewa kazi na Rais Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi) aongoze tume inayochunguza sababu za kukubali ama kukataa kuanza mfumo wa vyama vingi.
“No reform - No election ina mnyororo mrefu, ni kampeni ya nguvu, na ni kampeni ya maana kabisa isipokuwa wasiwasi wangu ni namna utekelezaji wake utakavyotekelezwa..."
“Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa Kwanza wa Tanzania) alikuwa anaongea lugha hiyo hiyo, alisema itakapofika mahala wananchi wakapoteza maana ya michakato muhimu kama uchaguzi, ina maana uchaguzi utakuwa hauna maana tena..."
“Kwa hiyo hawa Chadema wanaongea kitu cha uhalisia kabisa, binafsi hadi sasa nimekwishaangalia chaguzi 41 duniani, uchaguzi wa Tanzania nimeanza 1993 kule Kwahani, Zanzibar, uchaguzi wa vyama vingi nchini 1994 niliangalia uchaguzi kadhaa pia Tanzania Bara, niliangalia uchaguzi babu kubwa kule Kigoma Ujiji ambapo Azim Premj akichuana na Dkt. Aman Kabour, huko mambo yalikuwa mazito mno na fukuto la siasa likionekana bila kuwa na uhakika nani atashinda," ameongeza. Kitu gani kimebaki? Kibamba anaendelea;
"Yale niliyoyaona kwenye chaguzi hizo miaka hiyo, ndiyo haya haya malalamiko ya leo na hali ya mwaka 1994 ilikuwa nzuri kuliko leo, kwa sababu mapambano ya No reform - No election yalikuwa makali sana..."
“Hii kampeni aliwahi kuizungumzia Kabour na Dkt. Masumbuko Lamwai, hawa walikuwa wanamnukuu Jaji Francis Nyalali ambaye mwaka 1991 aliwahi kusema ili mfumo wa vyama vingi vya siasa uweze kuwa na maana na uweze kumea na kutekelezeka, lazima sheria 40 ziondolewe na zitungwe mpya..."
“No reform - No election ina mnyororo mrefu, yaani kwenye uchaguzi, wakuu wa wilaya ndio wanawaamrisha ma-OCD na wao wanawaamrisha mapolisi wakasimame kwenye vituo vya kupigia kura, wakuu wa wilaya ni wajumbe wa kamati za siasa za CCM, Tanzania tupo gizani katika siasa..."
“Hii kampeni ilitakiwa hata Steven Wasira (Makamu Mwenyekiti CCM) aiunge mkono kwa sababu hata CCM wenyewe huwa inawaumiza. Wasira aliwahi kumlalamikia Jaji Warioba kuwa uchaguzi fulani alipokuwa amegombea ulikuwa wa hovyo kabisa, kwamba ulikuwa feki..."
“Hapo alikuwa ‘amepigwa chini’ kule Bunda, sasa leo hii kinachomfanya mtu wa CCM aseme hakuna haja ya kubadilisha hizo sheria ni kwa sababu hazijamng’ata hizo sheria, kwamba zinampendelea yeye,”alisema.
Aidha, Kibamba aligusia hoja ya CCM kuhusu muda wa kubadilisha sheria za uchaguzi kwamba haupo ni hoja dhaifu kwa kuwa bunge linaweza kuongezewa muda ili kufanya maboresho muhimu ya mfumo wa uchaguzi ikiwamo sheria ya uchaguzi.
Wengine wakoleza Akizungumza na Pambazuko, Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Dkt. Isaac Safari alisema suala la baadhi ya wanachama wa Chadema kupinga mkakati wa No reform - No election, ni jambo la kawaida katika siasa na hasa jambo hilo likiwa ni geni lazima lipate upinzani.
Hata hivyo, alisema kama uamuzi huo ulipitishwa na mkutano mkuu au kamati kuu basi, hakuna mtu mwingine anaweza kuutengua hadi mkutano huo ukae tena.
“Slogan (kauli mbiu) hiyo ya ‘No reforms - No election’ ni shinikizo kabla ya uchaguzi na mabadiliko hayo ni muhimu, sasa katika siasa lazima mambo hayo yaibuke, lazima kuwepo na upinzani.
“Sasa hoja ni je hiyo slogan ilipitishwa na nani? Kama ilipitishwa na mkutano mkuu, basi hakuna mtu yeyote anayeweza kutengua hadi mkutano huo mkuu ukae ndiyo utengue,”alisema Dkt. Safari.
Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. George Kahangwa alizungumzia kampeni hiyo ya Chadema kuitisha kuitisha petition kutafuta saini za watu milioni 15 kupinga Uchaguzi mkuu ujao.
“Yamkini petition kama itapata idadi yote hiyo wanayotarajia itasaidia kuonyesha kwamba agenda husika si ya Lissu, au Chadema peke yake.
“Kama itakuwa na watu wengi kiasi hicho inatosha kuwa kauli ya umma, kumbuka hayati John Magufuli alishinda uchaguzi wa mwaka 2020 kwa kura 12,516,262. Hiyo ni kidogo kuliko milioni 15 zinazotafutwa na Chadema. Umma mkubwa namna hiyo, umefanikisha harakati katika nchi kadhaa,” alisema Dkt Kahangwa.
Chanzo: Gazeti la Pambazuko, Toleo Na. 116, Jumatatu, 07 Aprili 2025, uk. 1, 6-8.
