Wadau wanastahili kujivunia kwa kutangazwa siku ya Kiswahili Duniani lakini juhudi za kukikuza zinahitajika zaidi

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,014
1,040
VCG211164811812.jpg


Na Pili Mwinyi

Kiswahili ni lugha ambayo kwa sasa imejibebea umaarufu mkubwa sana duniani ikiwa ni mojawapo ya lugha zinazotumiwa zaidi na watu wa Afrika. Kwa makadirio kina wazungumzaji zaidi ya milioni 200 katika nchi nyingi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika na hata Mashariki ya Kati.

Lugha ya Kiswahili imepitia vipindi mbalimbali vya makuzi yake. Juhudi na mchango mkubwa uliotolewa na viongozi wengi waasisi ili kuhakikisha lugha hii inakua na kutambulika kimataifa, hazitasahaulika kwani sasa kimetanua mawanda yake na kuzungumzwa katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa. Waswahili wanasema “juhudi huzaa matunda”, ni kweli matunda sasa yanaonekana kwani Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika Mkutano wake Mkuu wa 41 ulipitisha rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

UNESCO imechagua Julai 7 kwasababu ina historia ndefu. Kwanza katika mwaka 1954 ilikuwa ni siku ambayo chama cha TANU chini ya uongozi wa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania, alitumia lugha ya Kiswahili kuunganisha watu katika mapambano ya uhuru. Baadaye rais wa zamani na baba wa taifa la Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta, naye alifuata mkondo kwa kutumia lugha ya Kiswahili kuhamasisha watu wa Kenya katika mapambano dhidi ya ukoloni.

Lakini mbali na hapo Julai 7 2000, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilifufuliwa ili kuibua upya moyo wa ushirikiano na mafungamano baina ya watu wa Afrika Mashariki zikiwemo nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambako lugha ya Kiswahili inazungumzwa zaidi. Baadaye Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zilijiunga na EAC na sasa ni nchi wanachama. Lugha ya Kiswahili ni mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Licha ya juhudi zilizofanywa na viongozi wa Afrika katika kukikuza Kiswahili, lugha hii ilianza kutambulika muda mrefu sana. Umoja wa Mataifa kupitia redio yake ulianzisha idhaa ya Kiswahili katika miaka ya 50, ambapo baadaye mwaka 1961 Redio China Kimataifa nayo pia ilianzisha idhaa ya Kiswahili na mwaka huu wa 2021 Idara ya Kiswahili ya redio China Kimataifa imefanya maadhimisho makubwa ya kusherehekea kutimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.

Kwa sasa licha ya kwamba nchi mbalimbali duniani zimefungua idhaa za Kiswahili, lakini pia lugha hii inaendelezwa na kukuzwa kwa kufundishwa katika vyuo mbalimbali duniani. Nchini China Kiswahili kimejijengea umaarufu mkubwa sana kwani mbali na kufundishwa na kutumika vyuoni pia kuna makampuni mengi yanayotumia lugha hii ya Kiswahili.

Kwa kutambua umuhimu wa Kiswahili duniani kama lugha ya mawasiliano ya kimataifa, siku hii itaadhimishwa na wadau wote. Hii ni fursa adhimu kwa lugha ya Afrika kutambulika na Umoja wa Mataifa. Tunafahamu kuwa lugha inaunganisha watu na pia lugha ni sauti za watu, hivyo kutambulika kwa lugha ya Kiswahili kimataifa kutafanya sauti za waafrika wengi ambazo muda mrefu zimekuwa chini tu hazisikiki, sasa kuweza kusikika na kupaa zaidi duniani.

Lakini matokeo haya yasiwe ndio mwanzo wa kuridhika na kubweteka, kwasababu tunafahamu kuwa Kiswahili bado kina mapungufu makubwa ya misamiati. Lugha ni sawa na binadamu, huzaliwa, hukua na kama haina watumiaji mwisho hufa. Katika kipengele cha kukua ni muhimu sana kwa wadau hasa wa Lugha kukitilia maanani. Kiswahili kinahitaji kukuzwa zaidi kwa kuongeza misamiati mipya, hasa ya kiteknolojia na kisayansi.

Tumeshuhudia wadau mbalimbali wanaojikita na masuala ya utafsiri na ukalimani kutoka lugha za kigeni kwenda Kiswahili, baadhi ya wakati hukumbwa na ugumu kutokana na upungufu wa misamiati, hivyo tunatoa wito kwa Mabaraza ya Kiswahili kujifunga kibwebwe na kuhakikisha lugha hii kweli inashiba na kubeba hadhi ya kimataifa.
 
Walimu wa kiswahili nchi nyingi duniani wanatoka Kenya, Tza tunafeli wapi?
 
Back
Top Bottom