Wachumi Washauri Kariakoo uwe Mkoa maalum wa kibiashara

benzemah

JF-Expert Member
Nov 19, 2014
1,504
3,034
Wataalamu wa uchumi wameshauri eneo la Kariakoo, Dares Salaam liwe mkoa maalumu wa kibiashara na pia mamlaka za serikali zinazohusika na biashara ziwe na mifumo inayosomana ili kuepuka migomo ya wafanyabiashara kwenye eneo hilo.

Walisema serikali inapaswa kuipa Kariakoo hadhi ya kuwa Mkoa Maalumu wa Kibiashara na Uchumi kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa nchi kama ilivyo kwa mji wa Guangzhou nchini China. Mchambuzi wa uchumi, Goodluck Ng'ingo alisema Kariakoo inatakiwa uwe mkoa maalumu wa kibiashara wenye Meneja wake wa Mkoa wa TRA na Meneja wa Biashara wa Mkoa wa TRA wenye mamlaka kamili.

"Kariakoo haipaswi kuendeshwa vile, serikali ifanye kuwa mkoa maalumu wa kibiashara, lengo la kodi ni kusaidia kuchochea uchumi ukue siyo kuua biashara, pia kodi inapaswa kuwa rafiki," alisema Ng' ingo.

Mchambuzi mwingine, Gabriel Mwang'onda alisema Kariakoo inapaswa kupewa kuwa eneo maalumu la kiuchumi ambalo serikali itakuwa inaliangalia kwa ukaribu ikiwemo kutoitoza kodi mizigo inayoingia hapo ila mizigo itozwe inapotoka kwa kuwa maeneo kama hayo yapo nchi nyingi duniani ikiwemo China.

"Sidhani kama itakuwa busara kuendelea na mfumo uliopo pale Kariakoo, hauna afya sana, tuone juhudi za serikali kwenye kulihuisha na kulifanya soko liwe la kisasa zaidi," alisema Mwang' onda.

Pia alisema sheria iliyotumika kuanzisha soko la Kariakoo inaangalia zaidi soko lililoungua, hivyo kuna haja ya kuiboresha ili iweze kuwajumuisha wenye maduka na maghorofa yanayofanya biashara nyingine.

"Takwimu za mwaka 2015 zilionesha shilingi takribani bilioni 10 zinapita mikononi mwa watu kwa siku moja, ni soko kubwa, linatakiwa liangaliwe kwa upekee," alisema Mwang'onda.

Aidha, Ng'ingo alisema kutosomana kwa mifumo kati ya Mamlaka za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Ofisi ya Mkemia. Mkuu wa Serikali na mamlaka nyingine kunazalisha urasimu.

"Kwa mfano ukitaka kutoa mzigo bandarini, lazima TBS, TMDA, Ofisi ya Mke-mia Mkuu, Tanroads, TRA, waukague, lakini hawa wote wana mfumo unasomana? Huo mfumo haupo, hatimaye mteja anaona anatengenezewa urasimu," alisema Ng'ingo. Alisema masuala yote yanayohusu ukusanyaji wa kodi za TRA yanatakiwa ku-fanyika bandarini badala ya kukusanya kwenye vizimba Kariakoo na hakuna haja ya kuwa na kikosi kazi cha kukusanya kodi Kariakoo.

"Kodi ya mapato inatokana na mahesabu ambayo kila mtu anafunga mwishoni mwa mwaka, na yanafanyiwa hesabu za kikaguzi, kwa hiyo hutakiwi kutumia kikosi kazi kukusanya kodi ya mapato kwa sababu maduka yanauza bidhaa zilizopita Bandari ya Dar es Salaam," alisema Ng'ingo.
Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi alisema mgomo unaathiri uchumi hivyo ni vyema serikali na jumuiya za sekta binafsi kuwa na mazungumzo mara nne kwa mwaka.

"Wafanyabiashara lazima wakubali kwamba kuna wafanyabiashara wengine wanaokwepa kodi kwa kutumia njia za panya, pia kuna mizigo inaingia kama ya kupita kwenda nje lakini ikifika njiani inapakuliwa inarudi Kariakoo, kwa hiyo nao waache tabia ambazo zitaifanya serikali kutowaamini, waheshimu sheria," alisema Profesa Moshi.
 
Back
Top Bottom