Vitu kadhaa bado vinawatesa watu wa mkoa wa Kigoma, hili ni swala la Uraia

Kigoma Region Tanzania

JF-Expert Member
May 25, 2021
229
593
Ni wakati wa kubadili mwelekeo kukomesha ubaguzi wa kimfumo, ni muhimu kwa nchi kupitisha "ajenda maalum ya mabadiliko ili kung'oa ubaguzi wa kimfumo juu ya ukiukaji wa haki za kibinaadamu, kiuchumi, kijamii, kitamaduni, kiraia na kisiasa unaowakabili watu wa asili ya mkoa wa Kigoma.

Mijadala mingi imeshatolewa kunako kudhoofishwa kwa wenyeji wa mji wa Kigoma, hivyo ni muhimu serikali sasa kukomesha mifumo iliyokita mizizi tangu uhuru wa Taifa hili.

Tunahitaji mtazamo wa mabadiliko ambao utakabiliana na masuala yanayoingiliana ambayo yanachochea ususuwavu kwa watu wa Kigoma na yanarejea tena na tena.

Bado Mkoani Kigoma tunasumbuliwa na kasumba ya Uraia tangu uhuru!

Je nchi yetu haina mfumo wa utatuzi wa swala hili ambalo limekua ni kero na linazidi kukomaa siku hadi siku? Kigoma imekua ni sehemu ya Rushwa za Uraia, kesi za uraia na mambo mengine kadhaa yenye maudhi.

Kasumba ya Uraia kwa watu wa Kigoma haijaishia mitaani tu bali imejikita hadi kwenye mifumo ya Serikali. Ikiwemo upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa watu wenye asili ya Kigoma ni mtihani mkubwa, Upatikaji wa hati ya kusafiria ni changamoto kubwa kwa watu wenye asili ya Kigoma. Ukijiingiza kwenye siasa ndio kabisaa ujiandae kwa mashambulizi ya kesi za uraia.

Sisi tunafikiria kukusanya wanasheria 50 wenye asili ya mkoa wa Kigoma ambao watakua wakijikita zaidi katika kesi zote za uraia zitakazo mkabili mtu yeyote wa Kigoma popote pale alipo.

Lakini kabla ya kufikia huko Serikali iangalie namna ya kukomesha swala hili kabla hali haijawa mbaya zaidi, moyo wa mtu huwa unavumilia manyanyaso kisha huchoka. Maofisa waserikali ndio wanatakiwa wawe marafiki na raia ili kwa wao kuwasaidia kupata taarifa muhimu, nasio Maofisa wanageuka kua maadui, wanakua na viburi, wananyanyasa raia wao na kuwadhuru.

Je! kuna sheria inayosema utoe uhai wa mtu kwakosa la uraia??

Serikali iunde kikosi kazi maalum ambacho kitakomesha mashambulizi haya ya uraia yanayojitokeza mara kwa mara hapa mkoani kwetu. TAKUKURU tupieni jicho la 3 mkoa wa Kigoma.

Haipendezi katika safari ya BUS kusimamishwa na kuanza kukaguliwa, kuhojiwa na kutiliwa mashaka, je kuna ulazima gani wa kufanya haya?

1700389669774.png


Treni ndio chombo kikubwa cha usafiri, mbona hakuna ukaguzi wa uraia kwenye treni? mbona hakuna ukaguzi wa uraia kwenye ndege?

Ukataji wa tiketi za Mabus uambatane na masharti ya kuwa na kitambulisho kama vile kwenye Treni ili kuepuka kuwasimamisha watu kwenye safari, wamechoka na kuanza kuwahoji na kuwakagua kana kwamba mkaguzi ndio mwenye nchi na msafiri ni mkimbizi.

Tunafahamu kwamba sisi tupo mpakani, tena tumepakana na nchi zenye machafuko ya mara kwa mara, je serikali inajipanga vipi kuhakikisha kwamba raia wake wa Kigoma watabakia kua na matumaini makubwa ya wao kutambulika bila kutiliwa mashaka ya uraia wao? bila kukaguliwa mara kwa mara? bila kuhojiwa kwa kupindukia kama mikoa mingine? bila kusumbuliwa katika vitambulisho? bila kubughudhiwa katika kibali cha kusafiri? Serikali inafikiri nini juu ya jambo hili lenye utata kwa muda mrefu?

Hivi raia wa kigeni anadhibitiwa uraiani au anadhibitiwa mipakani? kwanini sasa raia halali wanasumbuliwa? huyu mgeni kafikaje uraiani bila kupitia mipakani? inamaana hakuna ulinzi wa mipaka? je nani awajibishwe ikiwa raia wakigeni atapatikana mtaani? mwenyeji ndio asumbuliwe au walinzi wa mipaka ndio wawajibishwe?

Na ikiwa tunaruhusu watu hadi wanaingia uraiani je hapo kweli tuna ulinzi? kama watu hao ni wahalifu si tayari wameshaleta madhara makubwa? Kwanini asumbuliwe raia tena uraiani nyumbani kwake?
Vijana wengi wa mkoa wa Kigoma hawapati nafasi za kutumikia taifa kwa kisingizio cha uraia wao unamashaka. Inahuzunisha.

Vijana wengi wanahofia hata kurudi nyumbani akifikiria swala la ukaguzi wa uraia kwenye BUS atalopanda.
Mkaguzi anakagua mapua ya watu, kwamba hili pua ni la Kongo hili ni la Burundi na hili ni la Tanzania, anakagua ufupi na urefu wa watu, muonekano na muundo wa nywele, uvaaji n.k: Je hizi ndio simple procedures za kumtambua mkimbizi? Ukaguzi ni wa hisia zaidi kuliko uhalisia.

Mnasema Muha ni Mrundi na Mmanyema ni Mkongo hivi mnafahamu Mwl Julius Nyerere alikua anafikia nyumba ya nani hapa Kigoma?

Kwamba nikiwa na ndugu Burundi basi na mimi ni mrundi ndio kigezo cha uraia hicho? kwamba nikiwa na ndugu Congo basi nami ni Mkongo ndio procedures hizo za kumtambua raia kwakua ana ndugu Kongo basi huyu sio raia wa Tanzania?

Ila nikiwa na ndugu Marekani mimi sio Muamerika na pia nikiwa na ndugu Saudia mimi sio Msaudia.
Wangoni na Wayao ni wengi Malawi kuliko Tanzania, Wadigo na Waduruma na Wamasai ni wengi Kenya kuliko Tanzania. Hayo ni makabila yanapatikana pande zote mbili mbona huko hakuna usumbufu kama kwa watu wa Kigoma.?

Je mimi mtu wa Kigoma siruhusiwi kuoa au kuolewa Burundi? Siruhusiwi kuoa au kuolewa Congo? Siruhusiwi kufanya biashara na warundi au Wacongo? Maana hata wakija na vibali halali bado mnawafuata kwenye nyumba za wageni kuwasumbua.

Sasa leo inafikia Raia wa Tanzania anauwa huko Israel tunapiga kelele ilahali raia huyu huyu anauwawa kinyama chini ya maofisa wa serikali na kuzikwa halafu tupo kimya.

Kijana wetu Enos Elias alikamatwa na maafisa uhamiaji wilaya ya Kakonko, aliokotwa katika kijiji cha Chilbo kata ya Kasanda akiwa amesha kufa na kuzikwa hukohuko alikookotewa kwa idhini ya polisi.

Tar, 11/11/023 mwili huo wa kijana Enos Elias ulifukuliwa kwa kibali cha mahakama, na mama mzazi wa marehemu aliutambua mwili huo kuwa ni wa mwanae.

Tar 14/11/023 kijana Enos Elias amezikwa tena kwa mara ya pili.

Tar 18/11/023 Maofisa wa 4 wanashikiliwa kwa mahojiano kunako tukio hilo la mauwaji.

Tunaomba sheria ifuate mkondo wake na mambo haya yadhibitwe. Sisi tunapenda sana ulinzi na tunaitakia sana amani nchi yetu lakini majukumu ya maofisa wanajichukulia sheria mkononi badala ya kufuata miongozo na maadili ya taaluma zao.

Enos Elias
1700389825047.png

Mama Enos Elias
1700389875012.png
 
Back
Top Bottom