Elections 2010 Viongozi wa dini watoa tahadhari

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
headline_bullet.jpg
Wasema maisha binafsi ya wagombea si hoja
headline_bullet.jpg
Wataka uchaguzi wa amani, kukubali matokeo
headline_bullet.jpg
Chadema yawasilisha NEC mashitaka dhidi ya CCM



Dini%281%29.jpg

Mgombea urais wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akisalimiana na Sheikh Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum, wakati wa mkutano wa viongozi wa dini na chama hicho. Kulia ni Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laiser na kushoto ni mgombea mwenza wa Chadema, Saidi Mzee.


Viongozi dini nchini wameasa kwamba masuala binafsi kuhusu wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hayapaswi kuwa na nafasi kwa sasa na badala yake wananchi waangalie sera na wagombea watakaoweza kutatua changamoto zinazolikabili taifa.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Mhashamu Paul Ruzoka, pamoja na Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church (AIC) wa Dayosisi ya Shinyanga, John Nkola, waliyasema hayo kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, walipokuwa wakijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya mkutano wao na viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Askofu Ruzoka alisema kuzungumzia maisha binafsi ya wagombea sio hoja inayoweza kuleta manufaa kwa taifa na kwamba kinachopaswa kutazamwa ni sera za vyama na uwezo wa wagombea.
“Hatuoni kama ni hoja ya msingi kuzungumzia maisha ya mtu binafsi, kila mtu ana mapungufu,” alisema.

Askofu Ruzoka alisema kuwa yeye na viongozi wa dini waliwaeleza viongozi wa Chadema umuhimu wa vyama vya siasa kufanya kampeni za amani na kukubali matokeo kwa lengo la kuepukana na machafuko yanayoweza kutokea.

Kwa upande wake, Askofu Nkola, alisema kama kila mgombea ataangaliwa maisha yake binafsi, hakuna ambaye hatakuwa na kasoro.

“Hata ninyi waandishi wa habari mngefuatiliwa kila mmoja wenu maisha yake binafsi, nani angepona? Kila mtu ana mambo yake binafsi … haya sisi tunayaona kama ‘non-issues (mambo yasiyo na maana), kinachopaswa kuangaliwa ni sera ambazo zinaweza kututoa hapa tulipo,” alisema.

Mgombea ambaye amekuwa akiandamwa tangu kuanza kwa mchakato wa kampeni za uchaguzi ni Dk. Willibrod Slaa, anayewania urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chadema anayedaiwa ‘kupora’ mke wa mtu, Josephine Mushumbusi.

Hata hivyo, viongozi hao hawakutaka kuzungumzia changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa kwa kueleza kuwa: “Ninyi waandishi mnayajua zaidi matatizo tuliyonayo na mnayaandika kila siku, wananchi wanatakiwa kuangalia sera ambazo zinaweza kutukwamua.”

Akizungumzia sababu za kukutana na viongozi wa Chadema, Askofu Ruzoka ambaye alikuwa mkuu wa msafara wa viongozi hao wa dini, alisema ni kuwakumbusha wagombea umuhimu wa kuzingatia sheria ili kudumisha amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu.

Alisema ni jukumu la kila chama hususani wagombea wa nafasi mbalimbali kuendesha kampeni kwa kuzingatia kanuni na sheria za uchaguzi ili kudumisha misingi ya amani nchini.

Alisema tayari viongozi wa dini wamekwisha kwenda Zanzibar na kuzungumza na Maalim Seif Hamad Rashid anayewania urais visiwani humo kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF) pamoja na Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.

Viongozi hao wa dini wanajumuisha Masheikh kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Wakristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na maaskofu wa makanisa ya Pentekoste.

Miongoni mwa viongozi waliokuwepo kwenye mkutano huo ni Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salim na Sheikh Thabit Jongo kutoka ofisi ya Mufti Zanzibar.

Wengine na sehemu wanapotoka kwenye mabano ni Askofu Augustino Shayo (Jimbo Kuu Katoliki la Zanzibar), Askofu Thomas Laizer (KKKT Dayosisi ya mkoani Arusha), Askofu Peter Maduki (mratibu wa tume ya viongozi hao), Askofu Edgar Mbegu (Kaimu Katibu Mkuu-TEC), Askofu John Mapesa (CCT-Dodoma), Askofu John Sylvester (TEC) na Damas Mfoe (Katoliki Zanzibar).

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipongeza utaratibu uliofanywa na viongozi wa dini wa kuamua kuzungumza na viongozi wakuu wa vyama vya siasa na kueleza hofu yao juu ya ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi.

Mbowe aliituhumu CCM kwamba inatumia nguvu ya dola kukiuka kanuni na sheria za uchaguzi.
Alisema CCM kinatoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wake ‘Green Guard’ ambao alisema wamekuwa wakiwafanyia vurugu na kuwaumiza wafuasi wa Chadema.

Alitahadharisha kwamba iwapo vijana hao wataendelea kufanya vurugu: “itafika mahali watu wetu watashindwa kuvumilia.”

Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema, alisema wameamua kuwaeleza viongozi hao ukiukwaji wa kanuni unaofanywa na wapinzani wao, hususani waraka uliosambazwa kwa wasimamizi wa uchaguzi nchi nzima ukiwaelekeza kuhakikisha CCM inashinda.

Alisema taarifa walizonazo kwa sasa zinaeleza kwamba CCM imetuma timu ya watu wake kwa viongozi wa dini ili wakiwezeshe kushinda katika uchaguzi ujao.

“Tumeahidi kuendelea kuwaelimisha watu wetu juu ya haki na wajibu wao, lakini tumewaambia lazima haki itendeke kwenye uwanja wa kampeni na tumetahadharisha kwamba kama hili halitatendeka, amani inaweza kuvunjika,” alisema.

Mbali na Mbowe na Dk. Slaa, ujumbe wa Chadema katika mazungumzo hayo pia uliwahusisha Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika, Mkurugenzi wa Halmashauri na Bunge, John Mrema na mgombea mwenza, Said Mzee Said.

Chadema waishitaki tena CCM NEC

Wakati huo huo, Chadema, kimewasilisha malalamiko yao kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupinga mgombea wa urais kupitia CCM, Rais Jakaya Kikwete, kuendelea kufanya kampeni mpaka saa moja usiku badala ya saa 12:00.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mkurugenzi wa masuala ya Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema, alithibitisha chama chake kuwasilisha malalamiko hayo juzi mchana kupitia kwa mwanasheria wa Chadema alitemtaja kwa jina la Esater Dafi na kwamba yalipokelewa na Nec kwa kusaini kitabu cha kupokelea barua.

Hata hivyo, alipoulizwa Mwenyekiti wa Nec, Jaji Lewis Makame, alisema hajapata taarifa ya Chadema kuwasilisha malalamiko yao.

“Bado sijapokea malalamiko unayosema Chadema imeyawasilisha kwetu kupinga mgombea wa CCM, Rais Kikwete kufanya mikutano ya kampeni zaidi ya saa moja usiku,” alisema Jaji Makame.

Juzi mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza kusudio la chama chake kuwasilisha malalamiko hayo kwa Nec ndani ya saa 24 kwa Kikwete kufanya mikutano yake ya kampeni nje ya muda wa kisheria.

Alisema mojawapo ya mikutano iliyofanywa na Rais Kikwete nje ya muda wa kisheria, ni pamoja na ule wa mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Shinyanga, ambao alidai kuwa Rais Kikwete alihutubia hadi saa 1.30 usiku.

Mkurugenzi wa Nec, Rajabu Kiravu, kila alipotafutwa jana kuthibitisha kama malalamiko hayo yamepokelewa, simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila kupokelewa.




CHANZO: NIPASHE

haya tena Viongozi wa Dini mpeni kura zenu Dr Slaa
 
Viongozi wa dini siwaelewi kwa sababu wanataka kubariki wizi wakati amri ya saba ya Mungu inasema usiibe. Ilibidi washikilie kubadilishwa kwa katiba ya Tanzania ambayo inabariki wizi wa kura za Urais kwa chama tawala kwa kusema NEC ikimtangaza mshindi wa Urais basi hakuna mahakama yenye mamlaka nchini ya kuchunguza ushindi huo wa Urais. Kwa nini kukataza uchunguzi kama CCM si wezi? Kwa nini kukataza uchunguzi kama CCM ni kama Obama anavyowafikiria?
 
Kuijua Qoran au Bible siyo kigezo cha kujua sheria na kanuni za nchi.
Tunawaheshimu kama viongozi wetu kiroho lakini tukiwa ktk medani za kisiasa lazima warudishje heshima kwa wenye utaalam wa hizo siasa hasa taratibu na muundo.

KURA zikiibiwa siyo haki hata kidogo kumtangaza aliyeiba ameshinda. walipaswa waseme hivyo
 
Kuijua Qoran au Bible siyo kigezo cha kujua sheria na kanuni za nchi.
Tunawaheshimu kama viongozi wetu kiroho lakini tukiwa ktk medani za kisiasa lazima warudishje heshima kwa wenye utaalam wa hizo siasa hasa taratibu na muundo.

KURA zikiibiwa siyo haki hata kidogo kumtangaza aliyeiba ameshinda. walipaswa waseme hivyo

Kwa taarifa yako AT THE END OF ALL LIVES there is Bible and Qoran, usilewe siasa mpaka hujui nafasi za dini katika maisha ya binadamu!!
 
Back
Top Bottom