SEHEMU YA 34
Naseku hakutaka kuelewa kitu, aliamini kabisa kulikuwa na tatizo kwa watoto wake na hivyo kutaka kuangalia kile kilichokuwa kimepigwa tumboni mwake, hali ya watoto wake kwani alichohisi ni kwamba walikuwa wamefariki dunia.
Bado Cassian alikataa, msimamo wake ulikuwa uleule, alijua kwamba kama mke wake angekiona kile kilichokuwa kimetokea kwa mapacha wake basi angeumia kupita kawaida.
Naseku hakukubali, bado alihitaji kuona tena huku akilia kabisa kitu kilichomfanya Cassian kumpa karatasi ile ngumu na kuangalia kilichokuwa kikiendelea.
Hakuamini, watoto wake mapacha waliokuwa tumboni mwake walikuwa na kila dalili za kuungana. Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini alichokuwa akikiangalia lakini wakati mwingine alihisi kwamba hata kama wangeungana, bado wangeweza kuwatenganisha kwa kuwa tu walikuwa na pesa.
Hiyo ndiyo hali iliyokuwa imetokea, kila mmoja alihuzunika mno, mioyo yao iliuma, ilichoma kupita kawaida.
Wakakumbatiana na kumshukuru Mungu kwa kuamini kwamba kila kitu kilichokuwa kikitokea, Mungu alikipanga na kamwe hakukuwa na mtu wa kufanya vinginevyo.
Mara kwa mara walikuwa wakifika hospitalini hapo kwa ajili ya kuangalia watoto wao ambao bado hawakuwa wamezaliwa, Cassian alikuwa na muda mwingi wa kuangalia picha za mapacha walioungana kama watoto wake ambao hawakuzaliwa, alitaka kuangalia maisha yao, waliishi vipi na hata mavazi yao yalikuwaje.
Hapo ndipo akaamua kuwafuatilia mapacha wa aina hiyo, Abby na Brittany Hansel waliokuwa wakiishi nchini Marekani. Kila alipoziangalia picha za mapacha hao moyo wake ulimuuma, hakuamini kama kweli Mungu aliamua kumpa watoto wa namna hiyo na wakati alikuwa amemuomba kwa kipindi kirefu mno.
“Mungu! Kama Abby na Brittany wanaishi, nina uhakika hata watoto wangu wataishi pia,” alijisemea Cassian huku akiangalia picha za mapacha hao, hakuishia hapo tu bali aliangalia za wengine wengi ambao wote kwa pamoja walimgusa sana moyoni mwake.
Siku zikaendelea, Naseku hakuonekana kuwa na furaha, muda mwingi alionekana kuwa na huzuni mno. Mama yake alitumia muda mrefu kumtia moyo, hakuataka kumuona akiwa kwenye hali hiyo kila siku.