Sehemu ya 119
Walker alitia huruma, moyo wake ulikuwa ukimfikiria mpenzi wake, Patricia, alimpenda, kwake, msichana huyo alikuwa kila kitu. Bado hakuamini taarifa za madaktari kwamba mpenzi wake asingeweza kukumbuka kitu chochote wala kusimama kama ilivyokuwa zamani, wakati mwingine alihisi kwamba alikuwa kwenye ndoto mbaya na ya kusisimua ambapo baada ya muda fulani angeshtuka na kujikuta akiwa kitandani.
Kama kulia, alilia sana lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika. Siku ziliendelea kukatika, kila siku alikwenda hospitalini hapo akiwa na pacha wake, Walter. Alihitaji kumuona mpenzi wake kitu ambacho baada ya siku tatu kuukatika, madaktari wakawaruhusu kuwaona.
Macho yake yalipotua kwa msichana huyo aliyekuwa kitandani hoi, hakuamini, alimsogelea na kumwangalia vizuri, hakuonekana kama alikuwa mzima, alionekana kama mfu kitandani pale. Alilia zaidi, akamsogelea na kumkumbatia.
Alijiona kuwa kwenye wakati mgumu, alijihukumu kwamba yeye ndiye aliyesababisha hayo yote kwani bila yeye Patricia asingesafiri mpaka nchini Marekani na kupata ajali hiyo.
“Patty! Wake up and talk to me,” Patty! Amka na uzungumze nami) alisema Walker huku akiendelea kulia.
Siku hiyo ilikuwa kimya, siku ziliendelea kukatika huku kila siku wakifika mahali hapo. Kwenye magazeti, mitandao ya kijamii na sehemu nyingine kila kona walikuwa wakiwazungumzia watu wao. Kila mmoja alimuonea huruma Walker, kwa jinsi alivyokuwa na pacha wake walipaswa kupata fulana maisha yao yote lakini kitu cha ajabu kabisa kilichokuwa kikiendelea kilikuwa ni maumivu makali.
Baasa ya siku kumi na sita kupita ndipo Patricia akayafumbua macho yake na watu wa kwanza kabisa kuwaona walikuwa mapacha hao hata kabla ya wazazi wake. “Patricia! Hatimaye umeamka,” alisema Walker huku akitabsamu.
Msichana huyo alinyamaza, hakukumbuka kitu chochote kile, alikuwa akiwashangaa, hakujua watu hao walikuwa wakina nani na walihitaji nini kutoka kwake.
Wazazi wake waliokuwa na nyuso za furaha hasa baada ya kumuona akiwa amefumbua macho wakamsogelea na kumwangalia, hata nao pia, Patricia hakuwa akiwakumbuka, alibaki akiwashangaa tu.