Sehemu ya 96
Siku nzima polisi walikuwa barabarani kuhakikisha kwamba mtu aliyekuwa akitafutwa, Edmund anapatikana kwa hali na mali. Hakukuwa na polisi aliyejua kwamba gari moja miongoni mwa magari yaliyotaka kuingia nchini Wales lilikuwa na mtu aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.
Kila mmoja alichoka, hawakuamini kama kweli mwanaume huyo alikuwa njiani kuelekea huko, walichokijua ni kwamba aliendelea kuwa Uingereza hivyo hata kwa jinsi walivyokuwa wakiyakagua magari mpakani hapo, hawakukagaua kama ilivyotakiwa kuwa.
Edmund akapewa kofia kama ya Malboro na dereva yule, akaivaa na kuanza kulisogeza gari kule walipokuwa polisi. Kila mmoja alichoka, walihitaji kuondoka kuelekea nyumbani kwani tangu asubuhi walikuwa mahali hapo, walizikumbuka familia zao, umakini wa kupekua magari uliwatoka na hivyo kuruhusu magari hata kama hawakufanya ukaguzi ambao ulitakiwa kufanyika.
Polisi alimuona Edmund akiwa na kofia, hakumjua, hakutaka kumkagua sana, ilikuwa ni usiku na mwili wake ulichoka mno. Hata kumwambia kuvua kofia ile ili amwangalie vizuri hakuwa na muda huo, akamulika tochi ndani ya gari kizushi, tena kwa haraka na kuliruhusu gari hilo kupita.
Edmund mwenyewe hakuamini, alihisi kama yupo ndotoni, alimwangalia polisi yule kwa makini, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyeliruhusu gari hilo kupita pasipo kufanyika ukaguzi kwa makini kama ambavyo ulitakiwa kufanyika.
Wakapita kirahisi kabisa, na baada ya dakika kadhaa gari likasimishwa nje ya hoteli kubwa ya Wales King ambapo Edmund akateremka, akaelekea mapokezi na dereva yule, akachukua chumba kwa ajili ya kwenda kupumzika.
“Utachukua chumba nikulipie?” aliuliza Edmund huku akimwangalia dereva, bado alimuhitaji, walikuwa na safari ndefu ya kuelekea katika Kituo cha Treni cha Bravein kwa ajili ya kupanda treni na kuelekea nchini Ireland.
“Haina shida. Nichukulie cha chini kabisa, ila kwanza ngoja niende baa kunywa,” alisema dereva huyo na Edmund kufanya hivyo.