SEHEMU YA 91
Edmund alihisi kabisa mtu aliyemshika bega kwa nyuma alikuwa akimfahamu na ndiyo maana aliamua kumfuata na kumtaka ageuke ili atambulike na kukamatwa.
Wakati mapigo ya moyo yakimdunda kwa nguvu tena huku akitetemeka, mara zikaanza kusikika kelele kutoka kwa binti mmoja aliyetoka chooni, alikuwa akikimbia kwa mwendo wa kasi.
“A bomb....a bomb...” (bomu...bomu...) alisema msichana huyo huku akikimbia kutoka chooni.
Vichwa vya Waingereza wengi vilikumbuka tukio ambalo lilitokea mwezi uliopita jijini Manchester ambapo kituo cha treni kililipuliwa kwa bomu lililowekwa na Waarabu kutoka Mashariki ya Kati.
Waliposikia hivyo, hakukuwa na mtu aliyebaki, kila mmoja akaanza kukimbia kwa hofu kuyaokoa maisha yake. Pale polisi wale waliposimama, wakashtukia wakikumbwa na watu waliokuwa wakikimbia, walipoinuka, Edmund hakuwepo, naye aliungana na watu wengine kukimbia.
Ilikuwa ni balaa ndani ya kituo hicho, watu wakatawanyika, si wale wanaosimama kwenye kizuizi, bali kila mtu aliyekuwa ndani ya kituo hicho ambao walikuwa ni zaidi ya elfu tatu, walikimbia kuelekea nje.
Edmund hakutaka kurudi, pale alipofika, akalikuta gari lake lakini hakutaka kulifuata, akahisi kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakilifuatilia na kutaka kuona ni mtu gani ambaye angeingia ndani ya gari hilo.
Alichokifanya ni kutembea kwa mwendo wa kasi huku watu wengine wakiendelea kukimbia hovyo. Alipofika umbali fulani, akasimamisha teksi, akaingia na kuondoka.
“Kuna nini?” aliuliza dereva teksi, alishangaa kuona watu wakikimbia huku na kule.
“Kuna bomu!”
“Kuna bomu! Wapi?”
“Kituoni!”
“Acha utani!”
“Kweli! Kuna bomu humo!”
Edmund akamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuondoka salama katika kituo kile pasipo kugundulika. Safari iliendelea, alipokuwa akielekea, hakupajua, wakati mwingine alijisikia kumwambia dereva kwamba wazunguke tu mpaka pale ambapo giza lingeingia.
Wakati wakiwa wanaendelea kuzunguka ndipo akapata wazo kwamba aondoke mpaka nchini Ireland kwa kutumia gari kwani wangepitia katika daraja kubwa lililokuwa likipita kutoka Uingereza mpaka Wales ambapo huko kusingekuwa na kazi kubwa ya kwenda huko.