SEHEMU YA 56 “Ninao!”
“Unao hapo? Niambie upo wapi nikufuate,” alisema Cassian.
“Naogopa!”
“Unaogopa nini?”
“Utanikamata!”
“Sikujua! Umenisaidia, uliagizwa kuwaua watoto wangu, hukufanya hivyo, kwa maana hiyo umenisaidia, siwezi kukumata. Nakuahidi hata kuja huko nakuja na mke wangu tu. Usiogope, niambie upo wapi,” alisema CAssian.
Alimaanisha, alichokuwa akikihitaji kilikuwa ni watoto wake tu, japokuwa Sikujua alikuwa akiogopa lakini hakuwa na jinsi, akawaambia mahali alipokuwa na mwanaume huyo kwenda huko kuwachukua watoto wake.
Njiani, hakukuwa na aliyeamini, hawakujua ni kwa namna gani walitakiwa kumshukuru Sikujua ambaye alitumwa kuwaua lakini hakutaka kufanya hivyo kwa kuwa tu moyo wake ulijikuta ukishikwa na upendo wa ajabu, huruma ambayo haikuwahi kumpata kabla.
“Mke wangu! Usilie, ngoja tukawachukue watoto wetu,” alisema Cassian huku akiendesha gari kuelekea Magomeni.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika huko, kwa maelekezo ya msichana huyo, wakatokea nyumbani kwake alipokuwa akiishi na kuingia ndani. Hawakuamini, waliwakuta watoto wao wakiwa kwenye kochi sebuleni huku kukiwa na chupa ya maziwa pembeni.
Haraka sana Naseku akawasogelea, akawabeba kisha kuwakumbatia. Huzuni aliyokuwa nayo moyoni, kilio alichokuwa amelia kwa siku tatu mfululizo kikapotea, furaha ya ajabu ikamuingia moyoni mwake.
Cassian akamsogelea mke wake na kumkumbatia. Wakati hayo yote yakiendelea, Sikujua alikuwa pembeni, alionekana kuwa na hofu nzito moyoni mwake, aliteteka, hakujiamini, aliona kama mwanaume huyo angemfanyia jambo lolote lile baya.
“Hutakiwi kuogopa Sikujua,” alisema Cassian huku akimwangalia msichana huyo.
Walimshukuru msichana huyo kwa wema wake, hawakuwa na cha kumlipa kwani kwa kuwaokoa watoto wao walimaanisha kwamba hiyo ilikuwa ni zaidi ya pesa, kilikuwa kitu kikubwa ambacho hata kama wangemlipa milioni mia moja bado isingelingana na kile alichowafanyia.
“Unataka tukufanyie nini?” aliuliza Cassian huku akimwangalia Sikujua.
Msichana huyo hakuhitaji kiasi chochote cha pesa, kitu pekee alichokihitaji ni kuwa huru tu.