Uzushiiii! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uzushiiii!

Discussion in 'Jokes/Utani + Udaku/Gossips' started by MziziMkavu, May 19, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 19, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,615
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  TUKO kijiweni kama kawaida, tunawaza jinsi nji inavyokwenda, tunafikiria malumbano haya yanayoanzia makanisani na misikitini na kuangalia mustakabali wa nji hii, ambayo ina Serikali isiyo na dini lakini watu wake ni waumini na waamini na wengine watambikaji.

  Haya yako juu ya vichwa vyetu, hivyo hayatumalizii muda wetu, kwa kuwa sisi wa vijiweni ni nadra kumsikia hata mmoja wetu akizungumzia kuwa siku moja atakuwa mjengoni pale, ajikamua, akijikakamua na kutunisha mishipa ya shingo kulalamikia yaliyoshindikana miaka hiyo.

  Sisi tunachoamini ni bora kono lifike midomoni kutumbukiza kitu na siku ipite, jua lipatwe lisipatwe hilo halituhusu, tunachoangalia hapa ni kama maisha yetu yatalindwa na kakipato ketu haka ka ngama, kama kanaweza kuzungusha mwezi, ambayo haijawahi kutokea kwetu.

  Ukishapata kaujira kako, ikikaribia katikati ya mwezi, ujue utamtafuta mtu wa kukukopesha kama huna mchezo na wenzako katika kibarua chenu wa kukopeshana kwa mzunguko, ambao kwa kweli hauna lolote zaidi ya kupunguza machungu kwa kipindi kifupi na kupeana fursa ya kushika fedha nyingi kwa wakati mmoja.

  Inakusaidia nini kama mtakuwa sita na mzunguko ukukute baada ya watano wengine kupata! Si ni ile ile pesa yako ndiyo inakusanyika na baadaye kupewa siku moja huku huko nyuma ulishajitengenezea maadui kibao kwa kuwakopa!

  Lakini hapa tunatafakari jinsi ya usajili huu wa simu za mkononi na kufikiria mbali zaidi kuona kama kweli huu ni usajili tu kama usajili, eti wa kubana wanaotukana na kutishana kupitia vilongalonga au kuna ajenda ya ndani zaidi!

  Tunashukuru pia kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya nji hii, kampuni hizi zinajitolea kufanya kazi bila malipo! Unashangaa kuwa nchi hii ambayo inauza hata maji ya kunywa, inatoza pesa hata mtu anapotaka kujisaidia haja ndogo, leo kuandikisha iwe bure! Ama kweli Watanzania wanaanza kubadilika, hivi huruma hii imetokea wapi? Tujiulize kama si kajimtego fulani ka kutuvuta halafu tuingie wenyewe.

  Mnakumbuka ule mtego wa zamani wa kukamata videge fulani vilafi vya mtama na uwele? Mnamwaga uwele au mtama au ulezi mahali fulani, mnaweka tenga lililofungwa kamba na kuegeshwa kwa kijiti halafu mnakaa mbali ili wakifika wasihofie kukamatwa, wakishatanguliza ulafi wao na kujikusanya kudonoa, mnavuta kamba, kijiti kinachomoka wanafunikwa.

  Hebu angalieni katika nji hii tajiri wa kodi, mnadhani mkishasajili tayari katika Daftari la Kudumu la Wenye Vilongalonga, baada ya Desemba mna uhakika kuwa Bunge la Bajeti la mwisho mwakani, Mustafa hatakuja na mapendekezo ya kodi! Atahanikiza:

  "Mheshimiwa Spika katika kipengele cha kodi, tunapendekeza kuwa kila mwenye simu ya mkononi alipe kodi ya Ongezeko la Thamani na Kodi ya Kusukuma Ujumbe wa Mkono, ili kufidia ile ekstrimuÂ… Serikali itapata mapato ya shilingi fulani..." Mpo hapo? Niambieni mtakimbilia wapi wakati mlishaingia katika Daftari la Kudumu na asiyelipa kodi, mawasiliano yanakatika, utaacha kweli na umezoea kubofya na kuwasiliana na washikaji zako saa za chombeza na ninyi wa ekstrimu?

  Thubutu... mchekwe! Wakati tunalifikiria hili, mara kinaingia kichokoraa kiko mbio kinalia na kuhanikiza eti baba yake kazushiwa huko nje eti mchawi, kinalia na kugaragara chini mpaka kinatoa ushuzi, tunashangaa na kukinyamazisha, kinaendelea kulia.

  Mara anaingia mwingine aliyekuwa anakifuatia anajitambulisha kuwa ni rafikiye anayesimulia eti kuwa dogo alikuwa akipita karibu na klabu cha ulaka, akasikia wazee wanamsema baba yake, eti ni mwanga wa kutupa na anatoka na ungo usiku kwenda kuwanga.

  Tunamuuliza huyo wa pili anasema ni uzushi tu usio na maana na wanamjua fika kuwa baba wa kijana huyu ni Mcha Mungu anayesali ile mbaya na kwamba hao waliokuwa wakizusha hivyo, ni walevi tu tena wanaomwonea wivu.

  Nasi tunashangaa kwa nini hayo, wakati tunamfahamu vizuri mzee huyu kwa heshima, staha, msaada na kwa kweli huruma aliyonayo kwa wenzake na hivyo tunapuuza uzushi, kwa kuwa ni uzushi hauna sababu ya kuukomalia. Lakini dogo anahanikiza mpaka sauti inamkauka.

  Tunaona kero na kumwambia aache uchuro na kumnyamazisha na kumwambia kelele zake ndizo zinaweza kusababisha watu waamini kuwa kweli faza ni bonge la mwanga, na kusababisha hata watu wasimtembelee kwake na ikibidi wamtenge katika masuala mbalimbali ya jamii.

  Lakini badala ya kukaa na kutafakari kuwa tunachomwambia ni cha ukweli, badala ya kutusikiliza, he, anaibuka na matusi kibao mpaka ya nguoni, anasema anampenda dingi wake na hivyo anataka watu hata wa mabondekwinama huko wajue kuwa kazuliwa jambo.

  Tunamuuliza kwa faida ya nani, anapiga kelele na kusema anatuheshimu sana na alidhani tutamuunga mkono kuwa alichofanya cha kulia, kupiga kelele na kutuchafulia hewa ni cha busara, lakini tunachokifanya anaona ni kinyume kabisa cha utaratibu.

  Anataka hata uzushi nasi tuuamini kuwa ni wa kweli. Hana adabu! Sisi tulichomwambia na kumwonya ni kuwa hatutaki malumbano na mabishano kwani kufanya hivyo watu hawataiona tofauti yetu na yeye, hatuwezi kukalia uzushi na fitna za watu mitaani na hasa wanapokuwa walevi!

  Na kama anawaamini wao, basi aende amtafute baba yake amwambie kuwa ni mwanga, akione cha moto. Tuliamini kuwa hata baba yake atamwona hana maana kukumbatia uzushi na kuusambaza kama alivyofanya, kitendo ambacho kilimwonesha kuwa kumbe ni mtu asiyeweza kufikiria na anaweza kuchota chochote kama lile dudu sukumamavi; mnalijua? Mjukuu wa Burito kuna mahali mwaka fulani aliulizwa na paparazzi, eti tunasikia wewe unamuunga mkono Mzee wa Kiraracha?

  Akajua tu haya ni ya uzushi yale yale akamjibu, hivi nikikwambia mimi ni baba yako utaamini na kukubali? Paparazzi domo pwaaa! Si ndio uzushi huooo? Tulipomwangalia kijana huyu akataka kusema jambo, lakini akaachia udenda tu na kutamka "mimi nilikuwa nawaaminini sana kuwa ni watu mnaelewa na ni mahiri katika mambo haya kumbe hamna lolote, mniache nilivyo."

  Nasi tukamwambia nawe tuache tulivyo na si saizi yetu. Kalaga baho na uzushi wako. Mnaonaje hili la simu? Mtakapoanza kulipia kodi ndipo mtakoma ubishi. Mkimaliza hii mtasajili redio, mtasajili televisheni, ili mradi mlipie kila kitu na hakuna atakayebisha, kwa sababu kama mnalipia kujisaidia sembuse vitu hivi? Yaani msikilize redio burebure tu hivi, mmwangalie Masako akikodoa macho runingani hivi hivi tu bwerere! Kasema nani? Alamsiki. (JK).
   
 2. Ndibalema

  Ndibalema JF-Expert Member

  #2
  May 19, 2010
  Joined: Apr 26, 2008
  Messages: 10,916
  Likes Received: 131
  Trophy Points: 160
  Du! ndefu hiyo!
   
 3. Papa Mopao

  Papa Mopao JF-Expert Member

  #3
  May 19, 2010
  Joined: Oct 7, 2009
  Messages: 3,354
  Likes Received: 387
  Trophy Points: 180
  Anazungumzia uchumi wa JK
   
 4. senator

  senator JF-Expert Member

  #4
  May 19, 2010
  Joined: Aug 9, 2007
  Messages: 1,927
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 133
  Kuna kaukweli flani katika huu uzushi!!
   
 5. Katavi

  Katavi Platinum Member

  #5
  May 19, 2010
  Joined: Aug 31, 2009
  Messages: 39,474
  Likes Received: 4,134
  Trophy Points: 280
  lakini ina ujumbe!
   
 6. F

  Fernandes Rodri JF-Expert Member

  #6
  May 19, 2010
  Joined: Apr 11, 2009
  Messages: 407
  Likes Received: 38
  Trophy Points: 45
  Maisha ni mafupi mno, ninaomba musiandikage articles refu kama hizo
   
 7. Azikiwe

  Azikiwe Senior Member

  #7
  May 20, 2010
  Joined: Nov 13, 2009
  Messages: 191
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Aaah ndefu sna, mtu ndefu kama hizi zaweza sababisha mtu kufutwa kazi.
   
Loading...