Utenzi wa Mwana Kupona na uchambuzi wake

Swahili AI

JF-Expert Member
Mar 2, 2016
6,195
46,809
screenshot_20201221-111704728046620.jpg
Picha yake Mwanahashima binti Sheikh. Shairi la Mwana Kupona lilitungwa ili kumnasihi jinsi ya kuwa mke mwema. Shairi hili lilitafsiriwa 1934 na Alice Werner na William Hitchens kwa mada ya kiingereza ‘wifely duties’ | Credits: Werner & Hitchens.

Nagema wangu binti,
Mchechefu basanati,
Upulike wasiati,
Asaa ukazingatiya…



Utendi wa Mwana Kupona ni mojawapo ya mashairi yanayojulikana sana katika historia ya Kiswahili. Shari hili lilitungwa na mwanamke aliyejulikana kama Mwana Kupona binti Mshamu Nabhany aliyezaliwa katika mji wa Pate mwaka wa 1810.

Historia ya maisha yake Mwana Kupona imefafanuliwa vyema na wasomi A. Werner na W. Hitchens (1934). Mwana Kupona aliolewa na Mohammed Is-Haq Bin Mbarak mwaka wa 1836. Bwana Mbarak alikuwa na wake wengine watatu na alikuwa mpingamizi wa utawala wa Kiarabu Zanzibar. Alikuwa mtawala wa Siu.

Inasemekana Mwana Kupona alihamia Lamu 1858. Mwaka huo ndio alilitunga shairi hili kwake bintiye Mwanahashimu bint Shee Mataka. Shairi hili lenye beti 102 na urari wa vina na mizani nane kila mshororo, lilikuwa wosia wake Mwana Kupona kwa bintiye na pia wanadada wengine wa enzi hizo za jadi. Ni shairi ambalo limekuwa muhimu sana katika ushairi wa Kiswahili kwani mtindo wake uliigwa na washairi wengine kama Said Karama(Wosia wa baba) na Shabaan Robert( Hati na Adili).

Shairi hili pia limewapa fursa wasomi wa Kiswahili lugha kupambanua baadhi ya vipengee muhimu vya Lahaja za Kiswahili. Lahaja ya Kiamu imetumiwa sana katika shairi hili ambalo lilipooandikwa, hati yenyewe ilikuwa ya Kiarabu. Hata hivyo kutokana na utafiti faafu ya Werner na Hitchens(1934), shairi hili lilipata hati ya Kiroma ambayo ni rahisi kusoma kwa wasomi wa kisasa.

Shairi hili pia limewapa fursa wanahistoria kuchanganua masuala kadhaa ya historia ya mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki katika enzi za Kisultani. Masuala ya kijamii kama vile dini, utabaka na mahusiano ya wanaume na wanawake katika jamii yameangaziwa vyema Kabisa. Fasihi ni kioo cha jamii, kwa hivyo kupitia shairi hili, tutaona jinsi jamii ya karne ya kumi na tisa ilivyoishi.

Senkoro (2011) anapambanua baadhi ya fani zionekanazo katika shairi hili.

Beti ya 1- 25. Shairi hili linamuasa Mwanahashamu awe mwadilifu kwake Mungu, awe mwaminifu kwake, asiwe mmbeya wala asijidunishe kwa macho ya jamii. Maudhui ya dini(Kiislamu) yanajitokeza vyema hapa. Pia tunapata taswira ya kuwa mtunzi alikuwa wa tabaka la juu na kuwa kulikuwa na ubaguzi wa kitabaka enzi hizo. Beti la ishirini kwa mfano:

Sitangamane na watumwa,
Ila mwida wa khuduma,
Watakuvutia tama,
Labuda nimekwambiya…


Tunaelewa kupitia ubeti huu kwamba watu wa tabaka la juu hawakufaa kutangamana na watumwa ila tu kwa kuwapa masharti ya hapa na pale. Swala la dini lajitokeza katika ubeti wa tano na sita:

Ukisa kulitangaza,
Ina la mola muweza,
Basi tuombe majaza,
Mngu tatufikiya,

Mwana Adamu si kitu,
Na ulimwengu si wetu,
Walau hakuna mtu
Ambao atasaliya…


Beti 26-36 Zinaangazia kwa urefu nafasi ya mke katika ndoa. Hapa ndipo utata hujitokeza. Ya kuwa mke hafai kujibizana na mumewe “…akinena, simjibu
Itabidi kunyamaa.
..” (Ubeti 28)
Mke anapaswa kumpa mumewe chochote
“…Atakalo simukbini” (Ubeti 29)
Mke anapaswa kumwaga na kumpokea mumewe kwa njia stahili. Usiku mke anapaswa kumpapasa mumewe, kumpepea hewa, kumkanda mwili na kumsinga. Beti za 35 na 36 zinasema:

Mtunde kama kijana,
Asiojua kunena,
Kitu changalie sana,
Kitokacho na kungiya…

Mpumbaze apumbae,
Amriye sikatae,
Maovu kieta yeye,
Mngu atakuteteya


Ni jambo ambalo limewaghasi wengi sana kumwachia mungu maovu ambayo huenda mwanamke katika jamii ile angetendewa na mumewe. Shairi hili linaendelea kuwa mwanamke alipaswa kumsifia mumeye kwa watu wengine, ampendezeshe na amnadhifishe mumeye. Mwanamke anaonywa kuwa iwepo atamghasi mumeye, atahukumiwa na mungu hadi jehanamu na ataikosa nafasi ya kuishi peponi.

Beti 37-56 zinamlenga mwanamke kujinadhifisha kwa ajili ya mumeye. Usafi, kuvaa vizuri, kujipamba, kuomba ruhusa kwake mume anapotaka kutoka, kutozungumza na watu njiani , aridhike na anachopewa na mumeye na asifunue buibui lake ovyo.

Mwanamke anaonywa kuwa iwepo atamghasi mumeye, atahukumiwa na mungu hadi jehanamu na ataikosa nafasi ya kuishi peponi.


Ubeti wa 44 unasema:

Ukutiwapo kutoka,
Sharuti ruhusa taka,
Uonapo meudhika,
Rudi na kuiketiya…


Ubeti wa 36 na 41.

Nawe ipambe libasi,
Ukae kama ‘arusi,
Maguu tia kugesi,
Na mikononi makowa…

Pete sitoe zandani,
Hina sikome nyaani,
Wanda siwate matoni,
Na nshini kuitiya…


Beti 56-66 zinaangazia kwa urefu jinsi mwanamke alivyofaa kuishi na wengine katika jamii. Alifaa kushirikiana na wengine na kuwapenda bila kuangazia hadhi zao(ambayo ni kinaya kwani alitaja kuwa watawala hawakufaa kutangamana na watumwa).

Beti 67- 102 ni dua yake Mwana Kupona kwa bintiye na Waislamu wote kwa ujumla. Dua lenyewe linawalenga wanawake wapate kulinata shairi hili na wosia uliotolewa.

Wosia huu hata hivyo una utata katika jamii ya kisasa. Baadhi ya mawaidha yaliyotolewa hayawezi kumwingia akilini mwanamke wa kisasa. Mengiyo yatafutiliwa mbali kama utumwa. Mijadala imezuliwa kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii ya enzi hizo na jinsi dini ilivyopata nafasi murua katika ndoa za jadi. Je, mwanamke wa janibu hizo alikuwa amesenea sana na kutumikwa kama chenzo cha kuwapumbaza wanaume? Alikuwa hana uhuru ama vipi?

Hizo tu ni baadhi ya mijadala inayozuka katika shairi hili. Hivyo kulifanya shairi ambalo lina manufaa mengi kwa usomi wa fasihi, historia na isimu za lugha iliyotumiwa.
 
Back
Top Bottom