Utajiri wenye uchungu

Dah mkuu barikiwa sana stor nzuri muendelezo tafadhar.
 
NYEMO CHILONGANI
UTAJIRI WENYE UCHUNGU
0718069269

Sehemu ya Ishirini na Tatu.

Siku iliyofuata, asubuhi na mapema Mike akachukua simu yake na kuanza kumpigia msichana Aisha, alitaka kuzungumza naye na kujua wakati huo alikuwa mahali gani.

Ndiyo kwanza msichana huyo alikuwa nyumbani kwake, hakuwa ametoka, alikuwa akijiandaa kwa ajili ya kupanda ndege na kwenda huko Dubai kuonana na mwanaume huyo aliyekuwa na uchu naye.

Mike akawa kwenye presha kubwa, japokuwa alikuwa chumbani hotelini lakini mara kwa mara alikuwa akikiangalia chumba hicho na kuangalia sehemu ambayo haikuwa imepangwa vizuri na kuipanga. Alikuwa na hamu ya kukutana na msichana huyo ambaye kwake alionekana kuwa mwanamke wa ndoto.

Ilipofika saa tano asubuhi, Aisha akampigia simu na kumwambia kwamba tayari alikuwa uwanja wa ndege hivyo amfuate kitu ambacho Mike alifanya haraka sana kwa kutumia magari maalumu ya kukodi yaliyokuwa hotelini hapo.

Alipofika, huku kofia ikiwa kichwani mwake, akateremka na kuanza kuelekea sehemu ya mapokezi, japokuwa alikuwa mtu maarufu kidogo kutokana na utajiri aliokuwa nao lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyemgundua, hata Aisha alipotoka, naye alijificha kwa kuvaa baibui, hijabu na nikabu.

Msichana huyo alimuona Mike japokuwa mwanaume huyo hakuwa amemgundua Aisha. Msichana huyo akamsogelea Mike na kusimama mbele yake, kitendo cha Mike kuyaona macho ya Aisha tu, akajua ndiye mwenyewe, hakuzungumza kitu, akampokea, akarudi garini na kuanza kuelekea hotelini.

“Nimekukumbuka sana mpenzi,” Mike alimwambia Aisha huku akiachia tabasamu pana na macho yake mara mojamoja yakiangalia mbele.

“Umekumbuka nini kutoka kwangu?” aliuliza Aisha huku naye akirudisha tabasamu pana.

“Kila kitu! Hayo macho yako, huwa yananiacha hoi sana,” alisema Mike huku akimwangalia vizuri msichana huyo.

Kadiri alivyomwangalia, moyo wake ulizidi kumpenda msichana huyo, alikuwa mzuri wa sura, kila alipoongea, sauti yake ilikuwa ikimtetemesha moyoni mwake. Humo ndani ya gari, Aisha akapata muda wa kubadilisha mavazi, akavua baibui lake na kupigilia suruali ya jinsi, ila kichwani hakuacha hijabu na miwani mikubwa ya kike.

Walichukua dakika kadhaa, wakafika katika hoteli hiyo ambapo wakateremka na kuingia ndani. Hakukuwa na watu waliowagundua, walikwenda kwenye lifti ambayo iliwapeleka mpaka katika floo ambayo Mike ndiyo aliyochukulia chumba.

“Karibu sana,” alisema Mike mara baada ya kuingia ndani.

“Asante sana, hivi ni kwa ajili yangu?”

“Ndiyo! Nimeandaa kwa ajili yako tu mrembo,” alisema Mike.

Mbele yao kulikuwa na meza iliyokuwa na vyakula kadhaa huku maua yakiwa pembeni. Aisha akabaki akiiangalia meza ile, moyo wake ulishtuka, hakuamini kuona kile alichokiona. Akakisogelea na kuangalia vizuri, moyo wake ukampenda Mike zaidi na zaidi.

Wakaelekea mezani na kuanza kunywa juisi, muda wote huo walikuwa wakiangaliana kimahaba tu. Kila mmoja alivutiwa na mwenzake, walipendana kiasi kwamba mbele yao hakukuwa na kitu kilichokuwa kikionekana zaidi ya ndoa tu.

Walinyweshana na kuonyeshana mapenzi ya njiwa. Baada ya kumaliza kunywa juisi, hakukuwa na kingine kilichoendelea zaidi ya kupanda kitandani na kuanza kushikana hapa na pale.

Aisha alikuwa akitetemeka kwa woga, hakuwahi kuwa kitandani na mwanaume, ni kweli alikuwa na miaka ishirini na nne lakini bado hakuwahi kumpa nafasi mwanaume yeyote yule kutokana na sheria kali iliyokuwepo nchini mwao.

“Mbona unatetemeka hivyo?” aliuliza Mike huku akiachia tabasamu pana.

“Sijawahi!”

“Kweli?”
“Ndiyo!”

“Hata siku moja?”

“Ndiyo! Sijawahi kabisaaa....” alijibu Aisha.

Mike akaachia tabasamu pana, hakuamini kusikia kwamba Aisha alikuwa msichana mbichi kabisa. Hakutaka kuchelewa, alijua namna ya kuwatuliza wanawake wa namna hiyo kitandani. Akafanya maandalizi yote, alipofanikiwa, mchezo ukaanza.

Muda wote Aisha alikuwa mtu wa kulalamika tu, alilia kwa kuwa alisikia maumivu makali chini ya kitovu. Muda mwingi alikuwa akimsukuma Mike atoke juu yake lakini mwanaume huyo alionekana kuwa mbishi, hakutaka kutoka wala kusogea popote pale.

Mchezo huo ulichukua dakika arobaini na tano, kila mmoja alikuwa hoi. Aisha hakuamini kama mwisho wa siku alilala na mwanaume kitandani. Kwake ilikuwa ni kama kuivunja ahadi aliyowaambia wazazi wake kwamba kamwe mwanaume wa kwanza kulala naye angekuwa mume wake, tena kipindi ambacho wapo ndoani kabisa.

“Mike, nimefanya nini tena?” aliuliza Aisha huku akianza kububujikwa na machozi.

“Kufanya nini tena?”
“Sikutaka kufanya hivi! Sikutaka Mike...” alisema Aisha huku akivuta shuka na kuanza kulia.

“Najua...najua Aisha, acha kulia mpenzi...”

“Mike, ninajuta, kwa nini nimefanya hivi? Nitauficha wapi uso wangu mimi?” aliuliza Aisha huku akilia kitandani pale. Kila alipomwangalia Mike, moyo wake ulimuuma mno.

“Kwani kuna tatizo gani?”

“Mike! Sikutaka kufanya hili kabla ya ndoa, niliuandaa usichana wangu kwa ajili ya mume wangu tu, kwa nini nimefanya na wewe kabla ya ndoa?” aliuliza msichana huyo, kulia hakuacha, muda wote machozi yalikuwa yakimtoka tu.

“Aisha...usilie mpenzi, nakuahidi kwamba nitakuoa!”

“Unanidanganya Mike!”

“Niamini! Ninakupenda sana, sitokuacha, nitakuoa, utakuwa mke wangu,” alisema Mike kisha kumkumbatia msichana huyo ambaye machozi yake yakatiririka mashavuni na kumwagika mgongoni mwa Mike.

Aisha hakukaa sana Dubai, siku iliyofuata tu, akaondoka na kurudi Kuwait. Moyo wake ulikuwa na maumivu kutolewa usichana wake na mwanaume huyo lakini wakati mwingine alikuwa akijifariji kwa kuhisi kwamba mwanaume huyo ndiye angekuja na kuwa mume wake wa ndoa.

Hawakuacha kuwasiliana, muda mwingi walikuwa wakiongea kwenye simu, walipendana, bado Mike aliendelea kumwambia Aisha kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumuoa na kuwa mke wake wa ndoa.

“Na vipi kuhusu dini?” aliuliza Aisha.

“Sijajua, ila nitakuoa tu.”
“Kweli?”
“Niamini!”

Siku zikaendelea kukatika, baada ya wiki mbili kupita, Aisha akaanza kujisikia tofauti mwilini mwake, akaanza kutapika hali iliyomfanya kukosa raha kabisa. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mwilini mwake, alichokifanya ni kumpigia simu Mike ambaye alikuwa nchini Marekani na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea.

Mike alivyoambiwa hivyo tu, akajua kwamba msichana huyo alikuwa mjauzito. Hakutaka kumficha, alimwambia aende akapime mimba kitu ambacho Aisha alipingana nacho.

“Haiwezi kuwa mimba!”

“Usiseme hivyo Aisha...nenda...”

“Sawa!”

Japokuwa hakuwa akiamini lakini akafanya hivyo ili kumfurahisha mpenzi wake tu. Akaenda mpaka katika Hospitali ya Al Tawfiq iliyokuwa katikati ya Jiji la Al Asimah kwa ajili ya kupima mimba.

Alipofika huko, moja kwa moja akaenda kwa daktari ambaye alimpima kipimo alichokitaka, kitu ambacho hakuamini hata mara moja ni pale alipopewa majibu kwamba alikuwa na mimba ya wiki mbili.

“Unasemaje?” aliuliza huku akionekana kutokuamini.

“Una mimba ya wiki mbili!” alijibu daktari. Aisha akachanganyikiwa kwani kupata mimba kabla ya ndoa, adhabu yake ilikuwa ni kupigwa mawe hadharani mpaka kufa pasipo kujali kama alikuwa binti wa mfalme au la.

****

Aisha alichanganyikiwa, hakuamini kile alichoambiwa, alimwangalia daktari yule mara mbilimbili na kumuuliza kama vipimo vyake vilionyesha sahihi, daktari huyo akamwambia kwamba vilikuwa sahihi na hata aliporudia, vilionyesha vilevile kwamba alikuwa mjauzito.

Akakosa furaha, akabaki akilia, hakuamini kile kilichotokea, aliifahamu nchi yao, sheria kali za dini hazikukutaka ufanye ujinga wowote ule, usipate mimba vinginevyo adhabu yako ingekuwa kupigwa mawe hadharani mpaka kufa.

Aisha hakutaka kubaki hospitalini hapo, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea nyumbani kwao. Kichwa chake kilichanganyikiwa mno, hakuamini kilichokuwa kimetokea. Alipofika nyumbani kwake, kitu cha kwanza kabisa kiliikuwa ni kujifungia chumbani na kuanza kulia.

Moyo wake ukamuuma, akajiona akiwa amefanya kosa kubwa sana maisha mwake. Hakutaka kabisa kubeba mimba akiwa na umri huo, kitendo cha kushika mimba tayari kilimaanisha kwamba kilichofuata mbele ni kifo tu.

“Mpenzi...” aliita Aisha huku akilia kwenye simu.

“Niambie mpenzi...”

“Nina mimba...”

“Kweli?”
“Ndiyo!”

“Hureee...” alisikika Mike akishangilia.

Kwa Aisha, hakukuwa na muda wa kushangilia zaidi ya kuwa na maumivu makali moyoni mwake. Mike alitakiwa kuwa na furaha hivyo kwani inawezekana alitafuta sana mtoto au alitamani kuzaa na mwanamke mrembo kama alivyokuwa.

Kwa msichana Aisha, furaha ya Mike ilikuwa ni sawa na kuukandamiza msumali wa moto moyoni mwake kwani alizidi kuumia mno. Siku hiyo hakutoka ndani ya chumba chake, alibaki humohumo, akizungumza na Mike na kumwambia hatari iliyokuwa mbele yake.

“Kwa hiyo wakijua watakuua?” aliuliza Mike.

“Ndiyo! Wataniua mpenzi...”

“Hapana! Hawawezi kumuua mwanamke mwenye mtoto wangu...” alisema Mike huku akionekana kushtuka.

Wakati wakizungumza kwa simu, tayari ilikuwa ni saa saba mchana hapo Kuwait. Hata kabla simu haijakata, mara Aisha akasikia mlango ukigongwa, akasimama na kuufuata, alipoufungua tu, polisi wawili walisimama mbele yake huku wakiwa na daktari.

“Upo chini ya ulinzi...” alisema polisi mmoja.

“Nimefanya nini?”
“Umeisaliti dini yetu...”

“Kivipi?”
“Umepata mimba! Uongo?” aliuliza polisi huyo huku mwenzake na daktari wakimwangalia Aisha.

Lengo la kufika na daktari huyo ilikuwa ni kumchukua vipimo Aisha pale ambapo angekataa kwamba hakuwa na mimba. Aisha alinyog’onyea mwili, hakuamini kabisa kile alichokisikia kutoka kwa madaktari hao, swali kubwa ambalo lilimjia kichwani mwake, watu hao walijuaje kama alikuwa na mimba?

Polisi hawakutaka kuchelewa, walichokifanya ni kumfunga pingu na kuondoka naye. Njiani, Aisha alikuwa akilia sana, hakuuamini kama mwisho wa maisha yake ungekuwa namna hiyo. Akaingizwa kwenye gari na safari ya kuelekea katika Kituo cha Polisi kuanza mara moja.

***

Mara baada ya Aisha kuondoka katika Hospitali ya Al Tawfiq, moja kwa moja daktari aliyempima, Dk. Fawdhil akawasiliana na Wazee wa Baraza la Sheria la nchini Kuwait na kuwaambia kile kilichotokea.

Japokuwa kilitakiwa kuwa siri baina yake na mgonjwa hasa katika mambo yanayohusu vipimo lakini daktari huyo hakutaka kunyamaza, akachukua simu yake na kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea.

Wazee hao wa Baraza la Sheria hawakutaka kuchukulia jambo hilo harakaharaka, walitakiwa kuwa na ushahidi mkubwa hivyo kuwaagiza watu waende katika hospitali hiyo na kuonana na daktari huyo.

Alichokifanya ni kuwapa kuwapa majibu ya vipimo vile ambavyo wakavichukua na kuviangalia, hawakuamini baada ya kugundua kwamba msichana aliyepata mimba alikuwa binti wa mfalme wa nchi hiyo.

“منأيوقتمضىالحملهي,” (msichana aliyepata mimba ni binti wa mfalme) alisema mmoja wa vijana waliotumwa waende huko.

“ماذاتقول؟,” (Unasemaje?)

“كانالأمركذلك،هوعائشة,” (Ndiyo hivyo! Ni Aisha) alijibu kijana huyo.

Kila mmoja alishangaa, hawakuamini kama msichana huyo angeweza kufanya kitu kama hicho na wakti alijua dhahiri jinsi sheria za nchi za Uarabuni zilivyosema. Hawakutaka kubaki hospitalini hapo, walichokifanya ni kuondoka na kurudi kwa Wazee wa Baraza la Sheria ambapo wakawaambia kila kitu kilichotokea.

“Yaani unamaanisha huyuhuyu Aisha binti mfalme?” aliuliza mzee mmoja.

“Ndiyo!”
“Hapana! Siwezi kuamini!”

“Ndiyo hivyo mkuu! Ni Aisha huyohuyo!”

Walichokifanya ni kuwasiliana na waziri mkuu na kumwambia kile kilichotokea, kila mmoja aliyepata taarifa hiyo alishangaa, iweje binti wa mfalme apate mimba na wakati alizijua sheria zote kwamba msichana yeyote hakutakiwa kuzini mpaka pale atakapoolewa.
Waziri Mkuu akafanya mipango ya kuwasiliana na Mfalme Sabah Al Ahmad ambaye ndiye alikuwa baba yake Aisha. Mfalme alivyoambiwa kuhusu binti yake, hakuamini hata kidogo, alimfahamu msichana huyo, alikuwa radhi kuulinda usichana wake kwa nguvu zote lakini si kufanya uzinzi hata kabla ya kuolewa.

“Binti yangu hawezi kufanya hivi,” alisema mfalme huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Amefanya, na vipimo hivi hapa,” alisema mzee mmoja huku akimpa karatasi iliyokuwa na majibu ya vipimo alivyochukua.

Kilichofuata baada ya kuyaangalia majibu yale ni machozi kuanza kumbubujika mashavuni mwake. Mbele yake alihisi aibu kubwa ikimkumba, aliwaona watu wote wakimsogelea na kisha kuanza kumzomea.

Kama alizishika sheria zote tena huku akiwaambia watu wengine wazishike, ilikuwaje akashindwa kumwambia binti yake? Alichanganyikiwa lakini hakuwa na jinsi, kama zilivyokuwa sheria nyingine kwamba ni msumeno, basi naye Aisha alitakiwa kukamatwa na kuhukumiwa kifo cha kupigwa risasi au mawe hadharani.

Yeye ndiye alikuwa mfalme, kwenye muda wa kuweka saini katika karatasi ya kuruhusu msichana huyo akamatwe, akaingia kwanza chumbani kwake, yeye na mkewe wakalia sana, alipotoka, hakuwa na jinsi, akasaini karatasi hiyo, Aisha alitakiwa kukamatwa, kusomewa kesi yake kisha kuhukumiwa.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne.
 
UTAJIRI WENYE UCHUNGU
0718069269

Sehemu ya Ishirini na Nne.

Watu wengi walishangaa, hawakuamini kile walichokisikia kwamba binti wa mfalme, Aisha alikuwa amefanya mapenzi na mwanaume na kupata ujauzito. Taarifa ile ilisambaa kwa kasi kama moto wa kifuu na hata magazeti ambayo yalitoka siku hiyo yalikuwa na habari hiyo huku picha ya msichana Aisha akiwa na pingu ikionekana vizuri kabisa.

Macho yake yalikuwa mekundu, alikuwa akilia kila wakati, kila alipohojiwa, hakusita kumuomba msamaha kila mmoja kwamba kile kilichotokea hakikuwa lengo lake, alifanya hivyo kwa kuwa alimpenda mwanaume huyo ambaye hakutaka kumtaja.

Selo alipolala, kila wakati alikuwa na huzuni tele, hakujua ni kwa namna gani angeweza kukiepuka kifo kilichokuwa mbele yake. Wakati mwingine alijiona kuwa mkosefu mkubwa kwa kulikosea taifa hilo, ila pamoja na yote hayo, hakumlaumu Mike, alikuwa mwanaume aliyempenda sana katika maisha yake.

Huko hakupata nafasi ya kuwasiliana na Mike, hakukuwa na simu, alikuwa kwenye ulinzi mzito ambao hata kumuona tu ilikuwa kazi kubwa. Mfalme Sabah alikuwa kwenye huzuni kubwa, kilichotokea, hakuamini, alijidharau kwa kuona kushindwa kumlinda mtoto wake asipate mimba.

Uhuru aliokuwa amempa, leo hii ndiyo ulimfanya kuwa katika hali hiyo, alijifungia chumbani na mkewe na kuendelea kulia. Ile ilikuwa sheria, hakuweza hata kuipindisha kwani kulikuwa na watu wengi huko nyuma ambao nao walipigwa mawe na risasi hadharani kwa kubambwa wakizini au hata kupata mimba.

Shirika la Haki za Binadamu Duniani (Human Rights) likaingilia kati, kile kilichotaka kutokea nchini Kuwait, hawakukubaliana nacho hata kidogo, ilikuwa ni lazima wawasiliane na serikali ya nchi hiyo na kuzungumza nayo ili isifanye kile kilichotakiwa kufanya, cha ajabu, serikali ikakataa katakata.

“Haiwezekani, hii ni nchi inayoendeshwa kwa misingi ya kidini, kitu hicho hatuwezi kukifumbia macho, ni lazima hukumu itolewe,” alisema msemaji wa serikali ya Kuwait.

“Lakini ni kinyume na haki za binadamu...”

“Hiyo ni huko kwenu, ila huku kwetu, kila kitu kipo kwenye misingi ya dini,” alijibu, hakuiacha simu hewani, akaikata.

Huko alipokuwa, Aisha hakutakiwa kuonana na ndugu zake, alitakiwa kukaa hukohuko, kama kuwaona angewaona siku ambayo angepelekwa mahakamani tu, tena kuwaona na si kuzungumza nao.
Siku zikaendelea kukatika, mwili wake ukakonda, ukakosa nguvu, kila siku ilikuwa ni huzuni kwake, hakuamini kama kuna siku angeweza kupata furaha maishani mwake.

Baada ya siku kadhaa, akatakiwa kufikishwa mahakamani, huko hakukuwa na muda wa kusikiliza kesi, kilichotakiwa ni kutolewa kwa hukumu juu ya kile alichokuwa amekifanya.

“ويتمالحكمعلىأنهاعلنارجمحتىالموت ,” (Unahukumiwa kupigwa mawe hadharani mpaka kufa) alisema hakimu, hakukuwa na kilichoendelea zaidi ya kufunga keso hiyo kwa kuwaambia watu kuwa hukumu hiyo ingefanyika wiki moja baadaye, mbele ya macho ya watu wote ili iwe fundisho.

Mahakamani hapo, ndugu zake wote walikuwepo, hukumu ilipotolewa, sauti za kilio zilisikika kutoka kwa ndugu zake, mfalme, mama yake na watu wengine. Hakuruhusiwa kuzungumza nao, akachukuliwa na kurudishwa tena sero ambapo huko akabaki peke yake akisubiri siku ya hukumu.

Dunia haikunyamaza, kila siku wanaharakati wa haki za binadamu wakahangaika ili kumnasua Aisha kwenye hukumu hiyo lakini halikuwezekana, walichanganyikiwa, hawakutaka kumuona msichana huyo mrembo aliyekuwa na mimba akihukumiwa adhabu kubwa kama hiyo.
Walijitahidi kwa kushirikiana na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi lakini juhudi zao zote hizo ziligonga mwamba, hawakuchoka, waliendelea kufanya jitihada nyingine lakini bado Waarabu walimng’ang’ania Aisha, hivyo wakaachana naye.

Humo sero, siku zilikatika kwa haraka sana, Aisha alilia mno, hakuamini kama kweli alibakisha siku chache kabla ya kifo chake. Zilipobaki siku mbili kabla ya tukio, mahakama ikalegeza msimamo kwa kuwaruhusu ndugu zake kuzungumza naye akiwa humo sero.

“Ninakufa mama...” alisema Aisha huku akilia.

“Mwanangu, mwa nini umefanya hivi?” aliuliza mama yake, naye alikuwa akilia tu.

“Mama! Nilimpenda mpenzi wangu! Najua nimekosa lakini sikuwa na jinsi, sikuwa na jinsi mama, naombeni mnisamehe,” alisema Aisha huku akilia mno.

“Aisha binti yangu! Kama ningekuwa na uwezo, ningepindisha sheria ili uachiwe huru, nimejaribu sana lakini nimeshindwa,” alisema baba yake, mfalme Sabah.

Walizungumza mengi lakini katika yote hayo, Aisha hakutaka kumtaja mtu aliyempa mimba. Hilo lilibaki kuwa swali kubwa lililomuumiza kila mtu, walitaka wamfahamu mwanaume huyo ili kama ikiwezekana naye apokee adhabu lakini Aisha hakutaka kulitaja jina lake.
Siku hizo mbili zilipokatika, mlango wa sero ukafunguliwa na mwanaume mmoja kuingia ndani. Akamchukua Aisha, akamfunga kitambaa usoni na kuanza kutoka naye ndani ya chumba cha sero hiyo.

Walipofika nje, wakaingia ndani ya gari lililokuwa na polisi wengi kisha kuanza safari ya kuelekea katika uwanja maalumu wa kuhukumia watu, uwanja ambayo ulionekana kuwa kama laana, hata jina lake uliitwa kwa Kiarabu, Laenatan (لعنة) yaani, Laana.

Watu walikuwa wengi njiani, wengi walitaka kuona binti huyo mrembo, Aisha, binti mfalme akichukuliwa na kwenda kupigwa mawe. Kila mahali gari hilo lilipopita, watu walimzomea Aisha, alimtia aibu baba yake, hakutakiwa kuishi tena, kitu ambacho kila mtu alitamani kukiona ni binti huyo akipigwa mawe hadharani na kufa.

Mpaka gari linafika katika uwanja huo, Aisha alikuwa amelia vya kutosha, hakukuwa na msaada wowote ule alioupata, hakuona kitu kutokana na kitambaa alichokuwa amefungwa, akateremshwa kutoka garini, akapelekwa katika sehemu uliokuwa na shimo, alitakiwa kuingizwa humo, kufukiwa na kichwa tu ndicho kibaki na hicho ndicho ambacho watu walitakiwa kukipiga mawe mpaka kufa.

Akaingizwa kwenye shimo lile, likafukiwa. Toroli lililokuwa limebeba mawe makubwa likaletwa mahali hapo, mawe yale yakateremshwa. Katika uwanja huo kulikuwa na watu zaidi ya mia tano, wale waliotaka kumpiga Aisha wakayafuata mawe tayari kwa kuanzia kutoa hukumu hiyo.

Aisha ambaye ni kichwa chake tu ndicho kilichokuwa kimebaki juu, alikuwa akilia tu, hakuamini kama huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Alitamani kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo kuwa ndoto, ila hicho hakikuwezekana, kilichokuwa kikitokea, kilitokea kwenye maisha halisi.

“Moja, mbili...ta...” alisema mwanaume aliyekuwa akihesabu, watu wengine wakayaandaa mawe yao.
Wakati mwanaume huyo akimalizia kuhesabu, ghafla mabomu ya gesi yakaanza kupigwa mahali hapo. Hakukuwa na mtu aliyejua nini kilitokea, mabomu kadhaa yalipigwa mfululizo, watu wakaanza kukimbia, hakukuwa na aliyemuona mwenzake, kila kona, kulikuwa na moshi mkubwa na kuwafanya watu kukohoakohoa tu.

Aisha mwenyewe hakujua ni kitu gani kilichokuwa kimeendelea, alisali sala yake ya mwisho na kitu pekee ambacho alisubiri mahali hapo ni kufa tu. Mabomu ya gesi yaliyokuwa yamepigwa yalimshtua na hakujua kitu gani kilikuwa kimetokea.

Watu walikohoa, wengine walijigonga na wenzao, uwanja huo ulibadilika, na si hapo tu hata nje ya uwanja kote huko kulipigwa mabomu hayo. Wakati Aisha akijiuliza ni kitu gani kilikuwa kimetokea, ghafla mbele yake akatokea mwanaume mmoja, alikuwa akitembea huku mkoni mwake akiwa na bunduki kubwa, alipomfikia, akaanza kufukua kwa kasi ya ajabu.

“We have to go,” (Tunapaswa kuondoka) alisema mwanaume huyo huku akiendelea kumfukua.

“Please don’t kill me,” (Usiniue tafadhali) alisema Aisha.

“I am not here to kill you, but to save you,” (Sipo hapa kukuua bali kukuokoa) alisema mwanaume huyo huku akiendelea kumtoa Aisha katika shimo lile.

Bado mabomu ya gesi yaliendelea kusikika kila kona hali iliyoonyesha kwamba mwanaume huyo hakuwa peke yake mahali hapo, alikuwa na wenzake ambao walikuwa wakiendelea kuyapiga mabomu hayo mahali hapo kuwatawanyisha watu zaidi.

Kwa sababu Aisha alikuwa amekaa kwenye gesi hiyo kwa kipindi kirefu, mwanaume yule akachukua kinyago kile alichokivaa na kisha kumvisha msichana huyo na kumtoa katika shimo lile.

Kilichofuatia ni kuanza kuondoka mahali hapo kuelekea sehemu iliyokuwa na gari. Moshi wa gesi ulitapakaa kila kona, ilikuwa ni vigumu mno kuona hata hatua tatu mbele lakini mwanaume yule alikuwa makini na walifanikiwa kufika mpaka kwenye gari wakiwa salama kabisa.

Walipoingia tu, na wenzake wakaja na kuingia, kilichofuatia, gari likawashwa na kuondoka mahali hapo huku Aisha akiwa na maswali mengi kichwani mwake, watu hao walikuwa ni wakina nani? Kila alipojiuliza, alikosa jibu.

Watu waliokuwa wamesogea baada ya kuona moshi wa gesi umepungua, wakasogea kule uwanjani, wakaokota mawe tayari kwa kumshambulia Aisha kama walivyotaka kufanya.

Kitu kilichowashtua, Aisha hakuwepo. Shimo lilikuwa wazi, lilifukuliwa na msichana huyo hakuwemo humo. Kila mmoja alishangaa, wakaanza kujiuliza kama msichana huyo alilifukua shimo hilo yeye mwenyewe na kukimbia au kulikuwa na mtu mwingine aliyelifukua, kila walilojiuliza, wakakosa jibu, kitu pekee walichokisema ni kwamba msichana huyo aanze kutafutwa kila kona.

Je, nini kitaendelea
 
Ina maana sasa hivi jamaa jogoo anasimama? Haya mimba kwa aisha imeingiaje?
 
NYEMO CHILONGANI
UTAJIRI WENYE UCHUNGU
0718069269

Sehemu ya Ishirini na Tano.

Mike alishindwa kuamini kile alichokuwa akikiona kwenye televisheni kwamba mpenzi wake, msichana aliyekuwa akimpenda kuliko msichana yeyote katika dunia hii alitarajiwa kuhukumiwa kwa kupigwa mawe hadharani au kupigwa risasi.

Moyo wake ulimuuma mno, hakutaka kuona msichana huyo akiuawa, alimpenda na kubwa zaidi alikipenda kiumbe kilichokuwa tumboni, alichokitaka ni baada ya miezi tisa tu.

Alijiona kuwa na kitu cha kufanya, kumuacha msichana huyo auawe kilikuwa ni kitu kisichowezekana hata kidogo. Aliendelea kufuatilia kwa kuhisi kwamba kwa sababu baba wa msichana huyo alikuwa mfalme basi hilo lisingekuwa tatizo hata kidogo, baada ya hukumu kutolewa na baba kuridhia, hakuwa na jinsi, alitakiwa kufanya kila liwezekanalo kumuokoa msichana wake.

Alichokifanya ni kuandaa kiasi cha dola milioni moja kwa ajili ya watu ambao walikuwa na kazi kubwa ya kufanya. Akawatafuta vijana ambao walikuwa katika wakichukua mafunzo na kuwa CIA. Ilikuwa ngumu sana kuwapata lakini kutokana na kuwa na ukaribu na watu hao, hasa viongozi, akawapata na hivyo kuwapa kazi hiyo.

Walikuwa vijana wanne, mbele yao kulikuwa na kazi kubwa lakini hawakuwa na jinsi, kwa sababu kiasi kikubwa cha fedha kiliwekwa mezani, ilikuwa ni lazima wafanikishe kile walichoambiwa.

Baada ya siku mbili, wakaanza safari ya kuelekea nchini Kuwait, njiani, walitumia vitambulisho vilivyowaonyesha kwamba walikuwa katika safari ya kuelekea katika kituo cha kijeshi cha Marekani nchini humo, hivyo hawakupata tabu.
“Tutapata kila kitu kambini, msijali,” alisema Kurt, mmoja wa vijana hao.

Walipofika nchini humo, walichokifanya ni kwenda katika kambi ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa nchini humo, walipofika, kwa kuwa walikuwa na vitambulisho na walijulikana kupitia Mike ambaye aliwapa taarifa mapema, wakapewa silaha ambazo wangezitumia katika safari yao ya kumuokoa msichana Aisha.

Siku zote hizo walilala hapohapo huku wakifuatilia ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Mahakamani, nao walikuwepo, kila sehemu ambayo walitakiwa kuwepo, walikuwepo.

Siku ambayo ndiyo hukumu ingetekelezwa, waliwahi asubuhi na mapema katika uwanja huo, kitu cha kwanza wakaweka vinasa sauti vilivyokuwa na nguvu mahali hapo, waliangalia huku na kule kama kuisoma ramani na kisha kurudi ndani ya gari.

Gari lao halikutoka katika eneo hilo. Ilikuwa ni vigumu kuwafahamu watu waliokuwa ndani ya gari hilo kwani lilikuwa na vioo vilivyowekwa tinted kila kona.

Watu wakaanza kukusanyika mahali hapo, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Kurt na wenzake walikuwa wakifuatilia kila kitu. Silaha zao zilikuwa mikononi mwao. Mpaka Aisha analetwa mahali hapo, tayari walikuwa wamekwishajipanga na kusikiliza kila kitu kilichokuwa kikiendelea kupitia vinasa sauti walivyokuwa wameviweka.

“Vipi! Tuanze sasa hivi?” aliuliza kijana mmoja.

“Subiri kwanza...”
“Ila watamuua, si unasikia ndiyo wanakwenda hatua nyingine!”
“Wala msijali! Hatuwezi kuchelewa hata kidogo!” alisema Kurt huku akiwa na uhakika kwamba wasingeweza kuchelewa.

Baada ya mtu mmoja kuhesabu moja mpaka mbili, ndipo Kurt aliposhusha kioo na kupiga mabomu matatu ya gesi, watu walipoona moshi mkubwa ukitanda, wakashindwa kufanya walichotaka kufanya, hapohapo wakaanza kukimbia kwani tayari sehemu hiyo ilionekana kuwa si salama tena.

“Nyie endeleeni kupiga, acha nikamchukue...” alisema Kurt huku akiufungua mlango wa gari na kutoka.

“Sawa! Wewe nenda, tutakulinda,” alisema kijana mwingine na Kurt kuteremka, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuelekea kule alipofukiwa Aisha.

Alipomfikia, akamfukua, akamchukua na kumpeleka garini. Safari ikaanza mara moja.

****

Ilikuwa ni lazima waondoke nchini Kuwait kwa kutumia usafiri wowote ule lakini si kubaki mahali hapo. Ndani ya gari, bado msichana Aisha alikuwa akijiuliza juu ya watu waliokuwa humo, hakujua walikuwa wakina nani na kwa nini waliamua kumuokoa kutoka katika kifo.
Gari liliendeshwa kwa kasi, walichomwambia Aisha ni kwamba walikuwa wakitaka kuelekea nchini Iraq. Aisha ndiye alikuwa muelekezaji kwamba wapi walitakiwa kupita mpaka kufika nchini humo.

Njiani, hawakutaka kuendesha kwa kasi sana kwa kuogopa kugundulika, waliendelea mpaka walipofika sehemu ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya watu, hapo ilikuwa ni kwenye Soko Kuu la Jahra ambalo asilimia kubwa ya watu kutoka sehemu mbalimbali Kuwait walipendelea kufika hapo kwa ajili ya kufanya manunuzi yao.

“Nyie ni wakina nani?” aliuliza Aisha baada ya ukimya wa muda mrefu.

“Sisi?”
“Ndiyo!”

“Huwezi kutufahamu!”

“Kwa nini? Nataka niwafahamu na kwa nini mmeniokoa,” alisema Aisha.

“Kwa sababu tulitumwa.”
“Na nani?”

“Usijali! Utajua tu.”

Hawakutaka kuzungumza kitu kingine chochote kile, walichokitaka ni kufika kule walipoambiwa wafike na mambo mengine kuendelea. Tayari walikuwa wamekwishafika Khaitan, wakaambiwa wageuze, wasitumie tena mpaka wa kuingilia Iraq kwani tayari serikali ilishaagiza kufungwa kwa mipaka hiyo, hivyo walitakiwa kutumia boti.

“Amesemaje?”

“Tutumie boti. Hivi hapa tunaweza kupita wapi mpaka tufike baharini?’ aliuliza Kurt.

“Kama kilometa mia nane hivi, hapa ni Khaitan, kwa hiyo inatupasa turudi mpaka katika Jiji la Kuwait, huko, tutachukua njia ya kwenda Salmiya,” alijibu Aisha.

“Sawa.”
Walichokifanya ni kugeuza na kisha kuanza safari nyingine, njiani, kila mmoja alikuwa na wasiwasi, kilometa mia nane zilikuwa nyingi sana hivyo kila wakati walitulia njiani kisha kuendelea na safari.

Bado kichwa cha Aisha kilikuwa na maswali mengi, hakuwafahamu watu hao, walikuwa wageni na kitu kilichomuumiza kichwa chake ni kwamba hakujua mtu ambaye aliwatuma kuja kumuokoa.

Mawazo yake yalikuwa kwa baba yake tu, aliamini kwamba ndiye alitumia kiasi cha fedha kumuokoa kwani bado alikuwa akimpenda mno. Kuna kipindi alihisi kwamba inawezekana akawa Mike lakini kila alipokumbuka kwamba mtu huyo hakuonekana kujali sana hata kipindi alichomwambia kwamba atauawa, hakufikiria kama angeweza kufanya kitu kama hicho.

Safari iliendelea zaidi, walipobakiza kilometa kama mia tano kabla ya kuingia katika Jiji la Kuwait, wakaona magari mengi yakiwa yamesimama kando ya barabara na polisi wakilikagua kila gari lililopita mahali hapo.

Wakashtuka, hawakuwa wamefikiria kama kungekuwa na msako kiasi hicho, hawakutaka kujiuliza sana, walijua tu kwamba ni msichana Aisha ndiye aliyekuwa akitafutwa. Alichokifanya Kurt ni kuwasha redio.

“Wanasemaje?” aliuliza Kurt huku akimwangalia msichana Aisha.

“Mungu wangu!”

“Nini?”
“Mipaka yote imefungwa na ulinzi umeimarishwa, natafutwa kwa udi na uvumba huku kiasi kikubwa cha fedha kikiwa kimeandaliwa,” alijibu msichana Aisha.

Kwanza wakaangaliana, wakapata jibu juu ya foleni ile iliyokuwepo. Kuvuka mahali hapo pasipo kukaguliwa lilikuwa jambo gumu sana, hivyo wao kama majasusi walitakiwa kufanya kitu fulani.

“Tufanyeje?” aliuliza Shawn.

“Subiri, hebu nipeni dakika kadhaa,” alijibu Kurt, akaegemea usukani, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alijifikiria ni kwa jinsi gani wangeweza kuvuka mahali pale.

Sehemu ile ilionekana kuwa na msako mkubwa, polisi, wenye bunduki na mbwa walisimama kila kona. Walikuwa makini mno kwa kila gari lililokuwa likipita mahali hapo.

Watu wengine waliamriwa washuke garini na wao kupekua gari, wengine walipelekwa pembeni kabisa. Mtu aliyekuwa akihitajika mahali hapo alikuwa mmoja tu, msichana Aisha ambaye kwa kipindi naye alikuwa safarini kuelekea baharini, kupanda boti na kuelekea nchini Marekani.

****

Taarifa za uvamizi uliofanyika nchini Kuwait ukamfanya kila mtu kuashangaa, hawakuamini kama kweli kungetokea na tukio kama lile kwani hapo kabla, halikuwahi kutokea hata siku moja.

Nchi nyingi za Kiarabu zilikasirika, kwao, kuchukuliwa kwa msichana Aisha ilionekana kuwa aibu. Alifanya kosa kubwa, hakutakiwa kusamehewa hata mara moja na hata ule uvamizi uliofanyika wa kumuokoa, haukukubalika.

Ilichokifanya nchi ya Kuwait ni kuhakikisha mipaka ya nchi yote inafungwa, si ya kutoka nchini tu bali hata ya ndani kwa ndani, yaani mkoa kwa mkoa, jiji kwa jiji ilitakiwa kufungwa.

Picha nyingi za Aisha zikachapishwa na kubandikwa barabarani na kwenye vituo vya mabasi, alionekana kuwa mtu mbaya ambaye hakustahili msamaha wowote ule, iwe isiwe ilikuwa ni lazima apatikane na kurudishwa katika sehemu ya hukumu na mambo mengine kuendelea.

“Tunatoa saa ishirini na nne, awe amepatikana,” alisema waziri mkuu.

Hilo suala mfalme Sabah halikumuhusu hata mara moja, kila mtu nchini Kuwait alihisi kwamba yeye ndiye alikuwa nyuma ya kila kitu japokuwa watu waliomuokoa hawakuwa wameonekana. Wapo wengine waliosema ni Wazungu, wengine wakasema ni Waarabu wenzao lakini wengine walikwenda mbali na kusema kwamba msichana huyo aliokolewa na Waisrael.

“Tutajua tu ukweli!”

Suala la Aisha likawa gumzo. Shirika la kijasusi la nchini Kuwait likaamua kuchukua video ya kila kitu kilichotokea katika uwanja ule. Walifanikiwa kuliona bomu la gesi likidondoshwa katika uwanja huo ila hawakujua mahali lilipotoka.

Walituliza vichwa vyao lakini hawakufanikiwa kuona kitu chochote kile. Baada ya kuendelea kukaa na kuangalia, kwa mbali wakawaona watu wawili wakikimbia na kuelekea katika gari ambalo nalo hawakuliona vizuri kutokana na moshi kutapakaa kila kona.

Hawakuwa na shaka kwamba watu hao walikuwa ni Aisha na mtu aliyekuja kumchukua. Walichanganyikiwa, ingekuwa bora hata kuliona hilo gari, au mtu kujua alikuwa mtu kutoka nchi gani, kilichoagizwa ni kufungwa kwa mipaka yote huku kwa mtu ambaye angefanikisha kupatikana kwake, angezawadia kiasi kikubwa cha fedha.

“Ni lazima apatikane, cha msingi anzeni kufunga mipaka ya kila kona,” alisema mkuu wa polisi hapo Kuwait, kamanda Abdul Aziz.

“Hakuna tatizo mkuu!”

“Na hakikisheni hata hao watu waliomtorosha wanapatikana pia,” aliongezea.

“Hakuna tatizo mkuu!” walijibu polisi kisha kupiga saluti na kutoka ndani ya ofisi ya kamanda wao.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumapli hapahapa.

Umeipenda? Dondosha LIKE yako, sema chochote kuhusu simulizi hii!
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…