UTAJIRI WA DAMU - 4
LIPOISHIA
Wakati anaendelea kunihoji katika, redio yake ya upepo tulisikia Inspekta Ado akiambiwa kuwa kuna mwanaume mwingine amekutwa ananing'inia kwenye mti akiwa amenyongwa.
"Khaa, mwingine tena?" alisikika akisema yule askari aliyekuwa akinihoji na akawa anasikiliza kwa makini majibizano kati ya askari wa doria na Inspekta Ado.
Endelea...
Askari huyo wa kike alionekana kuchanganyikiwa na kuanza kuwapigia simu watu mbalimbali ambao nihisi walikuwa ni wapelelezi.
Baadaye aliniambia kuwa mahojiano yetu yametosha lakini akaniambia ni lazima nirudi rumande kwa kuwa yeye hakuwa na uamuzi wowote kuhusu kuniachia huru.
"Lakini kwa maelezo yangu afande unaona nina hatia?"
"Mimi siwezi kujua."
"Una uzoefu, tafadhali nieleze maana si ni nyinyi ndiyo mnatayarisha mashitaka?"
"Hapana, siku hizi anayetayarisha mashitaka ni ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka."
"Ina maana kuna siku atakuja hapa kunihoji?"
"Hapana, tunachokifanya siku hizi ni kwamba sisi polisi tunampelekea jalada hili ofisini kwake kisha yeye akishalipitia anaona kama kuna kosa anaandaa shitaka au mashitaka."
Wakati anaendelea kunifahamisha, ghafla aliingia Inspekta Ado huku akiwa na simu yake mkononi. Alikuwa akizungumza na mtu fulani ambaye upande huo wa pili wa simu yake nilikuwa sisikii maneno aliyokuwa akiyasema.
"Umesema ameuawa na ananing'inia kwenye mti?"
Baadaye alimuamuru yule askari aliyekuwa akinihoji anirudishe rumande.
"Chepriska hakuna namna rudi ndani tukashughulikie hili tukio jipya," alisema askari yule huku akiniongoza kwenda kunifungia mahabusu.
Kilichoendelea huko walikokwenda sikukijua kwani mimi nilikuwa ndani huku giza likiwa limetanga na mbu wakilia kutaka kunyonya damu yangu japokuwa usiku ulikuwa haujaingia.
***
"Cheprisca, nakuachia, unajidhamini mwenyewe kwa kuwa nimesoma maelezo kwenye jalada, nimeona hakuna kitakachonifanya niendelee kukushikilia lakini tukikuhitaji, tutakuita, sawa?" Alisema Inspekta Ado
"Sawa."
Niliachiwa na nikaenda moja kwa moja kwa Bwana Mitimingi. Huyu alikuwa tajiri aliyekuwa akinituma mara kwa mara kazi zake, zingine ni za kijinga kabisa, kama vile kumletea mavi ya tembo au takataka za kwenye kona.
Niliamini kwamba alikuwa akinituma vitu vile ili avifanyie mambo ya kishirikina na nilihakikisha hilo baada ya kumuona siku moja akiweka kipande cha mavi ya tembo niliyompelekea kwenye siti ya dereva ya moja ya mabasi yake.
Lakini siku nyingine alinituma nimpelekee yai la bundi ambalo nililinunua kwenye maduka ya dawa za asili kwa bei mbaya. Sikujua yai lile alilifanyia nini.
Kuna siku alinituma nimletee nyasi zilizo kwenye makutano ya barabara, baada ya kuzileta nilimuona akiziweka chini ya kiboksi cha fedha za mauzo.
Niliwahi kusikia kwenye ‘redio mbao' kuwa mzee huyu ni kigagula ambaye ana mbinu nyingi za kishirikina za kupata fedha, hivyo nilikuwa makini sana kwa kila alichokuwa akinituma.
Nilisikia watu wakisema utajiri wa mzee Mitimingi ulitokana na mambo ya giza na wengine walikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa alikuwa akiua watu na kuwageuza misukule.
Maneno hayo yalinifanya nisiwe na raha kwa sababu nami watu waliokuwa wakiniona niko naye karibu walikuwa wakinihusisha na imani za kishirikina na iliwahi kutokea mtu mmoja kuniambia laivu kuwa mimi ni mchawi.
Mawazo hayo niliyaweka kando nikawa nafikiria la kusema pindi nikionana na mzee Mitimingi kwani nilitaka anilipe fedha zangu kwa kuwa aliwahi kunipa kazi za kumtafutia nywele za watoto wachanga.
Ilikuwa ni dili, ilibidi niongee na kinyozi aliyefanikisha kunipa bunda la nywele hizo na akawa ananidai fedha nikawa ninamzungusha kwani mzee Mitimingi aliyekuwa bahili hakunilipa ujira wangu.
Kitendo cha kutomlipa fedha zake yule kinyozi kilimkera ndipo akaniambia:
"Usiponilipa fedha zangu nitakutangaza kwamba wewe ni mchawi."
"Hapana ndugu yangu usifanye hivyo, mimi zile nywele nilitumwa tu."
"Alikutuna nani kama na wewe siyo mchawi, nilipe fedha zangu Chapriska."
"Ndugu yangu usiwe na wasiwasi kuna mzee atanipa fedha zako na nitakuletea, naomba niamini."
"Nakuamini nakupa siku mbili uwe umenilipa, usinifanye mimi sijui fedha," alifoka kinyozi huyo.
Niliondoka kwenda kwa mzee Mitimingi nikiwa na wasiwasi mkubwa kwamba kwanza, siku alizonipa kinyozi zilibaki mbili maana moja niliipoteza nikiwa mahabusu.
Nilikuwa naomba Mungu mzee huyo nimkute na anipe fedha ili nimlipe kinyozi aliyegeuka kuwa mkorofi kwangu.
Nilipokaribia jumba la mzee Mitimingi nilisikia mbwa akilia.
Nilijiuliza kwa nini yule mbwa alikuwa analia kilio kilichoonesha alikuwa anapigwa.
Sikukosea kwani nilipokaribia geti niliona mzee Mitimingi akimpiga mbwa wake.
Kilichonishangaza zaidi ni kuona mzee huyo akisema na mbwa yule akimuambia anampiga kutokana na kutotii alichomuagiza.
"Nitakupiga sana kwa sababu umeniudhi." Alipotoa kauli hiyo alikuwa akimpiga mbwa huyo kwa fimbo. Nilijitahidi kuchungulia nikamuona mbwa kafungwa kamba kichwa kikiwa kibandani na sehemu ya mapaja yake yakiwa nje.
Nilipigwa na butwaa kwani ilikuwa mara yangu ya kwanza kushuhudia jambo kama lile!
Je, kwa nini anaongea na mbwa? Fuatilia ujue siri hiyo..........Baadae...........