#COVID19 Utafiti Uingereza: Chanjo inasaidia kupunguza kuenea kwa virusi vya corona kwa asilimia 85

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Takwimu kutoka nchini Uingereza zinaonesha kuwa chanjo dhidi ya virusi vya corona inasaidia kupunguza uwezekano wa kuenea kwa maambukizi kwa hadi asilimia 85.

Utafiti uliochapishwa na taasisi ya Public Health England (PHE) unaonesha kuwa chanjo ya Pfizer-BioNTech inapunguza uwezekano wa kupata maambukizi kwa zaidi ya asilimia 70 mara baada ya kupokea chanjo ya kwanza, na uwezekano wa kuepuka maambukizi huongezeka hadi asilimia 85 mara baada ya kupokea chanjo ya pili.

"Inaonesha kuwa chanjo inafanya kazi," Msemaji wa Taasisi hiyo aliwaambia waandishi wa habari. "Tumeona matokeo makubwa sana ya kupungua kwa kiwango cha maambukizi kwa watu wanaoonesha dalili na wale wasioonesha dalili," alisema.

Kiwango cha wagonjwa wanaolazwa hospitali na wale wanaopoteza maisha kimepungua kwa asilimia 75 baada ya kupata chanjo ya Pfizer-BioNTech, kwa mujibu wa utaifiti uliofanywa katika maeneo ya England na Scotland nchini Uingereza.

Taifa hilo ni moja ya nchi zilizoathiriwa vibaya zaidi na maambukizi ya virusi vya corona kwa kuwapoteza zaidi ya watu 121,000, kwa mujibu wa takwimu za Chuo Kikuu cha John Hopkins.

Uingereza ndilo taifa la kwanza duniani kuanza matumizi ya chanjo ya corona mwezi Desemba, huku zaidi ya watu milioni 17 wakipatiwa chanjo, ikiwa ni sawa na theluthi ya watu wazima nchini humo.

Utafiti wa PHE si wa kwanza kugundua kuwa chanjo inapunguza maambukizi ya virusi vya corona. Mapema mwishoni mwa juma, wizara ya afya ya Israel ilisema kuwa chanjo ya corona ilikuwa na matokeo ya 'kushangaza' ikisema kuwa inasaidia kupunguza uwezekano wa vifo kutokana na virusi hivyo kwa asilimia 98.9.

Takwimu zilizotolewa na Wizara hiyo zinaonesha kuwa chanjo inasaidia kupunguza uwezekano wa kupata maradhi makali kwa kiwango cha asilimia 99.2, na kupunguza uwezekano wa kulazwa hospitali kwa kiwango cha asilimia 98.9, ikihusisha watu waliopatiwa dozi zote za chanjo, siku 14 baada ya kupatiwa dozi ya pili ukilinganisha na wale ambao hawakupatiwa chanjo.

Israel, kama ilivyo kwa Uingereza, imekuwa ikitumia chanjo ya Pfizer-BioNTech. Katika takwimu zingine zinazoonesha matumaini siku ya Jumapili, Taasisi nyingine ya afya yenye makao yake jijini Tel Aviv, Kupat Holim Maccabi, imesema kuwa hakukuwa na kifo chochote kati ya watu 523,000 ndani ya kipindi cha zaidi ya wiki moja baada ya kupata chanjo.
 
Sisi tunasubiria miujiza halafu tukipigwa pini tulalamike mabeberu wanatufanyia makusudi.
 
Wawaongezee wamarekani maana inaonekana ya huko haifanyi kazi vizuri.
 
Back
Top Bottom