FAhamu zaidi kuhusu Chanjo

Kidaya

Member
Dec 20, 2011
55
49
Karibia kila mmoja wetu amewahi kuchoma chanjo ya kujikinga na ugonjwa fulani hasa alipokuwa mtoto. Chanjo za watoto kama chanjo ya kifua kikuu, polio, pepopunda na surua kwa kiasi fulani zimekuwa na mwitikio mkubwa kutokana na kampeni zinazofanywa na serikali na wadau wa afya kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo. Kwa chanjo ambazo wanachomwa watu wazima kama za homa ya ini(hepatitis), homa ya manjano (yellow fever), chanjo ya uviko na chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi taarifa na tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mwitikio umekuwa mdogo hali inayopelekea baadhi ya chanjo kuisha muda wake wa matumizi na kulazimu kuharibiwa licha ya kwamba zilinunuliwa kwa gharama sana. Watu wengi wamekuwa wakikataa au kusita kuchomwa chanjo au kukataza watoto na ndugu zao kuchoma chanjo kutokana na kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa chanjo unaotokana na uelewa mdogo juu ya chanjo. Kupitia makala hii, nitagusia mambo muhimu ya kukuongezea uelew kuhusu chanjo.

1. Chanjo ni nini?
Chanjo ni maandalizi ya kibaiolojia yanayoupa mwili wako kinga hai dhidi ya vimelea vya ugonjwa fulani unaoambukiza.
️Chanjo ina aina ya vimelea (kirusi au bakteria) kisicho kufa au kilicho dhaifu kwahiyo hakiwezi kusababisha ugonjwa au kitu kilichotolewa kwenye miili yao (protini au sukari) kwa ajili ya kuamsha mfumo wako wa kinga uweze kutengeneza kinga dhidi ya kijidudu husika, ili utakapopata maambukizi mwili wako uweze kupambana haraka na kwa mafanikio kuzuia usipate ugonjwa.
Mtu hupewa chanjo kwa njia ya mbalimbali kama kuchomwa sindano kwenye msuli (mfano kwenye bega au paja), matone au kidonge kwa njia ya mdomo, njia ya kupulizia puani n.k kutegemea aina ya chanjo na sifa ya kimelea kinachotegemewa kujengewa kinga.
Uwepo wa chanjo ndio mafanikio makubwa zaidi ya sekta ya afya katika kuzuia magonjwa na vifo tangu dunia iumbwe.️ Japokuwa mafanikio yanaongezeka, wasiwasi kuhusu usalama wa chanjo umekuwa ukiongezeka pia hali inayofanya watu wengi wasite na kukataa kupokea chanjo.

2. Usalama wa Chanjo
Chanjo ni salama na dhabiti. Chanjo hufanyiwa tafiti na majaribio mengi kabla mamlaka za dunia na za nchi husika mfano Advisory Committee on Immunization Practices (ACIP) kuipitisha chanjo fulani itumike na kutoa mapendekezo ya chanzo husika itolewe kwa watu wa umri gani, idadi ya dozi, muda kati ya dozi na dozi, tahadhari na muingiliano wa chanjo na vitu vingine unaoweza kutokea. Ufuatiliaji wa karibu hufanyika kutafuta kama kuna madhara yatakayoripotiwa baada ya matumizi ili kuiboresha zaidi. ️Pamoja na usalama mkubwa wa chanjo, madhara madogo madogo yamewahi kuripotiwa kama kuwashwa eneo la mwili wako ulipochomwa chanjo, homa na uchovu.️ Hakuna madhara makubwa kama kifo, kusababisha ugumba n.k yamewahi kuthibitishwa kusababishwa na chanjo. Watu wengi wamekuwa wakipata wasiwasi kwanini tunachoma chanjo nyingi tofauti tofauti, hii ni kwa sababu magonjwa tofauti yanasababishwa na vimelea tofauti kwahiyo kila kimelea au ugonjwa una chanjo yake kama tuu ilivyo kwa kila ugonjwa una dawa yake.

3. Umri wa mwisho wa kupata chanjo
Umri wa kuchoma chanjo hutegemea kundi la umri gani linalopata zaidi vimelea vya ugonjwa husika na au linaathirika zaidi na ugonjwa husika. Ndio maana kuna chanjo wanapewa watoto tuu, na chanjo za mabinti tuu. Kama vilemea vya ugonjwa vinampata na kumuathiri mtu wa umri wowote basi chanjo hiyo itatolewa kwa watu wa umri wowote kama ilivyo kwa chanjo ya homa ya manjano, uviko n.k. ️Bila kujali umri, wafanyakazi wa afya ni kundi muhimu linalopata chanjo mara kwa mara kutokana na mazingira yao ya kazi kuwa rahisi kwao kupata maambukizi. Kwahiyo chanjo sio kwa ajili ya watoto tuu.

4. Idadi ya kichoma chanjo
Kutokana na ufanisi wa chanjo husika, kuna chanjo inaweza kukukinga kwa maisha yako yote ukichoma mara moja tuu mfano chanjo ya homa ya manjano. ️Chanjo zingine zinaisha nguvu kadri siku zinavyoenda au kadri unavyopata maambukizi ya kujirudiarudia, au kadri kijidudu kinavyojibadilisha (strain) au mwili wako haukupata kinga japo umechoma chanjo, hivyo itakulazimu uchome zaidi ya mara moja (booster dose) ili kukuongezea kinga mfano chanjo ya homa ya ini.

5. Magonjwa mengine ya kuambukiza kama malaria, ukimwi hayana chanjo
Kutengeneza chanjo za baadhi ya magonjwa imekuwa vigumu kwa sababu ya urahisi wa kupata maambukizi ya kujirudiarudia, sifa za kimelea kinachosababisha ugonjwa kujibadilisha mara kwa mara (strain) na vile kinaingiliana na mfumo wa kinga ya mwili. Kwa mfano, kirusi cha ukimwi kinabadilika sana, na kijidudu cha malaria kina hatua nyingi za ukuaji na kinauwezo mkubwa wa kubadilika sana hali inayofanya wanasayansi kupata changamoto ya kutengeneza chanjo yenye ufanisi kwa baadhi ya magonjwa. Taarifa njema ni kuwa kuna majaribio ya chanjo hizo yameanza kufanyika na endapo chanjo zitaonesha ufanisi basi zitaanza kutumika.

6. Kumpa chanjo mtu ambae tayari ana maambukizi au ugonjwa
Mwanzoni chanjo zilikuwa kwa ajili ya kinga tuu kwa mtu ambaye bado hajapata maambukizi au ugonjwa husika, na chanjo zilionesha kuwa na mwingiliano na tiba, na kuwa kama zinamchokoza kimelea kumfanya awe hatari zaidi na vigumu kutibika, hali iliyofanya wagonjwa kuwa na hali mbaya zaidi wakichanjwa. Hali hii ililazimu mtu kufanyiwa uchunguzi na vipimo (screening) kama hana maambukizi kabla ya kumpa chanjo. Kutokana na maendeleo ya teknolojia, baadhi ya chanjo zimeboreshwa na kuwa na sifa ya kusaidia kutibu (therapeutic vaccine) kama mtu ana ugonjwa na kisha kumjengea kinga kwa maambukizi yajayo.

7. Mambo ya kuzingatia kabla hujapewa chanjo
  • ️Umri na jinsia; kuna chanjo wanapewa watu wa umri fulani tuu au wa jinsia fulani tuu, uliza vuzuri kabla ya kupata chanjo usije ukaingia cha kike
  • Historia binafsi na historia ya familia; wewe au wana familia yako kuwa na ugonjwa fulani kunaweza kuwa sababu ya wewe kuhitaji kupata chanjo fulani ili kukukinga
  • Hali yako ya kiafya; kuna chanjo hutakiwi kupewa kama una maambukizi ya kimelea au ugonjwa husika hivyo itakulazimu kufanyiwa vipimo kabla ya kupewa chanjo hizo.
  • Ujauzito; kuna chanjo wanapaswa kupewa wajawazito na kuna chanjo hazifai hazifai kwa wajawazito, toa taarifa kama una ujauzito au unahisi huenda ukawa na ujauzito.
  • Kuwa na kinga dhaifu; chanjo zilizotengezwa kwa kutumia vimelea dhaifu (virusi au bakteria) huweza kusababisha ugonjwa kwa mtu mwenye kinga dhaifu. Ni muhimu sana kufanya vipimo vya kujua uimara wa kinga kabla hujapewa chanjo hizi hasa kwa watu wenye magonjwa ya kudumu au wanaotumia dawa au tiba zinazoshusha kinga ya mwili.
  • Zingatia idadi ya dozi na ratiba chanjo; kama chanjo inatakiwa uchome dozi mara tatu, mfano leo, baada ya mwezi na baada ya miezi sita zingatia kuzipata dozi zote kwa tarehe husika ili kuongeza ufanisi wa chanjo husika. Tafiti zinaonesha changamoto hii ipo sana kwa waliochoma chanjo ya uviko, saratani ya shingo ya kizazi na homa ya ini, wengi hawamalizi dozi hivyo chanjo kutokuwa na ufanisi ulitarajiwa.
  • Madhara; toa taarifa kama chanjo imewahi kukusababishia madhara ya kiafya kama vile mzio (allergy) ili usipewe chanjo hiyo tena na itafutwe chanjo itakayokufaa.
  • Una safari ya kwenda nchi au eneo lenye historia, mazoea au mlipuko wa ugonjwa fulani; choma chanjo husika ndio uende. Kuna baadhi ya nchi huwezi kupata kibali cha kuingia kama huna kadi ya kuonesha umepata chanjo ya homa ya manjano na au ya uviko.
  • Una haki ya kuridhia au kukataa kupata chanjo yoyote baada ya kuelimishwa kuhusu faida, madhara, njia mbadala na kujibiwa maswali yako yote khs chanjo. Pamoja na hiari hii, kuna mazingira unaweza kulazimika kuchomwa chanjo ili upate huduma fulani kama kuingia baadhi ya nchi.

8. Kupungua kwa msisitizo wa kuchoma chanjo fulani
Kampeni na msisitizo wa kuchoma chanjo fulani huweza kupungua au kusiha kabisa kama ilivyo kwa chanjo ya uviko hivi sasa, kwa sababu zifuatazo;
  • Takwimu za hali ya maambukizi ya ugonjwa; kama takwimu zinaonesha maambukizi ya ugonjwa au uhatari wa ugonjwa umepungua au kuisha basi panakuwa hakuna ulazima wa kuendelea kutoa chanjo
  • Kuwa na jamii ya watu wengi waliochanjwa; kama jamii fulani wamechanjwa kwa kiasi kikubwa basi kampeni itaelekezwa kwa jamii ambazo bado hazijachanjwa au makundi fulani tuu.
  • Mabadiliko ya kisera; nchi na mamlaka za afya zinaweza kubadilsha sera za chanjo fulani baada ya kupata ushahidi wa kisayansi na takwimu juu ya ufanisi na ulazima wa chanjo fulani.

Ni muhimu sana kwa wananchi kupata chanjo kulingana na sera za afya zilizopo ili kuweza kukinga watu zetu dhidi ya magonjwa yenye chanjo, na hatimae kufanikiwa kudhibiti na kuyaondoa kabisa baadhi ya magonjwa kwenye nchi zetu kama ambavyo Tanzania tumefanikiwa kuondoa ugonjwa wa polio. Ni wajibu wa kila mtu kupata chanjo inayotolewa kulingana na sera zilizopo ili kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya magonjwa ya kuambukiza yenye chanjo. Ni wajibu wa mamlka za afya kuhakikisha usalama na ufanisi wa chanjo ili kuongeza imani ya jamii juu ya chanjo. Serikali na wadau wa afya tuna wajibu wa kuhakikisha urahisi wa upatikanaji wa chanjo, elimu na taarifa sahihi kuhusu chanjo ili watu wetu wawe na utayari wa kupata chanjo hivyo kufikia malengo ya kidunia ya kudhibiti na kuyaondoa kabisa magonjwa yenye chanjo.

Mwezi huu wa kuongeza uelewa wa jamii juu ya saratani ya shingo ya kizazi, tuwapeleke mabinti zetu kupata chanjo ya kuwakinga dhidi ya virusi vya HPV vinavyochea kwa zaidi ya 95% wanawake kupata saratani ya shingo ya kizazi. Picha kutoka ukurasa wa intsagram wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Screenshot_20230327-170603.png
 
Back
Top Bottom