Halafu nani humu keshawahi kunya pombe chafu? Basi bana, mi nshawahi. Kuna mshikaji wangu mmoja anaitwa Eriki, mama yake alikuwa anazipika na kuziuza hizo pombe chafu.
Alianza na kutengeneza ulanzi, akaja akawa anatengeneza kangala, baadaye akawa anatengeneza wanzuki. Kuna kipindi wanzuki ilibamba sana.
Basi bana hapo nyumbani kwa kina Eriki kwa nyuma kule wakapafanya klabu ya pombe. Mtu kama hujawahi kwenda kwenye klabu ya pombe chafu jaribu tu siku moja ukajionee. Nakwambia hata kama una sonona kiasi gani ukienda itaisha tu maana kuna vituko kushinda maelezo.
Mida ya jioni jioni ndo huwa bomba zaidi. Panachanganya sana maana wabeba zege, wauza mkaa, wasukuma mikokoteni na wengineo wa sampuli hizo ndo wanakuwa wanapitia kuzimua kabla hawajaenda makwao.
Ila usafi ndo hivyo tena. Enzi hizo walikuwa wanatumia makopo ya Tan Bond kunywea. Halafu walikuwa wanashea sasa. Likopo lile linajazwa, linazungushwa raundi na kila mtu anapiga sip.
Binafsi sikuzipenda hizo pombe. Zilikuwa chungu chungu hivi. Ila niliipenda sana pombe ya Kibuku. Ila sina hakika kama na hii ni pombe chafu maana ilikuwa inatengenezwa kiwandani pale Ubungo.
Nshanunua sana mimi hiyo pombe. Halafu ukiiwekea sukari ndo ilikuwa inakuwa bomba zaidi. Hata kilevi chake kilikuwa si cha juu kivile. Nashukuru tu sikuoza meno na kutoka mapengo.