Ushindi mwingine wa Tanzania kwenye vita ya uchumi

ray jay

JF-Expert Member
Sep 27, 2011
1,084
485
USHINDI MWINGINE WA TANZANIA KWENYE VITA YA UCHUMI

Na Bwanku M Bwanku

Jana Oktoba 13, 2020 Tanzania na dunia kwa ujumla ilishuhudia tukio kubwa la kihistoria na la ushindi kwa nchi ya Tanzania kwenye vita nzito ya kiuchumi. Kwenye tukio hilo, Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliwaongoza Watanzania wote kupokea gawio la pili kutoka kampuni ya madini ya Barrick la bilioni 100 kama faida ya biashara ya madini, fidia ya malimbikizo ya kodi na mafanikio ya kupitia upya mikataba ya madini na sheria zinazolinda rasilimali za Tanzania.

Mfululizo wa magawio haya ya Barrick na uvunaji mwingine mkubwa wa faida ya madini kwenda kwa Serikali ya Tanzania yanakuja baada ya sakata la mchanga wa madini ya dhahabu lililopata umaarufu mkubwa sana mwaka 2017 kama ripoti ya Makinikia, sakata lililoibuliwa na ripoti mbili za kamati ya Prof Mruma na ile ya Prof Osoro zilizobaini kuwepo kwa wizi mkubwa na wa muda mrefu wa madini ya dhahabu kwenye migodi ya Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara uliokuwa ukifanywa na kampuni tanzu ya Barrick, Acacia.

Baada ya mgogoro huo, majadiliano ya muda mrefu mrefu yaliyochukua zaidi ya miaka miwili kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni mama ya Barrick yakaanza, majadiliano yaliyojikita kutatua mgogoro huo wa kikodi kati ya pande hizo mbili baada ya kampuni hiyo kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini kinyume na sheria na kukwepa kodi.

Licha ya sauti za Watanzania wenzetu kutoa lugha za vitisho na kunanga kwa Serikali kwamba ingeshtakiwa na kwamba isingelipwa kwenye mazungumzo hayo lakini Serikali iliendelea kusimamia msimamo wake wa kusimamia haki na maslahi ya Watanzania mpaka Barrick iliposanda na kukubali kuilipa Serikali ya Tanzania Dola za Kimarekani Million 300 (Ths Bil 682.5), kugawana faida sawa ya kiuchumi kati yake na Tanzania kwa 50 kwa 50 huku serikali ikipandisha hisa zake kutoka sifuri mpaka asilimia 16 kwa kila mgodi.

Katika msururu wa makubaliano hayo hatimaye Januari mwaka huu, Serikali ikafungua ukurasa mpya wa sekta ya madini baada ya kusaini mkataba wa makubaliano ya pamoja kuunda na kuendesha kampuni mpya ya Twiga, kampuni mpya ya madini iliyoundwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Barrick baada ya ile ya mwanzo (Acacia) kufa kwa mgogoro huo wa kikodi.

Kampuni mpya ya Madini ya Twiga, iliyoundwa kutoka Acacia ikafungua ukurasa mpya zaidi wa usimamizi na ulinzi wa rasilimali za nchi. Acacia iliyokuwa na ofisi zake na mitambo yote ya kuchakata madini nje, sasa kampuni mpya ya madini ya Twiga, iliyoundwa kwa ubia wa Tanzania na Barrick baada ya kifo cha Acacia ikatakiwa iendesha shughuli zake zote hapa hapa nchini na kuhamisha maskani yake nje ya nchi huku waendeshaji wakuu wa kampuni hii wakiwa wazawa. Kumbuka kampuni ile ya Acacia licha ya kushughulika na madini ya Tanzania lakini ilikuwa ikisimamiwa na kuendeshwa nje ya nchi tena Watanzania wakiwa hawana sauti na kutohusika kabisa.

Baada ya mgogoro wa kikodi na Serikali kuitaka kampuni hiyo ilipe fidia kwenye ulimbikizaji wake wa kodi, hatimaye Jumanne ya Mei 26 mwaka huu kampuni hiyo ya Acacia iliyokufa kwa mgogoro huo kupitia Barrick ikaanza kuilipa Tanzania Dola Million 100 (Tshs Bil 250) kama sehemu tu ya awamu ya kwanza ya fedha za makubaliano Dola Milioni 300 iliyotakiwa kulipa kama fidia ya kodi.

Mbali ya makubaliano hayo ya kuendelea kupata magawio, kubwa zingine ni kwamba kampuni hiyo ya Barrick itakua ikitoa Dola Million 5 kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa mtambo mkubwa wa kuchakata madini hapahapa nchini badala ya ile ambayo mitambo yote ya kuchakata madini iko nje ya nchi. Sasa shughuli zote za kuchakata madini na kuyachuja itakuwa ikifanyika hapa nchini, kuajiri Watanzania hapahapa na faida zote za uendeshwaji wa shughuli hizo nchini.

Pia Barrick imeanzisha ushirikiano na Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kutoa Dola za Kimarekani Million 10 kwa kipindi cha miaka 10 kwa ajili ya kutoa mafunzo ya madini hapa hapa nchini. Kwa maana hiyo wataalamu wote wa madini watakuwa wanapikwa hapa hapa nchini.

Zaidi makubaliano hayo yote hapo juu ni nje ya makubaliano mengine makubwa ya kugawana faida sawa ya kiuchumi ya 50 kwa 50 zinazotokana na madini nchini. Zaidi kupanda kwa hisa ya Serikali kwa migodi hiyo mitatu. Kumbuka Serikali ilikuwa ina sifuri kwenye madini hayo kwa miaka mingi sana lakini leo itapata faida sawa za kiuchumi tena kwenye Kampuni ya Twiga ambayo pande zote mbili kati ya Tanzania na Barrick zina maamuzi sawa tofauti na ile ya mwanzo ya Acacia.

Yaani maana yake Acacia imekufa na sasa kuna Twiga Company ambayo Tanzania na Barrick wana sauti sawa kiuongozi na kimaamuzi na sasa faida ya madini kutoka Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara itakuwa sawa yani 50 kwa 50 kutoka kupata 0.

Huu ni ushindi mkubwa sana na wa kihistoria sana kwa Tanzania na Afrika nzima kwenye sekta hizi muhimu za uchumi na uwekezaji kuelekea kuzifanya sekta hizo zisaidie Tanzania na kuchangia pakubwa kwenye pato na uchumi wa Tanzania na zaidi akiliamsha bara zima la Afrika kusimama kidete kulinda rasilimali zake.

Tanzania ni moja ya nchi zilizobarikiwa rasilimali nyingi sana za madini ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa hili. Rasilimali hizi kama zitatumika kwa tija na maslahi ya Taifa basi zitaleta ushindi na mafanikio makubwa sana kwenye safari na ndoto ya Taifa hili kujenga uchumi wa kati wa juu zaidi.

Huu ni ushindi unaotuma ujumbe kwa makampuni na wawekezaji kote duniani kuheshimu na kufanya biashara kwa kile kinachoitwa Win-win situations. Kufanya biashara na uwekezaji unaonufaisha na kufaidisha pande zote. Hii ya makampuni ya nje kudhani Afrika ni shamba la bibi kwa kuvuna na kupata wanachokitaka inapaswa kukomeshwa kwa viongozi wa Afrika kusimama na kuweka misimamo isiyoyumbishwa linapokuja suala la maslahi na kutetea rasilimali zao. Tanzania imeonyesha njia. Afrika inapaswa kuamka.

0657475347
 
Dakitari Magufuli oyeeeeeeeeeeeeeeee

Rais wa awamu ya sita Dakitari Magufuli oyeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee
 
Back
Top Bottom