Kwanza ningependa kukupongeza kwa juhudi zako za kutaka kuliboresha jiji letu hili la Dar. Nimekuwa nikifuatilia juhudi zako tangu ulipokuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni. Naamini jitihada zako za kutaka kuboresha wilaya ya Kinondoni ndizo zilizomfanya Raisi akuongezee majukumu kutokana na kuona jinsi unavyochapa kazi.
Kwa muda sasa nimekuwa nikiona unaibuka kila siku na matamko ambayo baadhi ya matamko hayo hayajafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa mfano suala la ombaomba. Kwa ushauri wangu kabla ya kutoa matamko naomba ufanye utafiti mdogo kwanza na kujiridhisha na kuweka mpango kazi wa namna ya kutatua tatizo kabla ya na kutoa tamko kwamba hutaki jambo fulani katika mkoa wako. Kuna vita vingine hutaviweza zaidi ya kujifedhehesha.
Kwa ushauri wangu naomba uweke vipaumbele katika mambo yafuatayo.
=Kumaliza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati katika shule zetu
=Kuongeza na kuboresha maabara katika shule zetu
=Kujenga maktaba katika shule na maeneo mbalimbali kwa kuanzia ngazi ya kata na kuhakikisha kunapatikana huduma za inteneti na magazeti ya kila ziku hapa unaweza kuzishirikisha kata kutenga maeneo kwa ajili ya kujengwa kwa maktaba hizo ili kuhimiza watu kujisomea na kuongeza maarifa na sio kupiga soga vibarazani na kunywa kahawa
=Kuhakikisha jiji linakuwa safi kwa kuweka sheria ndogo ndogo kali zitakazowabana wachafuzi wa mazingira na ili kulitekeleza hili unaweza kupata uzoefu kutoka kwa viongozi wa mji wa Moshi
=Kupiga marufuku mifuko ya plastiki kutumika hapa jijini na badala yake wenye viwanda hivyo kulazimishwa kuzalisha mifuko ya karatasi kwa ajili ya matumizi au kushirikiana na SIDO kuja na njia mbadala ya mifuko ya karatasi ambapo ubunifu huo unaweza kuwezesha vikundi vidogo vidogo vya vijana na kina mama..
=Kutengeneza maeneo ya vivutio kwa watalii wanaokuja katika jiji letu kwani wengi hupita tu kwa sababu hakuna vivutio. Hili unaweza kuwashirikisha wabunifu na wakandarasi wetu na kutenga maeneo ambayo yana historia na kuyaboresha kwa kiwango ambacho kitavuta wataalii wengi kutumia siku kadhaa katika jiji letu kwa mfano kama mji mkongwe wa Zanzibar, na Makumbusho ni eneo mojawapo ambalo linaweza kuboreshwea zaidi.
=Kuweka utaratibu mzuri wa boda boda, kwa sasa bodaboda pamoja na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Dar lakini zimekuwa ni chanzo kikuu cha ajali hapa jijini na vijana wengi wamekufa au kupoteza viungo na hivyo kutishia nguvu kazi hapa nchini. Tusipoweka utaratibu na kutoa elimu kwa waendesha bodaboda na madereva kuheshimu sheria za barabarani na kuweka sheria kali kwa watakaokiuka miaka kumi ijayo nchi hii itakuwa na ukosefu wa nguvu kazi.
=Tenga maeneo mengi kwa ajili ya vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi na maeneo haya yakabidhiwe VETA ili vijana ambao wameshindwa kuendelea na masomo wapate fursa nyingine ya kujifunza masomo ya ufundi lakini pia ni vyema kukitengwa maeneo ya mafundi wetu kwa mfano mafundi wa magari kuwe na eneo lao, mafundi seremala wae na maeneo yao kama vile Keko, mafundi wa kuchomea vyuma wawe na maeneo yao ili wenye kuhitaji huduma hizo wawe wanajua zinapatikana wapi na kuondoa hizi vurugu mitaani
=Rejesha viwanja vya michezo vilivyovamiwa na hakikisha swala la viwanja vya michezo linapewa kipaumbele, na michezo isiwe ya aina moja, ongeza wigo wa michezo mbalimbali ili na sisi tuweze kushiriki michezo ya olimpiki.
=Mabango na matangazo yawekewe utaratibu maalum siyo kila mtu akiwa na tangazo lake anapita mitaani na kuchafua kuta za watu itungwe sheria kuondoa tatizo hilo n ahata haya makampuni ya matangazo nayo pia yawekewe utaratibu maalum kuondoa mabango mengi mitaani na kufanya jiji lisionekane nadhifu.
=Wanaohubiri usiku kucha na kelele za mziki kwenye mabaa katika makazi ya watu zipigwe marufuku na kila Pub kama watataka kupiga mziki kwa sauti ya juu basi lazima wawe na ukumbi usioruhu sauti kutoka nje.
=Njoo na njia mbadala ya kuhimiza matumizi ya baiskeli kwa wale wanaofanya kazi maeneo ya karibu na hili litafanikiwa kwa wakandarasi wetu kubuni njia ya waendeshao baiskeli ili kuepuka bughdha kwa watembeao kwa miguu. Mpango huu unaweza kuanza na zile barabara ndefu kama Tegeta mpaka Posta, Gongo la Mboto mpaka Posta, Mbagala mpaka Posta.
Mimi naamini kama ukiweka vipaumbele kwenye mambo hayo machache kati ya mengi ambayo sijayazungumzia utaacha historia katika jiji hili na utakumbukwa na vizazi vijavyo.
Unaweza kuitisha mdahalo kwa wakazi wa jiji hili ili kupitia mdahalo huo uweze kuibua mbinu mbalimbali za kuboresha jiji letu. Naamini wakaazi wa jiji hili hawafurahishwi na hali jinsi ilivyo kwa sasa na wangependa hali iwe nzuri zaidi kwa kuondoa kero nilizozitaja hapo juu, iwapo utawaalika kwenye mdahalo watakupa ushirikiano.
Nakutakia kila la kheri katika majukumu yako ya kila siku.
Ni mimi Mzee Mtambuzi.