Niliwahi kuona tangazo katika mtandao wakati Fulani , mmoja wa wabunge wa upinzani Tanzania ameacha namba yake ya simu atakayotumia atakapofika marekani , kwa wale ambao hawako busy wanapenda kuonana nae na vijana wengine wengi wenye muelekeo wa kipinzani .
Tafadhali tuoneshe tangazo hilo na uliliona wapi, "mtandao fulani" usije kuwa ni wa kufikirika. Tuoneshe ilo tangazo na hasa hapo liliposema kuwa "kwa wale ambao hawako busy wanapenda kuonana nae na vijana wengine wengi wenye muelekeo wa kipinzani". Utajijengea heshima kweli kama utamtaja Mbunge huyo na wapi uliona Tangazo hilo lenye maudhui hayo. Binafsi sijaliona na hivyo siwezi kusema kama lipo au halipo. Kama kuna mtu mwingine ameliona tunaomba atusaidie.
Sitaki kubisha inaonekana wapinzani wamewashika sana vijana wa kitanzania walio nchi za nje haswa marekani
Kuonekana kwa kitu kwenye fikra za mtu hakuwezi kuzuilika; kwa mfano inaonekana mafisadi wamewashika watu wengi wa Arusha na Bariadi kiasi kwamba na akili zao timamu wanakurupuka kuwapokea kwa shangwe watu walijiuzulu kwa kashfa!
kiasi kwamba zitto anapokanyaga huko wanaona mwokozi wao kafika watu wanasongamana wanataka kumwona kupiga nae picha na vitu kama hivyo .
Ni lini tena Zitto amewahi kukanyaga huku? Cha kushangaza umeshindwa kusema kuhusu maelfu ya watanzania waliokusanyika Jangwani kumsikiliza na wale waliojitokeza katika sehemu mbalimbali za mikoa ya Tanzania. Iweje Zitto kupokewa kama "Mwokozi" Tanzania na Watanzania wenzake ni jambo la kufurahia lakini akipokewa kiukimya Tanzania imekuwa nongwa?
Kwa kukupa taarifa tu, ni mimi niliyempokea uwanja wa ndege na hakukuwa na vimulimuli, saluti, pikipiki, na ngoma za sindimba kama alivyopokewa mzee wa Vijisenti ambaye anaonekana ni mwokozi kule Bariadi! au alivyopokewa yule mwenye ndege iliyopaa huku abiria wameachwa wameduwaa!!
Zitto hakupokewa kwa mbwembwe wala shangwe! Alipokewa kwa heshima ya kiongozi ambaye ameonesha uungwana wa kuja kututembelea hapa kwa gharama zake mwenyewe! Sisi tulitumia kidogo tu kwa chakula na zawadi za jiji la Magari!
Pamoja na kuacha hizo namba za simu na watanzania kujitokeza kuonana nae , sera na mambo anayoongea katika mikutano hii ni zile zile
Mambo mengine ni ya kufikirika, Kwanini mtu abadilishe sera anazozungumzia wakati tatizo bado ni lile lile? Hii inaelezea ni kwa sababu gani watawala wetu wameacha mambo ya msingi na sasa hawana cha kushikilia na badala yake hawachoki kuja na mipango mipya huku ya zamani ikiwa imekufa. Mara MKUTAKUTA, mara MFISADIKA, mara UKURUTU, n.k.. matatizo ya watanzania yako pale pale.
za ufisadi ambazo sasa hivi ni zilipendwa , yale yale ya epa na mambo mengine ambayo kwa hakika sio ya kujenga upinzani sio ya kujenga nchi ni ya kupasua hadhi ya nchi na watu wake nje ya mipaka yake .
Hii ni kejeli kwa Watanzania; yaani wewe ufisadi ni suala ambalo mtu alifumbie mdomo? yaani masuala ya EPA kwako ni masuala ya yaliyopitwa na wakati? Leo hii serikali haijui nani mmiliki wa Tangold, wewe unasema imepitwa na wakati? Leo hii haijulikani fedha zinazolipwa Dowans zinakwenda wapi wewe unasema zimepitwa na wakati? leo hii fedha zinaingia upande huu na kutokea upande ule wewe unasema kuzungumzia ni "imepitwa na wakati". Tupe pendekezo basi tuzungumzie mambo ya wakati kama siyo haya yaliyosimika mkuki wa ufisadi nje ya nyumba zetu na kuingia ndani na kuchukua mali na hazina ya watu wa Taifa hili? Wewe unasema yamepitwa na wakati!?
Namheshimu Nyepesi na Wenzake wengi kama watanzania lakini siwezi kuheshimu na kuendelea kusikiliza watu wenye mawazo ya kuvuruga wananchi wakiwa nje ya mipaka yao huwa nashangaa kama hawana masuala mengine ya kuongea zaidi ya haya .
Sijui "Nyepesi" ni nani, lakini inasikitikisha kuwa umeingia kwenye mtego wa kina Lowassa kuwa Wazalendo wa kweli na pekee ni wale walioko nyumbani; kwamba sisi tulioko nje ya nchi ni Watanzania nusu ambao hatutakiwi kutolea maoni. Kwa mawazo yako ni kuwa Mtanzania akishatoka nje ya mipaka basi utanzania wake umepungua kidogo na kwa kadiri anavyoenda mbali na ardhi ya Tanzania ndivyo ambavyo anatakiwa kukaa kimya!
Watu wana mambo mengi ya kuzungumzia ndani na nje ya nchi yao na si wewe na wala si mtu yeyote anayeweza kuamua vinginevyo. Kama ungechukua muda kidogo kusoma Katiba yetu ungeona kuwa haitoi mipaka ya maoni kuwa "mtanzania atakuwa na uhuru wa maoni akiwa Sumve, lakini akienda Mombasa maoni yake yatakoma!". Katika Katiba hiyo hakuna mahalia ambapo panasema "Mtanzania atazungumzia jambo hili akiwa Magomeni lakini akiwa London itakuwa mwiko". Ungeliewa hili ndugu yangu ungefurahia mchango wa mawazo ya watanzania wawapo nyumbani, wavukapo mipaka ya nchi yao na hata wale ambao wanaishi ugenini miaka nenda rudi. Usiwabague Watanzania kwa sababu ya ukazi wao kwa kujifanya wewe ni bora kuliko.
Pamoja na maneno yako hayo, hatutawaachia nchi mafisadi, na hatutapiga magoti mbele ya wabakaji wa nchi yetu na wezi wa mali za taifa letu. Hatutawaimbia nyimbo za shangwe waliondamwa na kashfa na wale watubezao hatuwasusia nchi!
Hao ni chadema ndio wameshikilia Epa , Ufisadi na Usalama wa Taifa ,
Wakati mwingine mtu anaandika hata ajuia anaandika nini? Hivi unataka kutuambia EPA, ufisadi na Usalama wa Taifa mbovu kabisa ndio Chadema? na CCM wamefanya nini? Ndio watetezi wa Taifa hili? Give me a break!
ukirudi kwa upande wa baba zako chama cha wananchi CUF , ningekuwa mimi ni mwanachama wa CUF ningehoji kwanini hao viongozi wawili wa CUF wako pale walipo mpaka sasa hivi
sasa kama ni si mwanachama wa CUF kwanini uhoji mambo ya CUF; Badala yake ungeuliza huko CCM (kama wewe ni mwanachama) imekuwaje Makamba na Kingunge wanasimamia muafaka? Wana ujuzi gani wa utatuzi wa migogoro? Wangempa Januari nafasi hiyo kwani angalau yeye kasomea mambo hayo!!
Tangia upinzani umeanzishwa ni viongozi wale wale wa CUF wanaowashika masikio baadhi ya wanachama wao , ni viongozi wale wale wakorofi wako madarakani katika chama hicho mpaka sasa hivi , sijui CUF hawana viongozi wengine ni lazima wawe hawa hwaw ?
Unatania! Viongozi wale wale? Hivi unataka tuanze kuhoji ni chama gani kina viongozi wale wale katika nafasi zake nyingi Tanzania? Kama hujui naomba uulize tu na nitakufa na furaha kuanza kukuorodheshea viongozi wakongwe katika chama fulani na serikali yake hadi sasa watoto na watoto wa watoto wao nao wameanza kurithi vyao! Kama ni sahihi kwa chama hicho iweje liwe kosa kwenye vyama vingine?
Mtihani wao wa kwanza wameshaushindwa wa kuleta maelewano huko visiwani , kwa sababu wameshashindwa jaribio hilo , sioni sababu ya kwanini wasiache nafasi hizo wazi waje watu wengine wenye utashi zaidi yao , watu wanaopenda kukaa mezani na kumaliza tofauti zao .
Huu ni mtihani wa CCM; ni wao wameshindwa na sasa wameanza kutumia nguvu za dola! Wameshindwa kwenye meza ya majadiliano na sasa wanaanza kutumia virungu vya kulazimishana. Nakubaliana na wewe hawa kina Makamba na Kingunge "kwanini wasiachie nafasi hizo wazi waje watu wengine wenye utashi zaidi yao, watu wanaopenda kukaa mezani na kumaliza tofauti zao". Hili ni kweli, kwanini kina Makamba wasiachie ngazi?!
Niliangalia hata wakati wa maandamano ya CUF visiwani wiki iliyopita mmoja wa washairi aliposema kwamba anaweza kujilipua kama mambo yataendelea kuwa hivyo , wengine wakawaambia wenzao wasipeleka bidhaa katika kisiwa kingine wakipeleka basi wao ni halali yao .
Yote hayo yanasemwa viongozi wa CUF wamekaa katika viti wanasinzia wengine wanacheka na kufurahia kwa madaha kama vile ile ni halali yao kusema vile na hakuna chochote kile mbele yake .
Nilitegemea mmoja wa viongozi hawa au msemaji wa CUF aje mbele na kusema kile kilichosomwa na yule mshairi sio msimamo wa CUF lakini hakikutokea kitu kama hicho kwahiyo tuchukulie basi kuanzia sasa hivi na mpaka hapo viongozi wa CUF watakapoamua baadaye
Kwamba sera za CUF kuanzia sasa hivi ni KUJILIPUA , KUKATAZA BIASHARA NA UNGUJA NA KUPUNGUZA UNDUGU WAO kwa sababu hawa wengine sio wanachama wao , wao ni CCM.
Wewe unaweza kuchukulia vyovyote lakini mtu anayehisi kunyanyaswa, kuteswa na kunyimwa nafasi ya kuthaminiwa na kutambuliwa utu wake kwenye nchi yake yeye mwenyewe unampa option gani? Tusitengeneze matatizo sisi wenyewe halafu tulaumu wengine. Kuanza kukamata watu na kuwatia kizuizini haiwezekani kuwa ni suluhisho la kudumu la matatizo ya kisiasa. Afrika Kusini walishindwa, Israeli wameshinda, Sadam alishindwa, Hitler alishindwa, Stalin alishindwa na CCM na serikali yake itashindwa vile vile.
Roho ya mwanadamu haifungwi pingu na tamanio la kutambuliwa utu, hadhi, usawa, na heshima ya mwanadamu haikomi kwa mwili kutiwa gerezani. Hakuna Taifa lililoweza kabisa kuzima matamanio ya watu kutambuliwa haki na nafasi yao katika jamii yao.
Njia pekee ya kutatua matatizo ya Pemba si kufungua kesi za uhaini kwani mkiwafunga hawa watoto wao watakuja kuhoji, na mkiwafunga watoto, wajukuu na vilembwe hadi vining'ina vitakuja kuhoji! Njia pekee ni kukaa chini kama ndugu na watu walio sawa, kuchambua tatizo na kiini cha tatizo, kukubali mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi, kutoa mapendekezo na kukubali kutokupata yote mtu atakayo (compromise). Kwa mtindo huu wa CCM kuwa inataka ipate yote, ijue inapandikiza mbegu za tatizo la umilele katika visiwa hivyo.
Ndugu Shy,
Wivu ni kitu kibaya sana na mtu mwenye wivu ni mtu ambaye hawezi kuona wema wa mtu mwingine. Mtu mwenye wivu hutiwa kiza cha macho kiasi kwamba lolote analofanya mbaya wake hata la kuja kumsaidia wakati nyumba yake inaungua mtu huyo atalichukulia kama njama. Ni wazi umezoea siasa za uzugaji ambapo wanasiasa wanafanya mambo kwa kujipendekeza tu na anapotokea kijana mdogo kama Zitto kutikisa nchi kwa kweli haingii akilini.
Alichokifanya Zitto kimeandikwa katika historia na kamwe hakuna anayeweza kufuta! Mchango wa Zitto kwenye mjadala wa hatima ya Tanzania na hali ya kisiasa ni mchango wa kukumbuka na ninaona fahari kabisa kutangaza kuwa natofautiana na Zitto kwenye mambo kadhaa lakini kwenye mambo mengi tuko karibu mno kuliko nilivyodhania. Nilipinga yeye kuingia kwenye Kamati ya Rais ya Madini na yeye anajua hivyo, lakini nimeheshimu ushiriki wake na mchango wake na historia itatuhukumu sote wawili. Na kwa kadiri ninavyoelewa sasa, nadhani historia itanihukumu mimi vibaya zaidi katika hilo.
Lakini nashangaa kwanini umetugusa sisi tulioko Marekani na kutuona kama mazezeta kwamba tunamfuata mtu alimradi tu? Mbona hujahoji Rais Kikwete alipokuja na kukutana na Watanzania New York? au DC? Hii Jumamosi iliyopita Rais Karume alikutana na jumuiya ya Watanzania DC kwanini hilo kwako ni sawa?
Kwa taarifa yako, Mhe. Zitto ni kiongozi wa Kitaifa na si wa Chadema tu. Ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano ambapo pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia Mashirika ya Umma. Kwanini asikutane na watanzania popote pale anapotaka?
Na nikuhakikishie tu na kukutoa hofu kuwa watakapokuja wabunge wengine wa CUF, au UDP au CCM na wakawa tayari kukutana nasi tutawapokea kwa mikono miwili isiyo na ubaguzi kama unaoupendekeza wewe. Na kwa taarifa yako, Zitto alipokuja hapa nilimuambia mapema kuwa mkutano huu si wa kisiasa, si kufungua tawi na siyo wa chama fulani. Aliheshimu hilo kwani hata watu walipokuwa wanauliza maswali kuhusu Chadema aliyakwepa na kuwakumbusha wasikilizaji kuwa mkutano haukuwa kuhusu Chadema.
Kama Pinda angeweza kufanya hilo alipoenda Iringa kwenye Mei Mosi na kutumia raslimali za serikali kufanya shughuli za CCM basi angeonekana ni mtu makini.
Natumaini nimekusaidia kuondoa wingu la utata, na chuki ya chinichini uliyoianzisha hapa.