SoC02 Unataka kuwa na furaha wakati wote? Jifunze sasa kufanya hivyo. Inalipa

Stories of Change - 2022 Competition

Mnyakyusa5000

Member
Sep 21, 2021
61
117
Umeshawahi kujiuliza kuwa ni nini utakachokifanya ikitokea utapata kila kitu unachokihitaji maishani? Ukiwa na kila kitu unachokitaka. Ukiwa na mpenzi au familia unayoitaka, kiasi cha fedha unachokitaka, kila aina ya mali unayoitaka. Utafanya nini baada ya hapo? Kama hujawahi kujiuliza swali kama hilo basi nakuomba ujiulize Leo na sasa hivi. Jiulize hivi. “Ikitokea nimepata kila kitu ninachokitaka maishani, nitafanya nini baada ya hapo?”

Maisha yetu yana mtego mkubwa sana. Kutofahamu ukweli kuhusu jambo hili kumetufanya tuishi maisha ya mateso yasiyokuwa na sababu ya msingi. Majibu ya swali letu hapo juu kwa vyovyote vile yatakavyojibiwa ingawa sio rahisi kujibu, yanatufanya tujihoji ni nini hasa kusudi la maisha yetu.

Asili na kusudi la maisha ya binadamu ni kuishi kwa furaha wakati wote. Kila kitu ambacho mtu hutafuta, hutafuta ili kimletee furaha katika maisha yake. Kila kitu. Fedha, mahusiano, pepo maendeleo na vingine vingi. Tunavitafuta vyote hivi ili tupate kitu kimoja tu. FURAHA.

Kwa bahati mbaya sana, vitu vyote tunavyovitafuta ili vitupe furaha haviwezi kufanya hivyo. Hii ni kwa sababu furaha sio matokeo ya kuwa na kila kitu tunachokihitaji. Bali furaha ni chanzo cha kupata kila kitu tunachokitaka. Furaha ndio msingi wa maisha yetu. Furaha ndio asili ya maisha yetu. Ukiwa na msingi huu muhimu katika maisha yako basi kila kitu unachikihitaji kitakuja kwako.

Katika makala hii tutaangazia kwa ufupi mambo yafuatayo: Maana ya furaha, nini huwakosesha watu furaha, namna gani tunaweza kuwa na furaha wakati wote na ni zipi faida za kuwa mtu mwenye furaha wakati wote.

Furaha ni nini?
Sio rahisi kujua maana sahihi ya furaha kwa kusoma kutoka katika kamusi. Hii ni kwa sababu maana zilizopo kwenye kamusi huturudisha kwenye jambo lile tulilolijadili katika utangulizi. Kwamba furaha ni hali anayokuwa nayo mtu baada ya kupata ama kufanikiwa kupata vitu anavyohitaji. Pengine maneno yanaweza kuwa tofauti. Lakini kwa uhakika ni kuwa maana nyingi kama sio zote za neno furaha katika kamusi huelezea kuhusu dhana inayofanana na tuliyoiona. Ambayo kwa kweli ni maana tegemezi na tunaweza kusema kuwa inapotosha maana ya msingi ya furaha.

Ukweli ni kwamba furaha ni hali ya kuwa na utulivu wa kudumu ndani ya nafsi ya mtu. Utulivu huu hautegemei kitu chochote isipokuwa uelewa wa mtu husika kuwa hakuna kitu chochote kinachoweza kumpa utulivu wa aina hii isipokuwa uelewa wake.

Kama tutaelewa kuwa furaha ina maana kama tuliyoiona hapo juu basi ni rahisi kuelewa kuwa hali ya kuwa na kila kitu tunachokihitaji katika maisha yetu hakutupi furaha isipokuwa hofu hasa ya kuvipoteza vitu hivyo. Hii ndio sababu mara nyingi watu wanaosemekana kuwa wana kila kitu ambacho mtu angehitaji kuwa nacho ndio huongoza kuonesha dalili za kutokuwa na furaha katika maisha yao.

Nini huwakosesha watu furaha?
Tukizingatia maana halisi ya furaha kama tuliyoiona hapo juu ni wazi kuwa watu hukosa furaha kwa sababu kuu moja ambayo ni ukosefu wa uelewa juu ya furaha ni nini hasa. Kutojua jambo hili hiwafanya watu kuwa watumwa wa vitu ambavyo wao wanaamini kuwa huenda ndio chanzo cha furaha yao. Na kwa vile binadamu ni kiumbe mwenye asili ya kutaka kuwa huru, hali hii huzidi kuwakoseha furaha.

Jambo jingine ambalo huwafanya watu kutokuwa na furaha ni ukosefu wa uelewa juu ya misingi ya maisha ya binadamu. Binadamu ni mkusanyiko wa vitu vinne kwa pamoja. Vitu hivyo ni mwili, akili, hisia na roho ambayo wakati mwingine hujulikana kama ndio uhai wenyewe.

Vitu hivi vinne hufanya kazi kwa kujitegemea. Mwili hauhitaji ruhusa yako kupumua, kuendesha mapigo ya moyo na vitu vingine kama hivyo. Akili haihitaji ruhusa yako kuwaza hufanya hivyo pale inapotaka kufanya hivyo. Hisia tofautitofauti huja wakati wowote zinapotaka kuja. Roho nayo huweza kutoka wakati wowote bila hata ruhusa yako, alimradi tu kuna mzingira ya yenyewe kutoka.

Ufahamu mdogo wa jinsi ya kuweza kumudu na kuendesha misingi minne ya maisha ya binadamu yaani mwili, akili, hisia na roho umetufanya binadamu tuishi maisha kama ajali. Tunapelekeshwa na vitu hivi. Ndio sababu tunakosa furaha katika maisha yetu.

Kama kwa namna yoyote ile uliwahi kufikiri kuwa kuna kitu chochote nje ya tulivyoviorodhesha hapo juu kama chanzo cha wewe kukosa furaha basi ni muhimu kubadilisha fikra zako. Hii ni kwa sababu furaha hutokea ndani ya nafsi ya mtu hivyo kwa namna yoyote ile sehemu pekee ambayo furaha hupotea ni ndani ya nafsi ya mtu. Hakuna kitu chochote nje ya nafsi yako chenye uwezo wa kukukosesha furaha yako Vila ruhusa kutoka ndani ya nafsi yako wewe mwenyewe.

Namna gani tunaweza kuwa na furaha wakati wote?
Ni rahisi kuwa na furaha wakati wote ingawa inahitaji mazoezi. Kama tulivyoona hapo swali, ukosefu wa furaha kwenye maisha yetu husababishwa na ukosefu wa uelewa sahihi juu ya dhana ya furaha na misingi minne ya maisha ya binadamu.

Kama hivyo ndivyo ilivyo basi, uelewa sahihi juu ya mambo haya ndio njia pekee ya kuwa na furaha wakati wote.

Tayari tumekwisha ona na kuelewa juu ya dhana sahihi ya neno furaha. Hebu sasa tuangalie na kuongeza uelewa wetu juu ya misingi minne ya maisha ya binadamu. (mwili, akili, hisia na roho.)

Mwili
Mwili wa binadamu ni mashine ya kipekee sana. Uelewa mdogo juu ya miili yetu na jinsi inavyofanya kazi kutufanya tukose furaha mara kwa mara. Kwa mfano, pale mwili unapouma au kuonesha dalili za kuumwa au kuhisi njaa na kiu, hipelekea watu wengi kukosa furaha.

Ukweli ni kwamba mwili unapouma au kuonesha dalili za ugonjwa ni njia ya mwili kuwasiliana na sisi wamiliki wake kuwa kuna jambo halipo sawa na hivyo hatua za muhimu kama vile kwenda hospitali ama kujipatia maji ya kunywa au chakula inabidi zichukuliwe. Kwa hivyo kwa namna yoyote ile hatupaswi kukosa furaha eti kwa sababu miili yetu inauma. Maumivu ni mazuri kwani ni njia ya mwili kujilinda.

Mwili pia una mahitaji yake ya ziada kama vile ngono na mahitaji ya mazoea kama vile vinywaji visivyo vya lazima kama vile soda na pombe. Mara zote mwili unapohitaji vitu kama hivi hutoa ishara fulani ya maumivu. Ni jukukumu letu kuuelewa na sio kupoteza furaha zetu. Pia ni muhimu kuuchagulia nini cha kuupa hasa katika mahitaji haya ya ziada kwani mahitaji haya huwa na athari hasi kwa mwili. Uelewa mwili wako. Kwa kufanya hivyo utakuwa na furaha daima.

Akili
Akili ni mkusanyiko wa mambo mawili. Kumbukumbu na matarajio kwa ujumla tunayaita mambo haya kuwa ni mawazo. Kama kwa namna yoyote ile unahitaji kuwa na furaha wakati wote, ni muhimu kuelewa kuwa mawazo yako hayana kitu chochote kipya. Ni kumbukumbu na matarajio. Usijaribu kuikataza akili yako kuwaza. Hapana. Ielewe akili yako na uiache iwaze kwa namna inavyotaka yenyewe.

Jambo la msingi ni kwamba mara zote inapowaza uwe macho kuitazama. Kitendo cha kutojua kuwa akili yetu ndio inayowaza kimetufanya tukurupuke kupoteza furaha zetu tukidhani kuwa kinachowazwa ni ukweli. Kwa vyovyote vile mawazo hayana uhalisia kwa asilimia zote. Kwa hivyo sio busara kuyaamini hasa yale yanayokimbilia kupoteza furaha zetu.

Hisia
Hisia ni mlinzi wetu. Hisia huja kutukumbusha juu ya makosa tuliyowahi kuyafanya na kutuonya tusiyafanye tena. Hisia ni kitu kizuri kama kitachukuliwa kama mlinzi na sio kiongozi. Hisia kama vile hasira na hofu hutuamsha na kutukumbusha kuwa mambo yanaweza yakaenda tofauti na tunavyoyatarajia. Jambo hili sio baya. Maisha ya nje ya nafsi zetu huenda vile yanavyotaka wenyewe kwa hivyo lazima tujifunze kukubaliana nayo na pengine kukabiliana nayo bila kupoteza furaha zetu.

Roho
Hatuna mamlaka makubwa kuhusu roho. Tunachotakiwa kujua ni kuwa roho ni nguvu inayotuwezesha kuishi. Mara zote tunapokosa furaha nguvu hii hupungua. Hii ndio sababu inasemekana kuwa watu wasio na furaha huwahi kufa. Naamini kuna ukweli katika hili. Sio kufa peke yake ukikosa furaha unausababishia mwili ukosefu nguvu ya kuishi na kupambana na mazingira yake na hivyo kupelekea maradhi na kifo.

Nini faida za kuwa na furaha wakati wote?

Furaha ndio chanzo cha kila aina ya mafanikio. Mwandishi Napoleon Hill ameandika katika moja kitabu chake kuwa “Furaha huvuta kila aina ya utajiri”. Kulingana na Napoleon kuna tajiri kumi na mbili ambazo huvutwa na kitendo cha kuwa na furaha wakati wote.

Tajiri hizo ni hizi zifuatazo: 1. Akili tulivu 2. Nidhamu 2.Mahusiano bora. 3.Afya njema 4.Uhuru dhidi ya hofu 5.Kuwaelewa watu 6.Ushirikiano 7.Upendo 8.Kujifunza 9.Matumaini 10.Imani 11.Afya bora 12.Uhuru wa kiuchumi (Fedha)

Kama kwa namna yoyote unataka kufanikiwa katika maisha yako kwa kupata tajiri hizo hapo juu, Napoleon anashauri kuwa, furaha inatakiwa kuwa rafiki yako. Furaha kwa namna unavyoweza. Fanya kila kitu ukiwa na furaha ndani ya nafsi yako. Tabasamu wakati wote. Utafanikiwa.
 
Back
Top Bottom