JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 625
- 938
Siku ya Ulinzi wa Faragha ya Taarifa Binafsi (Data Privacy Day) inaadhimishwa kila Januari 28
Haki ya Faragha inawezesha Raia kufurahia Haki nyingine kama:
- Uhuru wa Mawazo
- Uhuru wa Kujieleza
- Uhuru wa Kukusanyika
Ni Msingi wa Jamii ya Kidemokrasia
Katika Nchi nyingi, Faragha inatambulika kama Haki ya Msingi ya Binadamu, na Sheria za Kulinda Taarifa Binafsi zipo ili kuilinda
Ibara ya 16 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema, "Kila Mtu anastahili kuheshimiwa na kupata Hifadhi kwa Nafsi yake, Maisha yake Binafsi na Familia yake na Unyumba wake, na pia Heshima na Hifadhi ya Maskani yake na Mawasiliano yake ya Binafsi"
Ili Watu washiriki kikamilifu Mitandaoni, wanahitaji kuamini Taarifa zao Binafsi zipo salama
Bila Kulinda Faragha, tunaweza kuwa hatarini kutengeneza Jamii isiyoweza Kujieleza kwa Uhuru, suala ambalo ni Ukiukwaji wa Haki za Binadamu
FARAGHA YA TAARIFA BINAFSI NI NINI?
Ni Haki ya Msingi ya Binadamu kwa Mujibu wa Ibara ya 12 ya Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa la Mwaka 1948
Inahusisha Wananchi kuwa na Udhibiti wa jinsi Taarifa zao Binafsi zinavyokusanywa, kuhifadhiwa na kutumika. Taarifa hizo ni pamoja na Jina, Jinsia, Namba ya Simu, Baruapepe, Makazi, Taarifa za Kiafya na Kifedha
Haki hii ambayo ipo Kikatiba pia inalindwa na Mikataba mbalimbali ya Kikanda ambayo Tanzania imeridhia
KWANINI HAKI YA FARAGHA NI MUHIMU?
Taarifa Binafsi zinaweza kutumika vibaya ikiwa hakuna Kanuni na Taratibu za kuziweka salama
Faragha inapotambulika kama Haki ya Msingi ya Binadamu, wale wasioiheshimu huwajibishwa
Mtu anayekosa Ulinzi wa Faragha ya Taarifa zake anaweza kushindwa kufurahia Haki nyingine kama Kutoa Maoni kwa Uhuru
FANYA HAYA KULINDA TAARIFA ZAKO BINAFSI
1) Kumbuka Mlinzi wa kwanza wa Taarifa zako ni Wewe. Unapotoa Taarifa zako Mtandaoni au nje ya Mtandao, unajiweka katika hatari zaidi ikiwa zitatumiwa vibaya
2) Epuka kubonyeza 'Link' usizozifahamu kwani Wahalifu wengi kwenye Mitandao hutumia mbinu hiyo kujaribu kuingilia Faragha yako
3) Sasisha (Update) Programu zako ili kuboresha Usalama wa Vifaa vyako vya Kidigitali na kujilinda dhidi ya mianya inayoweza kuathiri Faragha ya Taarifa zako
ZINGATIA YAFUATAYO KUIMARISHA ULINZI WA TAARIFA ZAKO
- Funga Akaunti zisizo na Matumizi: Akaunti zisizotumika na kusimamiwa ipasavyo Mitandaoni bado zinaweza kuwa na Taarifa Binafsi ambazo zinaweza kutumiwa vibaya
- Weka Nywila (Password): Fanya hivi katika Vifaa vyako vya Kidigitali na Akaunti zako za Mitandao ya Kijamii. Kumbuka kuwa na Nywila Imara na jitahidi kuhakikisha hazifanani
- Epuka 'WiFi' za Umma: Wahalifu wanaweza kuitumia kuingilia Kifaa chako kupitia 'WiFi' zisizo salama na kuingilia Faragha ya Taarifa zako
(i) Epuka Programu au 'App' ambazo hazieleweki: Asilimia kubwa zinachukua Taarifa zako bila ridhaa hivyo kuingilia Faragha yako
(ii) Tumia 'Two-Factor Authentification' pale unapoweza ili kujenga Usalama zaidi unapoingia kwenye Akaunti mbalimbali Mitandaoni
(iii) Weka Mikakati ya endapo utapoteza Simu au Kifaa chako cha Kidigitali ili Taarifa zako zibaki Salama
MUHIMU:
UKUSANYAJI TAARIFA BINAFSI: Ni muhimu kuwepo kipimo/kiwango cha Taarifa zinazochukuliwa
KWANINI TAARIFA ZAKO BINAFSI ZINACHUKULIWA?: Ili kulinda Faragha yako, usisite kuuliza Matumizi ya Taarifa zako pale unapohitaji kufanya hivyo. Ni HAKI yao kufahamu!
MATUMIZI SAHIHI YA TAARIFA: Taarifa zetu Binafsi hazitakiwi kutumika kwa Masuala mengine tofauti na lengo husika
ULINZI WA TAARIFA BINAFSI: Ni muhimu kuwepo na Miongozo kuhakikisha Taarifa zipo salama
UWAZI: Ukusanyaji wa Taarifa Binafsi usifanyike kisiri. Wananchi wafahamiwe kuhusu Michakato inayohusisha Taarifa zao
UWAJIBIKAJI: Yeyote anayehusika na Ukusanyaji wa Taarifa awajibishwe ikiwa Misingi ya Faragha haitazingatiwa
SOMA VIGEZO NA MASHARTI: Kabla hujakubali kutumia App au Tovuti husika, ni muhimu kusoma Vigezo vyake ili kujihakikishia usalama