NI NANI KAMA LOWASSA
1. Kalamu ninakushika, ili nipate andika,
Habari zipate fika, kwa watu wa kila rika,
Jambo moja mi nataka, ya moyoni kuanika,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
2. Sifa alijizolea, utumishi lotukuka,
Ofisi kaiachia, nchi nzima kazunguka,
Roho zetu kaokoa, baa njaa kutimka,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
3. Pia uwajibikaji, kasimamia nchini,
Ripoti za utendaji, katilia maanani,
Kwenye miji na vijiji, misaada kila dini,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
4. Hakika Edo jasiri, Mola kampa kipaji,
Kawazima wamisri, kwenye mradi wa maji,
Kilimo kinashamiri, kisa umwagiliaji,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
5. Kajenga kwa umahiri, umoja wa kitaifa,
Kafanya kazi vizuri, kwa juhudi maarifa,
Kwa matendo kahubiri, naitaja yake sifa,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
6. Kazi mbele aliweka, kuleta maendeleo,
Nchi ikaimarika, ikapata mwelekeo,
Kweli tulinufaika, kwa mazuri matokeo,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
7. Ni mzalendo shupavu, thabiti asiyeyumba,
Si kiongozi mabavu, na sio wa kujigamba,
Mtii mnyenyekevu, hakika Edo ni mwamba,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
8. Kumbuka aliyofanya, na mema aliyotenda,
Usije ukatawanya, yale aliyoyapanda,
Jaribu kuyakusanya, hakika utampenda,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
9.Sekondari kila kata, lijenga kote nchini,
Zahanati zikafata, mijini na vijijini,
Kwa juhudi katafuta, masoko nje na ndani.
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
10. Walimu tunakusifu, twasema wewe ni namba,
Aliokoa maelfu, kwa kutujengea nyumba,
Ni kwa wako ubunifu, bado amani yatamba,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
11. Hata shule za msingi, sasa hawakai chini,
Madawati yako mengi, alosambaza nchini,
Heri ikawa kwa wengi, karo ikushushwa chini,
Ni nani kama lowassa, kwa mema lotutendea.
12. Tamati nimefikia, kwa yale niliyowaza,
Nilosema zingatia, kweli Edo anaweza,
Ni mengi katufanyia, machache nimeeleza,
Ni nani kama lowassa, kwa mema ulio tutendea watanzania