Ujio wa CHADEMA Iringa: Tafsiri Yangu

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

1.jpg


CCM inayumba, kusema kingine ni kuwadanganya CCM, haitawasaidia.

Ndio, jahazi linapopoteza mwelekeo kinachofuatia ni kuyumba na hatimaye kuzama. CCM kama chama, kiko hatarini kuzama. Kuna ishara zinazoonekana.

Nimeishi Iringa kwa miaka saba sasa. Nikiri, kuwa sijapata kushuhudia maandamano makubwa ya wafuasi wa chama cha siasa kama yale ya CHADEMA Alhamisi iliyopita. Sijapata pia kushuhudia mkutano mkubwa wa chama cha siasa kama ule wa CHADEMA pale viwanja vya Mlandege.

Na kuna Wana- CCM wenye kubeza; " Ah, wale vijana wa CHADEMA ni wavuta bangi tu!" Ananiambia Mwana-CCM hapa Iringa. Nikamjibu; " Kama vijana wale wa CHADEMA kwa mamia wameweza kujipanga vile wakaudhuria maandamano kwa amani na hata kukaa mkutanoni wakiwasikiliza viongozi wao, basi, bangi ya siku hizi inawatia watu akili kuliko kuwalewesha!"

2.JPG


4.JPG


6.jpg


Na si tuliona, pale Mlandege, kulikuwa na akina mama watu wazima pia. Katika Tanzania hii, ukiona mikutano ya Chama cha siasa inaanza kuhudhuriwa na akina mama watu wazima, basi, hicho si chama cha kukibeza.

Ndio, kwa CCM, CHADEMA sio wa kubezwa. Wahenga walinena; mdharau kipele hushtukia ana jipu. Unapoona wananchi wanaandama kwa miguu kwa kilomita 5 hilo si jambo la kubeza. Unapoona wananchi wanatoka Tanangozi, Ilula na kwengineko kwenda Iringa kumsikiliza Dr Slaa na wenzake, hilo si jambo la kubeza hata kidogo. Hapo kuna jambo.

Na kwa CCM, si busara kukimbilia kuwaparamia CHADEMA bali kuyafanyia kazi mengi ambayo CHADEMA wametumia majukwaa kuishtaki CCM na Serikali yake kwa Wananchi. Na katika hili, kuna Watanzania wanaiona CHADEMA kama wingu nene la mvua lililotanda angani kwenye nchi yenye ukame. Hata kama wingu litapotea bila mvua kunyesha, lakini bado , kwao ndio matumaini waliyo nayo, kwa sasa.

CCM haina jingine, bali kufanya kazi ya ziada kulinusuru jahazi lake lisije kuzama. Na Iringa ilikuwa moja ya ngome za CCM kisiasa, si hivi leo ninavyoandika. Kuna mawimbi makubwa wanayokwenda nayo CHADEMA kwa sasa, na kama fasheni, wengi wanaelekea kuyafuata mawimbi hayo. Na hata ukimwuliza mtu kwanini? Anakujibu; " Chama ni CHADEMA tu!".

Wenye kujibu hivyo hawajui ni kwanini hasa wanayafuata mawimbi hayo. Lakini wanajua walichokiacha nyuma yao, ni CCM. Kuna wanaosema wazi; " Ah, CCM tumeichoka bwana!" Kwanini? Namwuliza jamaa wa mtaani; " Tumeichoka tu, basi!" Na kuna wanaosema mitaani; " CCM ni Chama Cha Mafisadi!"

Na hilo la mwisho ndio haswa ' msalaba' mzito waliojibebesha CCM, au labda wamebebeshwa. CCM ina lazima, sio tu ya kuutua msalaba huo, bali kuuchimbia shimo na kuuzika. Kwa namna gani? Si kwa kujivua gamba kama Chama, bali kuongoza juhudi za taifa zima kujivua gamba. Ndani yake kuna KATIBA MPYA, Miiko ya Uongozi, Kuheshimu Haki za Kibinadamu na mengineyo.

Maana, bila Taifa kujivua gamba, inaweza kesho ikaondoka CCM na wakaja CHADEMA. Kisha tukabaki tukisema; " Alaa, tulistaajabia ya Mussa, tumeyaona ya Firauni!"

Na katika yote haya, CCM isije ikasahau dhamana yake kwa taifa. Ndio, CCM ni chama tawala. Ni chama kilichobeba dhamana kubwa ya uongozi wa nchi. Ni ukweli huo unaofanya yanayotokea ndani ya CCM yatuhusu sote hata tusio wafuasi wa itikadi za vyama.

Na historia ni mwalimu mzuri. Aliyekuwa kada wa CCM na Katibu Mkuu wa chama hicho marehemu Horrace Kolimba ndiye aliyeanza kuusema ukweli juu ya mwelekeo wa CCM. Ni zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kolimba aliusema ukweli wake na akausimamia.

Alitamka hadharani, kuwa CCM imepoteza dira. Hata wakati huo, uongozi wa CCM uliikana kauli ya Kolimba. Kolimba alikuwa na ujasiri wa kuisimamia kauli yake hadi kufa kwake. Atakumbukwa daima kwa kauli na msimamo ule aliouonyesha.

Miaka mingi imepita tangu Kolimba atamke kauli ile. Tumeanza kusikia sauti nyingi zaidi zikitamka mambo yenye kufanana na yale aliyoyasema Kolimba. Alianza Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ikafika mahali Mwalimu hakuishia tu kuzungumza juu ya yanayotokea ndani ya chama chake. Mwalimu aliandika kitabu ili kuacha kumbukumbu ya kudumu juu ya alichotaka kusema.

Hata baada ya Mwalimu tumeanza kuwasikia makada wengine wa CCM wenye kutamka hadharani yale yenye kufanana na ya Kolimba na Mwalimu. Ni leo tu, tumesoma kauli ya Mzee Ibrahim Kaduma, kuwa CCM imepoteza mwelekeo.

Kwamba wana- CCM wenyewe wameanza kujihoji ni jambo la heri kwa chama hicho tawala. Wenye kuhoji yanayotokea ndani ya CCM wanafanya hivyo kwa mapenzi mema na chama chao, hata kama wanajiweka katika hatari ya kupigwa mihuri ya "upinzani' na kuhatarisha kutengwa kutoka kwenye kundi kuu.

Tunapozungumzia dhana ya kuimarisha demokrasia ya ndani ya vyama ( Intra-party democracy) si jambo la busara hata kidogo kujaribu kuzuia sauti zenye kuhoji, kudadisi na hata kupinga na kushutumu. Si busara hata kama wenye kuhoji na kudadisi ni kumi tu kati ya wanachama milioni moja.

Hata katika familia ya watoto wa tumbo moja wote hawawezi kuwa na fikra na mitazamo yenye kufanana. Kuzizima sauti hizo kunasaidia tu kuongeza manung'uniko na minong'ono ya chini chini. Zinachangia kuongezeka kwa harakati za chini kwa chini.

Manung'uniko, minong'ono na makundi yanaimarika pale ambapo wenye fikra na mitazamo tofauti wanapobanwa sana ndani ya chama na hata kufikia kukosa majukwaa ya kusemea. Ni pale watu hao wanapojisikia hofu ya kuchapwa bakora za chama na hata kutengwa kutoka kwenye kundi kuu. Hofu hiyo hupelekea nidhamu ya woga na watu kutoaminiana. Hupalilia zaidi hulka za kinafiki.

Wanachohitaji CCM kwa sasa ni kurudi kwenye misingi yao iliyopelekea kuundwa kwa Chama mama TANU na Afro-Shiraz na baadaye kuzaliwa kwa CCM. CCM irejee kwenye misingi yake ya miiko na maadili ya uongozi. Na irejee kwenye ahadi za mwanachama wa chama hicho kwa chama chake. Moja ya ahadi muhimu za mwana TANU na baadaye Mwana – CCM ni hii ifuatayo; " Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko".

Nakumbuka, Tambwe Hizza, aliyeingia CCM akitokea CUF alipata kutamka hadharani, kuwa walipokuwa upinzani kazi yao ilikuwa ni kutunga uongo. Alichomaanisha Tambwe Hizza ni kuwa kama alikuwa ni mmoja wa watunga uongo kwenye kambi ya upinzani, basi, kuondoka kwake kutoka upinzani na kujiunga na CCM kulikuwa ni jambo la heri kwa aliowaacha huko kwenye upinzani. Bila shaka waliobaki huko walifurahia kwa kuondokewa na mtu mwongo.

Imefika wakati kwa Wana-CCM kuacha hofu ya kuambizana ukweli. Tulio nje tunakiona chama kinachoyumba. Rushwa na ufisadi ndani ya chama zinakiyumbisha chama. Ndani ya CCM kuna wanaoliona hilo pia. Baadhi yao kwa unafiki watamwambia nahodha; "Kanyaga mafuta baba!" Huku wakijua kinakoelekea chombo siko.

Na kila jahazi huwa na panya wake. Wenye kumsisitiza nahodha akanyage mafuta mara nyingi huwa na tabia za panya wa jahazini. Jahazi likianza kuzama, panya wake huwa wa kwanza kurukia majini na kukiacha chombo kikizama.

Inahusu umuhimu wa kusema yaliyo ya kweli. Na kuna aina tatu za wasema kweli. Kuna anayeusema ukweli na kujificha. Huyu anaweza kuwa na sababu za msingi za kutaka kuusema ukweli na kujificha. Ndiyo huyu atakayekwambia ukweli juu ya jambo fulani kisha kukutamkia; "Tafadhali jina langu lihifadhi".

Aina ya pili ya msema ukweli ni yule anayeusema ukweli na kisha kuukimbia. Atausema ukweli, akibanwa sana na wenzake, basi, ghafla ataukanusha ukweli aliousema hadharani. Atauruka ukweli wake mwenyewe. Atayakanusha maneno yake hata kama yamerikodiwa kwenye kaseti na kila mmoja akayasikia. Atang'aka, atakikimbia kivuli chake. Hii inatokana na woga unaozaa unafiki.

Lakini mwisho, kuna huyu anayeusema ukweli na kisha kuusimamia kwa lolote lile. Inyeshe mvua liwake jua. Ni watu wa aina ya akina Kolimba. Jamii yetu ilihitaji kuwa na watu wengi zaidi wenye kulikaribia kundi hili la tatu la wasema ukweli. Na siku zote , ukweli ni mzigo mzito, haupaswi kubebwa. Ukweli husambazwa.

Maggid,
Iringa, Jumapili, Mei 22,2011
 
well said Maggid ! siku hizi nimekuwa mpenzi wa makala zako kweli kweli kiasi kwamba nikiziona tu huwa nakimbilia kuzifungua,Nape yupo humu ndani natumai hata yeye atakuja na kusoma hapa na salamu atazipeleke hadi chumabi kwani yeye yupo sebuleni, na wajue kabisa kuwa huu moto uliowaka hautazimika kamwe hadi jahazi lizame au wananchi waweze kufaidi nation cake yao
 
ukwel ubak kuwa ukwel,mfano nimejivua gamba bila tendo kamil pana ueleweka!ccm wataalam wa ngonjera za uwongo hawajui mtz wa leo s wajana na wajua wataumbuaka na kuumbuana sana.
 
Good observation Maggid.

Tafsiri yangu kwa thread yako....

Hiki (cha kwako) ni kama kilio cha mtu aliaye nyikani ambaye sauti yake ina mawimbi makubwa yenye kusheheni sympathy kwa CCM.

Sauti imesheheni ujumbe uliojaa hofu ya CCM kuanguka.
Si ujumbe wa wa kuwapa matumaini mapya wananchi watambue kuwa neema yawezekana with or without CCM!

Ukweli ni kwamba there's no way back in for CCM come 2015....inaweza isiwe Chadema lakini anything other than CCM (and this does not exclude those uniformed and usually quiet guys in the barracks!).

Huo ndio ukweli and let's face it!
 
magid you said the truth and it shows that peoples power is working well...
People need reforms and they hope that the redemption will come from cdm only!!!
 
Siku nyingine Maggid anajivua gamba na kuamua kuongea ukweli!

Nafikiri amegundua kuwa kuendelea kumfariji mgonjwa mwenye terminal illness kwa kumwambia kuwa ugonjwa wako ni mdogo, au utapona soon, au hata kumwambia kuwa wewe si mgonjwa, hakutafanya mgonjwa huyo aepuke kifo mapema. Cha muhimu ni kumuambia kuwa una ugonjwa usiotibika na hatma yako itakuwa ni kufa hivyo aandae hatma yake baada ya kufa kwa kufanya ibada ili afikie mahali pema ni jambo muhimu.

CCM isipojitengezea legacy kwa kuwaachia watanzania demokrasia ya kweli isiyo na chakachua kwa kuwaacha wananchi waandae katiba yao wenye, basi itakuwa imekosa nafasi adhimu sana kwa chama kitakachokuja baada yake. Ni dhahiri kuwa CCM haiwezi kuendelea kutwaa madaraka kwa chakachua kwa kutumia polisi na mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na risasi za moto na wakati mwingine kuwadhaliisha makamanda wa JWTZ kujishusha kwenye level ya propaganda za kutisha wananchi kama alivyotumiwa Shimbo kulidhalilisha jeshi letu la wananchi ambalo wengi tunaliamini kuliko hata amiri jeshi wake mkuu.

Kuna wakati itabidi wachague ama kuendelea kutawala miti kwa kuangamiza raia wasiowakubali au kukubaliana na matakwa ya raia kupitia kura zao. Viongozi wa CCM wanatakiwa kujua kuwa, wapo wanaoweza kuchaguliwa na wananchi bila ya kuwa ndani ya CCM, neno CCM limekuwa sawa mumiani(nyinya damu) miongoni mwa watanzania, kuwabadili waamini vinginevyo itawachukua miaka mingine hamsini.
 
CCM hawawezi kubadilika majini wanayoyafuga yanahitaji kiasi kikubwa sana cha pesa za walipa kodi. Hamuoni jinsi wanavyozuia njia kuu za uchumi zisimilikiwe na Watanzania wenyewe?

Angalia kuanzia umeme ni jinsi gani wanavyotumia nguvu kubwa kuhalalisha ujambazi, hatujaongelea simu, reli barabara nk. Nchi yoyote haiwezi kuendelea kama njia zake kuu za uchumi zimeshikwa na majini ya mafisadi.


Hivi leo JK alikuwa na kazi kubwa ya kuyanyamazisha majini kwa sababu yamemshinda nguvu na hana uwezo, dawa yake ni kumng'oa na majini yake pale Magogoni.
 
Maggid, umesema ukweli.

Lakini ushauri wako, ninavyoamini mimi, hautasaidia chochote. CCM imeshapita kipindi hicho cha kujirudi na kuanza upya. There is NO WAY your party is gonna do that, NEVER.

CCM has only two choices:

1. kujiongezea nguvu na kuwa "tyranny" ya ki-imla (dictatorship). Hili haliwezekani ktk ulimwengu wa sasa, limepitwa na wakati. Nobody will let them kill hundreds of people.
2. Kuufuata mtiririko wa mafuriko ya mabadiliko na kutengeneza njia ili mafuriko yachukue mkondo wake. Kwa kufanya hivi chama kinaweza kusalimika, lakini CDM watachukua nchi.

Otherwise, hakuna njia nyingine itakayowasaidia.
 
Ukweli haufichiki daima, najua macho na ubongo wako maggid siku zote unaona na kujua hali halisi lakini wakati mwingine unakatisha tamaa, ukiwaonea aibu ngedere bro utavuna mabua, hii nchi tufumbuane macho it is of no good kuchekelea wanaoleta masihara na maisha yetu.

Siasa ni shule, hospitali, barabara, mshahara, nyumba, mahakama na kila kitu chako usiiache mikononi mwa manyang'au, join us bro, today u did good analytical work.
 
Ujumbe mzuri, kama ccm ni wasikivu na waelewa wataufanyia kazi ushauri huu!
 
Nakumbuka, Tambwe Hizza, aliyeingia CCM akitokea CUF alipata kutamka hadharani, kuwa walipokuwa upinzani kazi yao ilikuwa ni kutunga uongo. Alichomaanisha Tambwe Hizza ni kuwa kama alikuwa ni mmoja wa watunga uongo kwenye kambi ya upinzani, basi, kuondoka kwake kutoka upinzani na kujiunga na CCM kulikuwa ni jambo la heri kwa aliowaacha huko kwenye upinzani. Bila shaka waliobaki huko walifurahia kwa kuondokewa na mtu mwongo.

makamba akamsajii tambwe hiza katika timu yake(ccm) kwa kumuona ni mtunga uongo mzuri, akawa ni vuvuzela namba moja, sijui yuko wapi siku hizi?
 
hongera majjid kwa makala yako naomba niongezee hapo kwa kutaja majina hiyo aina ya pili ya wasema ukweli ambao wakibanwa wanakataa kabisa ndiyo ndg zetu kina mwakyembe,hawana misimamo ni wa kuwaogopa sana kwani waweza fanya kazi za kuwatumikia mabwana wawili at per
 
makamba akamsajii tambwe hiza katika timu yake(ccm) kwa kumuona ni mtunga uongo mzuri, akawa ni vuvuzela namba moja, sijui yuko wapi siku hizi?

hata mimi najiuliza yuko wapi Tambwe mtu mwenye busara ndani ya CCM.

mgao wa umeme umemfanya maggid aseme ukweli.......shida kipimo
 
Hapa hakuna habari mpya kwangu, kama Maggid mpaka aone mkutano mkubwa kwao Iringa ndio ajuwe ccm haitakiwi na Watanzania, basi natilia shaka na upeo wake. Watanzania hawaitaji tena makala za waandishi wajanja wajanja kudai haki zao, watu wameshajitambuwa.
 
Back
Top Bottom