Tokea Mh. Lissu anusurike kwenye shambulio dhidi ya uhai wake siku ashara na kitu zilizopita, kumekuwepo na sauti kadhaa zinazodai au zinazotaka tukio hilo lichunguzwe na wachunguzi 'huru' kutoka nje ya nchi.
Sababu yake kubwa ni kwamba vyombo vya ndani [ya nchi] vya usalama haviko huru kuweza kufanya uchunguzi huo kwa sababu vyenyewe ndivyo vinavyoshukiwa kupanga na kutekeleza jaribio hilo ili kutimiza matakwa ya mtu au watu wa huko serikalini na kwenye CCM.
Hisia hizo [za kuishuku na kuituhumu] nazielewa. Hivyo watu wanaotaka kuona wachunguzi huru wakichunguza nao nawaelewa.
Ila, kuna vitu vinanitatiza kidogo kuhusu huo u huru wa hao wachunguzi na utayari wa kambi ya Lissu na kambi ya serikali kuyakubali matokeo ya huo uchunguzi wao endapo utatokea.
La kwanza, ni nani atayeingia gharama za hao wachunguzi?
Tuseme CHADEMA na wafadhili wao ndiyo wataingia hizo gharama.
Kama hivyo ndo itavyokuwa, je, hao wachunguzi watakuwa huru kiasi gani ilhali wanalipwa na upande wa mnusurika wa jaribio?
CHADEMA kweli inaweza kuwalipa hao wachunguzi huru halafu hao wachunguzi watoe uchunguzi ambao ni kinyume na madai ya CHADEMA [kwamba serikali kupitia vyombo vyake vya usalama ndiye mhusika]? Kama wataletwa na CHADEMA maana yake ni kwamba wao ni waajiriwa wa hicho chama. Akili yangu haioni ni jinsi gani hao wachunguzi huru wanaweza kutoa matokeo yaliyo kinyume na hisia za watu waliowaajiri.
Je, serikali nayo ipo tayari kweli kuyakubali matokeo ya hao wachunguzi huru ambao huenda wakalipwa na hicho chama pinzani?
Na vipi kwa mfano serikali ikubali ujio wa hao wachunguzi na iingie gharama kwa kazi watayoifanya, je, CHADEMA ipo tayari kuyapokea na kuyakubali matokeo ya huo uchunguzi hata kama yakiwa tofauti na vile wao wadhaniavyo?
Kumbuka, kama serikali ndiyo itayoingia gharama za hao watu maana yake ni kwamba watakuwa wanaitumikia serikali iliyopo madarakani ambayo ni ya CCM.
Kwa mtaji huo hao wachunguzi huru watakuwa wapo huru kiasi gani?
Hili suala ni gumu kwa kweli. Kila ninapowaza na kuwazua sipati majibu.
Sijui nyie wadau mnalionaje hilo suala.
Jumapili njema.